35.Suurat Faatír |
Imeshuka Makka | Ina aya 45 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba
wa mbingu na ardhi, aliye wafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili,
na tatu- tatu, na nne-nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
1
2. Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia
watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye.
Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
1
3. Enyi watu! Kumbukeni neema
za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiye kuwa Mwenyezi
Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu
ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
3
4. Na wakikukanusha, basi walikwisha
kanushwa Mitume kabla yako. Na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
4
5. Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni
maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.
5
6. Hakika Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye
analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni.
6
7. Walio kufuru watakuwa
na adhabu kali; na walio amini na wakatenda mema watapata msamaha na ujira
mkubwa.
7
8.
8. Je! Yule aliye pambiwa a'mali zake mbaya na akaziona ni njema
- basi hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye.
Basi nafsi yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua
wanayo yafanya.
8
9. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue
mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada
ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo kutakavyo kuwa kufufuliwa.
9
10. Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda
neno zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga vitimbi vya maovu
watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu.
10
11. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha akakufanyeni
mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala hazai, ila
kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala hapunguziwi
katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi kwa
Mwenyezi Mungu.
11
12. Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye
ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari
zote mnakula nyama mpya (isiyo chacha). Na mnatoa mapambo mnayo yavaa.
Na unaona ndani yake marikebu zinakata maji ili mtafute fadhila zake, na
ili mpate kushukuru.
12
13. Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza
mchana katika usiku. Na amelifanya jua na mwezi kutumikia. Kila kimojapo
kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi.
Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake hawamiliki hata ugozi wa
kokwa ya tende.
13
14. Mkiwaomba hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia
hawakujibuni. Na Siku ya Kiyama watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakaye
kupa khabari vilivyo kama Yeye Mwenye khabari.
14
15. Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha,
Msifiwa.
15
16. Akitaka atakuondoeni na alete viumbe vipya.
16
17. Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
17
18. Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine.
Na aliye topewa na mzigo wake akiomba uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo,
na angamwomba jamaa yake. Hakika wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao
Mlezi kwa ghaibu, na wanashika Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa
kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.
18
19. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani.
19
20. Wala giza na mwangaza.
20
21. Wala kivuli na joto.
21
22.
22
23. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.
23
24. Hakika Sisi tumekutuma
wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri na mwonyaji. Na hapana umma wowote ila
ulipata mwonyaji kati yao.
24
25. Na wakikukanusha basi walikwisha wakanusha
walio kuwa kabla yao. Mitume wao waliwajia kwa dalili wazi wazi na kwa
maandiko na Kitabu chenye nuru.
25
26. Kisha nikawakamata walio kufuru.
Basi kuchukia kwangu kulikuwaje?
26
27. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu
ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi
mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi
mbali mbali, na myeusi sana.
27
28. Na katika watu, na wanyama, na mifugo,
pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni
mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye
kusamehe.
28
29. Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika
Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao
hutaraji biashara isiyo bwaga.
29
30. Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu,
na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe
Mwenye shukrani.
30
31. Na hayo tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli
yenye kusadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja
wake ni Mwenye khabari na Mwenye kuona.
31
32. Kisha tumewarithisha Kitabu
hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliye jidhulumu
nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliye tangulia katika mambo ya
kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.
32
33. Mabustani
ya milele watayaingia. Huko watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na nguo
zao humo ni za hariri.
33
34. Na watasema: Alhamdulillahi, Sifa njema zote
ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi
bila ya shaka ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani.
34
35. Ambaye kwa fadhila
yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu haitugusi taabu wala humu hakutugusi
kuchoka.
35
36. Na walio kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu, hawahukumiwi
wakafa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila
mwenye kuzidi ukafiri.
36
37. Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi!
Tutoe tufanye mema sio yale tuliyo kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni
umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na akakujieni Mwonyaji? Basi
onjeni! Kwani walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
37
38. Kwa hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliomo
vifuani.
38
39. Yeye ndiye aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na anaye
kufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii
kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii
ila khasara.
39
40. Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao
waomba badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika
ardhi? Au wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa
hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini madhaalimu hawaahidiani wao kwa
wao ila udanganyifu tu.
40
41. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia
mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipo
kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye kusamehe.
41
42. Na waliapa kwa Mwenyezi
Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila ya shaka watakuwa
waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia mwonyaji
hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki,
42
43. Kwa kutakabari kwao katika
nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe
aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale? Basi hutapata
mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika
mwendo wa Mwenyezi Mungu.
43
44. Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi
ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi
kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni
wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.
44
45. . Na
lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo yachuma, basi
asingeli muacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia
mpaka ufike muda maalumu. Basi ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kuwaona waja wake baraabara.
45
Sura Nyingine | Faharasa |