60.Suuratul Al Mumtah'inah |
Imeshuka Madina | Ina aya 13 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Enyi mlio amini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki
mkiwapa mapenzi, na hali wao wamekwisha ikataa haki iliyo kujieni, wakamfukuza
Mtume na nyinyi kwa sababu mnamuamini Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu.
Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu,
mnafanya urafiki nao kwa siri, na Mimi nayajua mnayo yaficha na mnayo dhihirisha.
Na mwenye kufanya hayo kati yenu basi ameipotea njia ya sawa.
1
2. Wakikuwezeni wanakuwa maadui zenu, na wanakukunjulieni mikono
yao na ndimi zao kwa uovu. Na wanapenda muwe makafiri.
2
3. Hawatakufaeni jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama. Mwenyezi
Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
3
4. Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwenu kwa Ibrahim na wale walio
kuwa pamoja naye, walipo waambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi
na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha
dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi
Mungu peke yake. Isipo kuwa kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika
nitakuombea msamaha, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi
Mungu. Mola wetu Mlezi! Juu yako tumetegemea, na kwako tumeelekea, na kwako
ndio marejeo.
4
5. Mola wetu Mlezi! Usitufanyie mtihani kwa walio kufuru. Na tusamehe,
Mola wetu Mlezi. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
5
6. Kwa yakini umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao, kwa anaye
mtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kugeuka basi hakika
Mwnyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
6
7. Asaa Mwenyezi Mungu akatia mapenzi baina yenu na hao maadui zenu,
na Mwenyezi Mungu ni Mweza, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu.
7
8. Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao
hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wafanyao uadilifu.
8
9. Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na wale walio
kupigeni vita, na wakakutoeni makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu.
Na wanao wafanya hao marafiki basi hao ndio madhaalimu.
9
10. Enyi mlio amini! Wakikujilieni wanawake Waumini walio hama, basi
wafanyieni mtihani - Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi Imani yao.
Mkiwa mnawajua kuwa ni Waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Wanawake
hao si halali kwa hao makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake
Waumini. Na wapeni hao wanaume mahari walio toa. Wala hapana makosa kwenu
kuwaoa mkiwapa mahari yao. Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo
cha ndoa zenu. Na takeni mlicho kitoa, na wao watake walicho kitoa. Hiyo
ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu anayo kuhukumuni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kujua, Mwenye hikima.
10
11. Na akitoroka yeyote katika wake zenu kwenda kwa makafiri, tena
ikatokea mkapata ngawira, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha
mahari waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
11
12. Ewe Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba
hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini,
wala hawatawauwa watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe
baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi
peana nao ahadi, na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwingi maghfira, Mwenye kurehemu.
12
13. Enyi mlio amini! Msiwafanye rafiki zenu watu ambao Mwenyezi Mungu
amewakasirikia. Hao wamekwisha kata tamaa ya Akhera, kama makafiri walivyo
wakatia tamaa watu wa makaburini.
13
Sura Nyingine | Faharasa |