Maelezo: Suuratul Yunus |
(1) Mwenyezi Mungu ameumba viumbe vyote kwa vipindi sita, na vipindi hivi ni viwango vya mamilioni ya makarne na makarne. Na hivyo ndivyo vinavyo itwa Siku Sita. Na katika kila nguzo za ulimwengu zipo Ishara wazi zilizo zagaa za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Miongoni mwa hizi, ni hivi kufanywa jua na mwezi na nyota kunyenyekea kwa faida ya binaadamu. Na kadhaalika kupishana zamu usiku na mchana, na kuwa mchana unaingilia kiza cha mbingu. Na umetajwa usiku mbele kwa kuwa kiza ndio asli. Ama mchana umezuka kwa kuathirika kwa mwangaza wa jua katika anga la ardhi, ambayo hiyo ardhi inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia ili ipate mwangaza wa jua, mara upande huu na mara upande huu. |
(1) Aya hii ya 5 inahakikisha ukweli wa kisayansi ambao haukujuulikana na hiyo sayansi ila hivi mwishoni. Hapo kwanza haukujuulikana, nao ni kuwa jua ni umbo lenye kuwaka moto, na ndio chanzo cha nguvu za kufanyia kazi zote, kwa Kiarabu huitwa T'aaqa, na kwa Kiingereza Energy, na kwa Kiswahili cha sasa Nishati. Katika nguvu hizo ni huo Mwangaza na Joto. Ama mwezi hauwaki moto, bali unarudisha mwangaza wa jua, kama kioo, kwa hivyo huonekana una nuru. Kwa hivyo Subhanahu ameeleza kuwa jua lina mwangaza wa asli, na mwezi unatoa nuru tu. Na Aya hii imeashiria hakika ya nyendo za falaki, nayo ni kuwa mwezi unaizunguka ardhi, na kila siku unakuwa katika mahala fulani kwa mintarafu ya dunia. Ukimaliza mzunguko wake ndio unatimia mwezi, huu wa siku 30 au 29. Kwa hivyo tunaweza kujua kiasi cha mwaka, na kwa hivyo twaweza kujua hisabu za miaka, miezi na siku. |
(1) Inaonyesha Aya hii tukufu kuwa mwili wa Firauni utabaki umehifadhiwa ili watu wauone, na wapime kwa macho yao hali ya ule mzoga wa yule aliye kuwa akijiona ni mungu, na akiwaambia watu wake wanao mnyenyekea: Hamna mungu ila mimi! Kadhaalika tujue kuwa kutoka Wana wa Israili katika nchi ya Misri kulikuwa mwishoni mwa karne ya kumi na tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s., katika enzi ya mmoja wa Mafirauni wa Ukoo wa kumi na tisa, naye ni Minfitah mwana wa Ramsis wa Pili, ambaye ndiye aliye wakandamiza Wana wa Israili akawalazimisha wamjengee Jiji la ufalme wake. Uvumbuzi wa machimbo ya vitu vya kale wa hivi karibuni umedhihirisha kuwa jina la mji huo ulio funikika chini ya ardhi, ni "Bur'amsis". Kulikuwa kutoka kwa Wana wa Israili pamoja na Musa ni kwa ajili ya wito wa Tawhidi, Umoja wa Mwenyezi Mungu, na kuikata shemere ya Firauni iliyo wadhalilisha, na ikawakutisha adhabu ya mwisho. Na ilikuwa haijuulikani na Waarabu ambao hawajui kusoma na kuandika, wala kwa wengineo, kwamba mwili wa Firauni huyu ungalipo mpaka hii leo. Lakini Qur'ani imeyataja hayo, na ukweli wake umethibiti mwaka 1900 B.K., yaani karne kumi na tatu baada ya kuteremka Qur'ani. Je, hii si dalili ya kuwa imetoka kwa Mungu? |