43.Suuratul Azzukhruf |
Imeshuka Makka | Ina aya 89 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. H'a Mim
1
2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.
2
3. Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu.
3
4. Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni
tukufu na yenye hikima.
4
5. Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio
pita mipaka kwa ukafiri?
5
6. Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
6
7. Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
7
8. Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa
watu wa zamani umekwisha pita.
8
9. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka
watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,
9
10. Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani
yake njia mpate kuongoka.
10
11. Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi,
na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.
11
12. Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na
akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.
12
13. Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola
wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya
huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.
13
14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
14
15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu
ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.
15
16. Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na
akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?
16
17. Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi
Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.
17
18. Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema
kwa bayana...?
18
19. Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni
wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao
watahojiwa!
19
20. Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi.
Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
20
21. Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia
hicho?
21
22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini
makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.
22
23. Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu
wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu
wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao.
23
24. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko
mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa.
24
25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha!
25
26. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika
mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu,
26
27. Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa.
27
28. Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake
ili warejee.
28
29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki
na Mtume aliye bainisha.
29
30. Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika
tunaukataa.
30
31. Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa
katika miji miwili hii?
31
32. Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia
baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao
juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe
wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
32
33. Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia
wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao
pia wanazo pandia,
33
34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake,
34
35. Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha
ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.
35
36. Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa
ndiye rafiki yake.
36
37. Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
37
38. Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na
wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe!
38
39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana
katika adhabu.
39
40. Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu
na waliomo katika upotofu ulio wazi?
40
41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao.
41
42. Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza
juu yao.
42
43. Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye
Njia Iliyo Nyooka.
43
44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja
ulizwa.
44
45. Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya
miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani?
45
46. Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni
na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa
walimwengu wote!
46
47. Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
47
48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi
kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
48
49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile
ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
49
50. Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
50
51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu!
Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu?
Je! Hamwoni?
51
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema
waziwazi?
52
53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika
pamoja naye wakamwandama?
53
54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa
watu wapotovu.
54
55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
55
56. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
56
57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele.
57
58. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia
mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
58
59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya
ni mfano kwa Wana wa Israili.
59
60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika
ardhi wakifuatana.
60
61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie
shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
61
62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri.
62
63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni
na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni
Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.
63
64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu
Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
64
65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao.
Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
65
66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui?
66
67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa
wachamngu.
67
68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
68
69. Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.
69
70. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.
70
71. Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo
ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo
milele.
71
72. Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
72
73. Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.
73
74. Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.
74
75. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
75
76. Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.
76
77. Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako
Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
77
78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa
mnaichukia Haki.
78
79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha.
79
80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi!
Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
80
81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa
kwanza kumuabudu.
81
82. Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi,
na hayo wanayo msifia.
82
83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku
yao waliyo ahidiwa.
83
84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye
ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
84
85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani
yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.
85
86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea
mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
86
87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi
Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
87
88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni
watu wasio amini.
88
89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.
89
Sura Nyingine | Faharasa |