Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani

Nani Yeye?


Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani , alie fanya tarjuma hii ni Mzalendo wa Zanzibar, aliezaliwa 13 January 1919, akapata mafunzo ya dini kwa baba yake Sheikh Muhsin bin Ali na kwa wanazuoni wengineo wa Afrika ya Mashariki. Pia Sheikh Ali amesoma ilimu ya zaraa katika Chuo Kikuu cha Makerere (Makerere University) huko Uganda.
Alianza maisha yake kwa kufanya kazi ya zaraa na uwalimu. Katika 1947 aliacha kazi ya serikali, ili ashughulikie jihadi ya nchi yake na Umma wake. Alikuwa Muhariri Mkuu wa gazeti la "Mwongozi" kwa muda wa miaka kumi na tano. "Mwongozi" lilikuwa ni gazeti la siasa, la ijtimaa na la dini. Na lilikuwa maarufu kwa kazi yake kubwa ya kudai haki za wananchi na kutapakaza misingi ya Kiislamu huko Zanzibar na sehemu mbali mbali za Afrika ya Mashariki.

Sheikh Ali Muhsin aliongoza chama cha "Hizbu" (Zanzibar Nationalist Party) na aliongoza jihadi ya Uhuru wa Zanzibar kutokana na Muingereza. Hapo alikuwa maarufu kwa jina la "Zaim" yaani Mwongozi. Alifanya kazi ya Waziri wa Ilimu na Waziri wa Mambo ya Ndani, kesha akawa Naibu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje katika serekali ya kidemokrasia ya Zanzibar kabla ya mapinduzi ya Zanzibar yalio mwaga damu za watu hata ulimwengu ukashituka hapo January 1964.
Baada ya machafuzi hayo ya Zanzibar, aliwekwa jela kwa muda wa zaidi ya miaka kumi bila ya kushitakiwa, kwa sibabu ya fikra zake za kisiasa.

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani ametunga tungo kadha wa kadha za dini. Miongoni mwake ni utenzi wa mashairi ya Kiswahili wa beti 1300 juu ya maisha ya Mtume (s.a.w.). Pia ametunga kitabu cha Kingereza cha kulinganisha Ukristo na Uiislamu ambacho kakifasiri mwenyewe Mtungaji kwa Kiswahili.
Hivi sasa Sheikh Ali anaishi Dubai, U.A.E.


Orodha ya Sura
Chagua Sura:
Faharasa

Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com 
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani