Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul H'ujuraat

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Enyi mlio amini! Msitangulie na kulikata jambo lolote la kidini na la kidunia bila ya kukuamrisheni Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na jiwekeeni kinga ya nafsi zenu isikupateni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata sharia yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia baraabara yote mnayo yasema, ni Mwenye kuyajua vilivyo mambo yote.
Rudi kwenye sura

* 2. Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii anapo sema na nyinyi mnasema. Wala msipambanishe sauti zenu na sauti yake, kama mnapo semezana nyinyi kwa nyinyi, kwa kuchelea visiharibike vitendo vyenu bila ya nyinyi wenyewe kutambua.
Rudi kwenye sura

* 3. Hakika wanao teremsha sauti zao katika baraza ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumtukuza yeye, hao peke yao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Kwa wengineo si hivyo. Nao watapata msamaha mkubwa kufutiwa madhambi yao, na thawabu zilizo fika ukomo wa kufika kwake.
Rudi kwenye sura

* 4. Hakika hao wanao kuita kwa makelele nawe uko vyumbani mwako wengi wao hawafahamu yanayo takikakana kukuhishimu na kukutukuza kwa makamo yako.
Rudi kwenye sura

* 5. Na lau kuwa hao wangeli ngojea, kwa kukufanyia adabu, mpaka ukatoka, bila ya shaka ingeli kuwa ni bora zaidi katika Dini yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kusamehe, Mwenye rehema kunjufu.
Rudi kwenye sura

* 6. Enyi mlio amini! Akikujieni mtu ambaye yuko nje ya sharia ya Mwenyezi Mungu akakupeni khabari yoyote, basi chungueni mjue ukweli wake, kwa kuchelea msije mkawaletea watu madhara, kwa kutojua hali yao. Hapo tena baada ya kwisha dhihiri kuwa hawana makosa mkaingia katika majuto ya daima, mkatamani yasingeli kuwa.
Rudi kwenye sura

* 7,8. Na jueni, enyi Waumini, kwamba Mtume yuko nanyi. Basi mkadirieni kama anavyo stahiki kadiri yake, na msadikini. Lau yeye angeli wafuata walio wachache wa Imani kati yenu katika mambo mengi, basi hapana shaka mngeli ingia katika mashaka na hilaki. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezesha Imani wale walio kamilika katika nyinyi, na akaipamba katika nyoyo zenu. Basi jilindeni na kujipamba na yasiyo takikana. Na amekufanyeni mchukie kukufuru neema za Mwenyezi Mungu, na kutokana na sharia zake, na kwenda kinyume na amri zake. Hao tu, peke yao, ndio wanao ijua njia ya uwongofu na wameishikilia. Na hiyo ni fadhila tukufu na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu juu yao. Na Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake, ni Mwenye hikima ya kupita mpaka katika kuendesha kila jambo.
Rudi kwenye sura

* 7,8. Na jueni, enyi Waumini, kwamba Mtume yuko nanyi. Basi mkadirieni kama anavyo stahiki kadiri yake, na msadikini. Lau yeye angeli wafuata walio wachache wa Imani kati yenu katika mambo mengi, basi hapana shaka mngeli ingia katika mashaka na hilaki. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezesha Imani wale walio kamilika katika nyinyi, na akaipamba katika nyoyo zenu. Basi jilindeni na kujipamba na yasiyo takikana. Na amekufanyeni mchukie kukufuru neema za Mwenyezi Mungu, na kutokana na sharia zake, na kwenda kinyume na amri zake. Hao tu, peke yao, ndio wanao ijua njia ya uwongofu na wameishikilia. Na hiyo ni fadhila tukufu na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu juu yao. Na Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake, ni Mwenye hikima ya kupita mpaka katika kuendesha kila jambo.
Rudi kwenye sura

* 9. Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yanapigana, basi enyi Waumini, yapatanisheni. Ikiwa moja ndilo linalishambulia la pili, na likakataa kupatanishwa, basi lipigeni hilo linalo shambulia, mpaka lirejee kwenye hukumu ya Mwenyezi Mungu. Likirejea basi wapatanisheni kwa insafu. Na fanyeni uadilifu baina ya watu wote katika kila jambo. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wenye kufanya uadilifu.
Rudi kwenye sura

