57.Suuratul Al H'adiid |
Imeshuka Madina | Ina aya 29 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Kinamsabihi kumtakasa Mwenyezi Mungu kila kiliomo ndani ya mbingu
na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
1
2. Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha.
Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu.
2
3. Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhaahiri
na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.
3
4. Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha
akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo
toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye
yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo
yatenda.
4
5. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote yanarejeshwa
kwa Mwenyezi Mungu.
5
6. Anaingiza usiku katika mchana, na anaingiza mchana katika usiku.
Na Yeye ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani.
6
7. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyo
kufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walio amini miongoni mwenu,
na wakatoa, wana malipo makubwa.
7
8. Na mna nini hata hamumuamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anakuiteni
mumuamini Mola wenu Mlezi? Naye amekwisha chukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi
ni Waumini.
8
9. Yeye ndiye anaye mteremshia mja wake Aya zinazo bainisha wazi
ili akutoeni gizani muingie kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu
ni Mpole, Mwenye kurehemu.
9
10. Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali
urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu
wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa
zaidi kuliko wale ambao walio toa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi
Mungu amewaahidia wema. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
10
11. Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie
mardufu, na apate malipo ya ukarimu.
11
12. Siku utakapo waona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru
yao iko mbele yao, na kuliani kwao: Furaha yenu leo - Bustani zipitazo
mito kati yake mtakaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
12
13. Siku wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo waambia walio
amini: Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Waambiwe: Rejeeni
nyuma yenu mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani
yake mna rehema, na nje upande wake wa mbele kuna adhabu.
13
14. Watawaita wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia:
Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na
matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi
Mungu, na mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu.
14
15. Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, wala kwa wale walio kufuru.
Makaazi yenu ni Motoni, ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!
15
16. Je! Wakati haujafika bado kwa walio amini zikanyenyekea nyoyo
zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyo teremka? Wala wasiwe kama
walio pewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao
zikawa ngumu, na wengi wao wakawa wapotovu.
16
17. Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake.
Tumekubainishieni Ishara ili mpate kuzingatia.
17
18. Kwa hakika wanaume wanao toa sadaka, na wanawake wanao toa sadaka,
na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, watazidishiwa mardufu na watapata
malipo ya ukarimu.
18
19. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio Masidiqi
na Mashahidi mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na nuru yao.
Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
19
20. Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo,
na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto.
Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha
hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu
kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia
si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.
20
21. Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake
ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Mwenyezi Mungu
na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.
21
22. Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha
andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu
ni mepesi.
22
23. Ili msihuzunike kwa kilicho kupoteeni, wala msijitape kwa alicho
kupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna akajifakhirisha.
23
24. Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili.
Na anaye geuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
24
25. Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha
Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha
chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue
anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu Mwenye kushinda.
25
26. Na bila ya shaka tulimtuma Nuhu na Ibrahim, na tukaweka katika
dhuriya zao Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walio ongoka, na
wengi katika wao ni wapotovu.
26
27. Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na tukamfuatisha
Isa bin Mariamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za walio
mfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi
hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata
inavyo takiwa kuufuata. Basi wale walio amini katika wao tuliwapa ujira
wao. Na wengi wao ni wapotovu.
27
28. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake,
atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru
ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
28
29. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya
fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.
29
Sura Nyingine | Faharasa |