* 10. Hakika wote wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni ndugu, Imani imezifanya nyoyo zao pamoja. Basi patanisheni baina ya ndugu zenu kwa kufuata udugu wa Imani. Na jiwekeeni nafsi zenu kinga cha kukinga adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri yake, na kuepuka anayo yakataza, na huku mkitaraji Mwenyezi Mungu akurehemuni kwa uchamngu wenu.
Rudi kwenye sura

* 11. Enyi mlio amini! Wanaume katika nyinyi wasiwadharau wanaume wenginewe, huenda hao mbele ya Mwenyezi Mungu wakawa bora kuliko wao. Wala wanawake Waumini wasiwadharau wanawake wenzao, huenda pengine wakawa hao ni bora kwa Mwenyezi Mungu kuliko wao. Wala msifanye kuaibishana nyinyi kwa nyinyi, wala mtu asimwite mwenzie kwa jina la kumuudhi. Ni uovu mno kwa Waumini kutajwa kwa upotovu baada ya kwisha sifika kwa Imani. Na wasio rudi wakaacha waliyo katazwa, basi hao peke yao ndio walio jidhulumu nafsi zao na wakawadhulumu wengineo.
Rudi kwenye sura

* 12. Enyi mlio amini, jitengeni mbali na wingi wa kudhania dhana mbovu kwa watu wa kheri. Kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi zinazo stahiki adhabu. Wala msiwe mkitafuta aibu za Waislamu. Wala msisengenyane, yaani kumsema mtu nyuma yake kwa jambo linalo muudhi. Hebu yupo yeyote kati yenu anaye penda kula nyama ya nduguye aliye kufa? Bila ya shaka hayo yanakuchukizeni! Basi ichukieni pia tabia ya kusengenyana na kusemana, kwani haya nayo ni mfano wa hayo. Na zikingeni nafsi zenu na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri zake, na kuyaepuka ayakatazayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kukubali toba ya wenye kutubia, Mwenye rehema kunjufu kwa walimwengu wote.
Rudi kwenye sura

* 13. Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni nyinyi sawa sawa kutokana na asli moja, ya Adamu na Hawa. Na tukakufanyeni mkawa wengi kwa mataifa makubwa na makabila mengi, ili kutimie kujuana na kuawiniana baina yenu, sio kubaguana. Na hakika mwenye cheo cha juu miongoni mwenu kwa Mwenyezi Mungu duniani na Akhera ni yule anaye mcha Yeye zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa kuvijua, ni Mwenye khabari za dogo na kubwa la kila jambo.
Rudi kwenye sura

* 14. Wakaazi wa majangwani wamesema kwa ndimi zao: Tumeamini. Ewe Muhammad! Waambie: Bado hamjaamini; kwa sababu nyoyo zenu bado hazijasadiki hayo mnayo yatamka. Lakini nyinyi semeni: Tumefuata dhaahiri ya Ujumbe wako. Bado Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kweli, hato kunyimeni hata chembe katika malipo ya vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kuwasamehe waja wake, ni Mwenye rehema kunjufu kwa kila kitu.
Rudi kwenye sura

* 15. Hakika Waumini wa kweli ni wale ambao wanamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha hapana shaka yoyote inayo ingia katika nyoyo zao kwa hayo wanayo yaamini; tena wakapigana Jihadi kwa kutoa mali yao na roho zao katika njia ya ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Hao peke yao ndio walio wakweli katika Imani yao.
Rudi kwenye sura

* 16. Ewe Muhammad! Waambie kwa kuwakanusha ile kauli yao kuwa wameamini: Ndio hivyo ati mnampa khabari Mwenyezi Mungu kuwa nyoyo zenu zimesadiki? Na Mwenyezi Mungu peke yake anajua kila kiliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye sura

* 17. Wanaona kuwa kusilimu kwao ni kukuunga mkono wewe, Muhammad, na hivyo inastahiki wewe uwashukuru. Sema: Msinisimbulie kusilimu kwenu; kwani kheri yake mnaipata nyinyi. Bali ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ihsani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli katika hayo madai yenu.
Rudi kwenye sura

* 18. Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila lilio fichikana katika mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuona vyema yote myatendayo.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani