Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suurat Yusuf

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Alif, Lam, Raa. Hizi harufi na mfano wake, zinazo fanya maneno yenu, enyi Waarabu, ndizo hizo hizo zinazo fanya Aya za hichi Kitabu, ambacho ni muujiza unao waemea watu kuuiga. Muujiza ulio wazi unao fafanua kwa kila mwenye kutafuta uwongozi ndani yake, na uwongofu. Na kwa hizi harufi za kutamkika zikasikilizana sauti yake wanazinduliwa watu watanabahi. Basi wasikilize, ijapo kuwa waliwafikiana kuwa wasisikilize.
Rudi kwenye sura

* 2. Hakika Sisi tumemteremshia Mtume wetu haya maneno kwa lugha yenu ya Kiarabu yasomwe na yahifadhiwe, ili muyafahamu, na muwafikishie watu wote.
Rudi kwenye sura

* 3. Sisi tunakusimulia, ewe Nabii, visa vizuri kabisa kwa kukufunulia Kitabu hichi. Na kabla ya haya ulikuwa umeghafilika nayo, huyajui, haya, wala mawaidha yaliomo ndani yake, na Aya zake zilizo wazi.
Rudi kwenye sura

* 4. Katika visa hivi, ewe Nabii, kipo hichi kisa cha Yusuf, (1) pale alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeona usingizini nyota hidaa'shara, na jua, na mwezi. Nimeona vyote hivyo vikininyenyekea, vikisujudu mbele yangu. (1) Yusuf, Alayhi Ssalam, alikuwa mwana wa Yaaqub, Muabrani, Mkanaani. Akauzwa Misri katika enzi ya utawala wa wavamizi wa kigeni waitwao Wahiksos. Na kwa ionekanavyo hao Wahiksos ni katika kabila za Kisami walio ingia Misri kutoka Sham wakaiteka Delta ya Misri mnamo mwaka 1730 k.k. ( kabla ya Nabii Isa a.s.) na kabla ya kumalizika enzi ya ukoo wa kumi na tatu wa Mafirauni. Wakaihukumu Misri kwa muda wa karne unusu. Wakafukuzwa mnamo mwaka 1580 k.k. na Ahmas wa Mwanzo aliye anzisha ukoo wa 18. Wakatolewa nje ya mipaka ya Misri.
Rudi kwenye sura

* 5. Baba yake akamwambia: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako hii. Itakuja watia husda katika nyoyo zao, na Shetani atawachochea wazue njama kukupinga. Watakuja kufanyia hila na vitimbi! Hakika Shetani ni adui wazi wa binaadamu!
Rudi kwenye sura

* 6. Kama ulivyo jiona katika ndoto kuwa ni bwana wa kut'iiwa, mwenye cheo na madaraka, basi Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakukhitari, akufunze kufasiri ndoto, kwa kukupa Unabii na Utume, kama hapo zamani, kabla ya baba yako, Yaa'qub, alivyo wafanyia baba zako, Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni mwingi wa hikima, basi hakosei. Ni mwingi wa ujuzi, basi humteuwa katika waja wake anaye mjua kuwa anastahili kuteuliwa.
Rudi kwenye sura

* 7. Hakika katika kisa cha Yusuf na nduguze zipo dalili na mazingatio kwa waulizao, wenye kutaka kujua.
Rudi kwenye sura

* 8. Walipo semezana nduguze Yusuf kwa baba: Bila ya shaka Yusuf na nduguye kwa baba na mama wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi. Na sisi ni kikundi chenye nguvu, chenye kumfaa yeye zaidi kuliko wao! Hakika baba yetu kwa kumfadhilisha Yusuf na nduguye kuliko sisi yumo makosani, na yuko mbali na haki. Yalio sawa yapo wazi yanaonekana.
Rudi kwenye sura

* 9. Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi iliyo mbali na baba yenu, asiyo weza kuifikia. Yatakuwafikieni nyinyi tu mapenzi ya baba yenu, na atakuelekeeni nyinyi tu. Na baada ya kumtenga Yusuf naye kwa kumuuwa au kumhamisha mtakuwa watu wema. Kwani Mwenyezi Mungu atakubali toba yenu, na baba yenu atapokea udhuru wenu.
Rudi kwenye sura

* 10. Mmoja wao katika wasemaji alisema: Msimuuwe Yusuf. Hayo ni makosa makubwa. Lakini mtupeni asipo onekana ndani ya kisima, baadhi ya wapita njia watakuja mwokota, watapo tumbukiza ndoo yao kisimani. Hao watakwenda naye pahala pambali nanyi na baba yenu vile vile. Haya ikiwa nyinyi mna lazima mumpeleke mbali na mtimize kwa kitendo hayo mtakayo.
Rudi kwenye sura

* 11. Baada ya kuwafikiana kumbaidisha Yusuf (kumpeleka mbali) walisema: Ewe baba yetu! Nini kinacho kutia shaka nasi hata unamtenga Yusuf nasi, wala huoni pana usalama anapo kuwa nasi? Sisi tunakuhakikishia kuwa sisi tunampenda, na tunamwonea huruma, na tunamtakia kheri, na tunamwongoza kwenye kheri. Hapati kwetu isipo kuwa mahaba, na nasiha safi kabisa.
Rudi kwenye sura

*12. Mwache ende nasi kesho machungani. Atastarehe kwa kula vyakula vizuri, atacheza na atafurahi. Na sisi kwa yakini tuna hima ya kumhifadhi kumkinga na madhara yoyote.
Rudi kwenye sura

* 13. Mzee akasema: Hakika mimi naona huzuni mkiondoka naye, akawa mbali nami. Na nina khofu nikikuaminini asije akaliwa na mbwa mwitu na nyinyi mmeghafilika naye.
Rudi kwenye sura

* 14. Wakasema: Tunakuapia, akiliwa na mbwa, na hali sisi ni kundi lenye nguvu, basi itakuwa ni fedheha na khasara kwetu! Likitokea hilo unalo liogopa basi sisi tutakuwa tumekhasiri kila linalo pasa kulishughulikia, na kuwa lisitokee. Basi tuwa kwa hayo! Hatutadharau kumlinda, ikiwa hivyo itakuwa tunajipelekea wenyewe kupotea na kupuuza.
Rudi kwenye sura

* 15. Walipo kwenda naye mbali na baba yake, na wakakubaliana rai yao ya kumtumbukiza ndani ya kisima, walifanya hayo waliyo yaazimia. Sisi tukamtia moyoni mwake Yusuf atulie, na awe na imani ya Mwenyezi Mungu, kuwa bila ya shaka atakuja waeleza haya mambo yao waliyo yapanga na wakayatenda, na wala wao wenyewe hawajui hapo utapo waambia kwamba wewe ndiye Yusuf waliye mfanyia vitimbi, na wakadhani wamekwisha mmaliza na wameepukana naye!
Rudi kwenye sura

* 16. Walirejea kwa baba yao usiku, wakijitia huzuni, na kupiga makelele kwa kilio!
Rudi kwenye sura

* 17. Wakasema: Ewe baba yetu! Sisi tulikwenda kushindana kupiga mishale na kwenda mbio, na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu avilinde. Mbwa mwitu akamla, na sisi tuko mbali tumeshughulika na mashindano! Na wewe hutusadiki tunayo yasema, ijapokuwa tunasema haki na kweli!
Rudi kwenye sura

* 18. Wakaileta kanzu yake nayo ina damu, ati kuwa ni ushahidi wa yale madai yao ya kuwa ile ni damu ya Yusuf, apate kusadiki baba yao! Walakini yeye alisema: Hakika huyo mbwa mwitu hakumla kama mnavyo singizia, bali nafsi zenu zimekupelekeeni kufanya jambo kubwa, na mkalitimiza! Langu mimi ni kusubiri subira njema isiyo legalega kwa mliyo nikutisha. Na Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye takiwa msaada kwa huo upotovu mlio uzua na mnao udai.
Rudi kwenye sura

* 19. Wakaja watu upande ule wa kisima katika msafara wao wa kwendea Misri. Wakamtuma mtu kati yao wa kuchota maji kisimani awaletee. Akatumbukiza ndoo yake, akiivuta na Yusuf kang'ang'anilia! Yule mchota maji akapiga kelele za furaha: Kheri! Kheri gani hii na furaha! Huyu ni kijana! Wakamficha katika vitu vyao, wakamfanya ni bidhaa ya biashara! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wayatendayo kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye sura

* 20. Wakamuuza Misri kwa bei ya chini kabisa, si kiasi chake! Thamani yake ilikuwa ni pesa chache tu! Wala hawakuwa wakimtakia Yusuf thamani kubwa, kwa kukhofia wasije watu wake wakamkuta wakamtambua, na wakawapokonya Yusuf.
Rudi kwenye sura

* 21. Yule aliye mnunua kule Misri alimwambia mkewe: Mfanyie wema huyu, na umhishimu, ili makao yake hapa nasi yawe mazuri. Huenda akatufaa, au tukamfanya kuwa ni mwenetu. Kama yalivyo kuwa makaazi yake ni mazuri na ya hishima, basi kadhaalika tulimjaalia Yusuf katika nchi ya Misri cheo kingine kikubwa, ili atekeleze uadilifu na mipango mizuri, na ili tumfunze kufasiri mambo na ndoto, ajue yatakayo kuwa kabla hayajwa, ili awe tayari kuyakabili! Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kutimiza kila jambo alitakalo. Kabisa haemewi na kitu. Lakini watu wengi hawajui siri ya hikima yake, na undani wa mipango yake.
Rudi kwenye sura

* 22. Na Yusuf alipo timia ukomo wa nguvu zake tukampa hukumu yenye kusibu, na ilimu yenye kufaa. Na kama malipo haya tuliyo mpa yeye kwa wema wake, ndio tunavyo wapa wote walio wema kwa vitendo vyao vyema.
Rudi kwenye sura

* 23. Na yule bibi aliye kuwa Yusuf anakaa nyumbani kwake, naye anamjua madaraka yake, alitaka kumghuri aache mwendo wake ulio safi. Akawa anajipitisha pitisha mbele yake kuonyesha uzuri wake, na kujitamanisha kwake. Hata mwishoe akamfungia milango, na akamwambia: Njoo kwangu, nimejitoa kwako! Yusuf akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu, aniepusha na hiyo shari! Na vipi nifanye uchafu huo nawe, na mumeo mheshimiwa ni bwana wangu aliye niweka bora ya makamo? Hakika hawafuzu wanao wadhulumu watu kwa udanganyifu na khiana, wakajitia wenyewe katika maasi ya uzinzi!
Rudi kwenye sura

* 24. Na yule bibi aliazimia aingiane naye, na nafsi ya Yusuf ilimvutia kwake, lau kuwa hakuiona nuru ya Mwenyezi Mungu ya haki imezagaa mbele ya macho yake. Basi hakuufuata mvutio wa nafsi, na akayashinda matamanio, na akajizuilia maasi na khiana. Akathibiti juu ya usafi na kutakasika kwake. Ndio hivi tulivyo mthibitisha Yusuf kwenye usafi na kutakasika, ili tumuepushe na uovu wa khiana na maasi ya uzinzi. Hakika yeye ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu walio itakasa dini yao kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 25. Yusuf akakimbilia mlangoni kutaka kutoka, na yule bibi naye akapiga mbio amtangulie ili amzuie kutoka. Akaivuta kanzu yake kwa nyuma ili kumzuia, akaichana. Hapo wakapambana na mume wa yule bibi mlangoni! Yule bibi akasema kumchongea Yusuf: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanya mkeo mambo mabaya ila atiwe gerezani, au akutishwe adhabu chungu!
Rudi kwenye sura

* 26. Yusuf akasema kujitetea: Ni yeye ndiye aliyenitaka, na akajaribu kunikhadaa! Ikawa ni kusutana. Alikata hukumu mmojapo katika jamaa zake mwenyewe yule mwanamke kwa kusema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi huyu bibi kasema kweli katika madai yake, na huyu kijana ni mwongo kwa aliyo yasema.
Rudi kwenye sura

* 27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi huyu mwanamke kasema uwongo, na kijana ni mkweli kwa aliyo yasema.
Rudi kwenye sura

* 28. Mume alipoona kuwa kanzu ya Yusuf imechanwa mgongoni alimwambia mkewe: Huku kumtuhumu kwako kijana kwa yaliyo tokea na hali yeye hana makosa, ni katika vitimbi vyenu, enyi wanawake. Hakika vitimbi vyenu ni vikuu mno!
Rudi kwenye sura

* 29. Ewe Yusuf wachilia mbali mambo haya, na wewe yafiche wala usiyaseme. Na wewe, mwanamke, omba maghfira kwa dhambi yako. Hapana shaka kuwa wewe ni katika wenye dhambi, wenye kuyakusudia makosa, na kutenda maasi, na kuwasingizia wengine uasi wasio ufanya!
Rudi kwenye sura

* 30. Khabari zikawafikia baadhi ya wanawake wa mjini, wakazungumza wakisema: Mke wa Mheshimiwa anamzaini mtumishi wake na anamkhadaa amkubalie anayo yataka kwake! Ama kweli amesalitika kwa mahaba hata hajitambui! Hakika sisi tunaamini kuwa kwa mwendo wake huu ameingia kwenye upotovu na makosa yaliyo wazi.
Rudi kwenye sura

* 31. Yule bibi alipo yasikia masengenyo yao wale wanawake na kuwa wanamsema kwa vibaya, aliwaalika nyumbani kwake na akawapangia matakia na mito ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu, baada ya kwisha hudhuria na wakakaa wakiegemea. Akawaletea chakula na visu vya kulia. Akamwambia Yusuf: Hebu watokee! Alipotokeza wakamwona walistaajabu. Uzuri wake ulio pita mpaka uliwatwaa wasijitambue, wakawa wanajikata mikono yao jinsi ya kushtuka kwao, na huku wanadhani wanakata chakula! Wakasema kwa mastaajabu na kushituka: Hasha Lillahi! Mungu apishe mbali! Huyu tunaye mwona si binaadamu! Hapana binaadamu mwenye uzuri namna hii, na mwenye jamali kama hivi, na usafi kama huu, na kunyooka kama huku! Huyu ni Malaika tu, mwenye uzuri huu, na sifa hizi zilio timia!
Rudi kwenye sura

* 32. Tena mke wa Mheshimiwa alisema kufuatiliza maneno yao: Huyu kijana ambaye uzuri wake umekuzugeni na ukakuemeeni hata yakatokea yaliyo tokea ndiye ambaye nyinyi mliye nilaumu kwa ajili yake! Na mimi kweli nilimtaka, na nikafanya juhudi kumghuri anikubalie, naye akajizuia na akakataa. Kama kwamba vile anavyo kataa ndio anazidi kumtia hamu yule mwanamke! Akasema mwanamke: Na mimi naapa! Kama hafanyi ninayo muamrisha atapata adhabu ya kifungo, na atakuwa katika madhalili wenye kudharauliwa!
Rudi kwenye sura

* 33. Yusuf akasema naye alisikia vile vitishio, na akasikia kwa wale wanawake nasiha ya kuwa amkubalie, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nakhiari kifungo kuliko hayo anayo nitakia huyu mwanamke. Kwani hayo ni kukuasi Wewe. Na kama Wewe hunikingi na shari ya vitimbi vyao na hila zao nitakuja wakubalia, na nitakuwa miongoni mwa wajinga walio potea.
Rudi kwenye sura

* 34. Mwenyezi Mungu akamuitikia, na akamuepusha na shari ya vitimbi vyao. Hakika Yeye peke yake ndiye Mwenye kusikia maombi ya wenye kukimbilia kwake, na Mwenye kujua yanao wafaa.
Rudi kwenye sura

* 35. Kisha ikadhihiri rai ya Mheshimiwa na watu wake, baada ya kwisha ona dalili zilizo wazi kuwa Yusuf hana makosa. Wakakubaliana rai hii, na wakaapa kuitimiza. Nayo ni kumtia yeye gerezani kwa muda mfupi au mrefu, ili kumkinga mkewe na maneno mabaya, na kumuepusha na masengenyo ya watu!
Rudi kwenye sura

* 36. Wakaingia pamoja na Yusuf vijana wawili katika watumishi wa Mfalme. Mmoja wao akasema: Mimi nimeota usingizini kuwa ninakamua zabibu kutengeneza mvinyo. Mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba kichwani mwangu mikate, na ndege wanaila! Hebu tuambie, ewe Yusuf, tafsiri ya haya tuliyo ota, na mambo yetu yataishia vipi. Sisi tunaamini kuwa wewe ni katika watu wanao sifika kwa wema na kujua tafsiri za ndoto.
Rudi kwenye sura

* 37. Yusuf akawaambia kutilia mkazo yale waliyo yajua kwake Yusuf: Hakitowahi kukufikieni chakula kuwa ni riziki mliyo kadiriwa ila nami nitakwambieni kitavyo kujieni kabla ya kukufikieni. Na nitakutajieni mapishi yake na vipi kilivyo. Namna hivyo ndivyo tafsiri ya ndoto na khabari zilizo fichikana katika alivyo nifunza Mola wangu Mlezi na akanifunulia, kwani nilimtakasia Yeye tu ibada yangu. Na nikakataa kumshirikisha na kitu chochote. Na nikajitenga mbali na dini ya watu wasio msadiki Mwenyezi Mungu, na wala hawamuamini Yeye kwa njia iliyo sawa, nao wanaikanya Akhera na hisabu zake.
Rudi kwenye sura

* 38. Mimi nimeacha mila ya hawa makafiri, na nikafuata Dini ya baba zangu Ibrahim, na Is-haaq, na Yaa'qub. Nikamuabudu Mwenyezi Mungu pekee. Haitufalii sisi kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika yeyote yule, akiwa Malaika, au jini, au mwanaadamu, licha ya masanamu ambayo hayaleti manufaa wala madhara, wala hayasikii, wala hayaoni! Hiyo ndiyo Tawhidi aliyo tutunukia Mwenyezi Mungu sisi na watu wote, kwa vile alivyo tuamrisha tuwafikilishie ujumbe. Lakini wengi wa watu hawaipokei fadhila hii kwa shukrani, bali wanaikataa!
Rudi kwenye sura

* 39. Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Je mabwana wengi mbali mbali ni bora mtu kuwanyenyekea kuliko Mwenyezi Mungu Mmoja asiye shindika?
Rudi kwenye sura

* 40. Hamuabudu badala ya Mwenyezi Mungu ila majina tu mliyo yazua nyinyi na baba zenu kwa mawazo bila ya kuwepo kweli. Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hao hoja wala ushahidi wowote! Hapana wa kuhukumu nini kinacho faa kuabudiwa na kipi hakifai ila Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimnyenyekee yeyote mwenginewe, na mumuabudu Yeye peke yake. Hiyo ndiyo Dini iliyo nzima iliyo nyooka, ambayo dalili zote na ushahidi unaelekea kwake. Lakini aghlabu ya watu hawataki uwongozi wa dalili hizi, wala hawajijui kuwa wamo katika ujinga na upotovu.
Rudi kwenye sura

* 41. Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Hii basi ndiyo tafsiri ya ndoto zenu: Ama mmoja wenu aliye kamua zabibu katika ndoto yake, atatoka jela, na atakuwa akimnywesha mvinyo Mfalme. Na ama huyu wa pili atatundikwa msalabani, na ataachwa msalabani ndege wakimla kichwa chake. Yamekwisha timia hayo mambo kama nilivyo eleza kwa mujibu mlivyo nitaka nieleze tafsiri ya hizo ndoto!
Rudi kwenye sura

* 42. Akamwambia yule aliye kuwa atavuka: Nitaje kwa Mfalme kwa sifa zangu, na kisa changu. Asaa huenda akanifanyia insafu akanivua na haya mateso! Shetani alimshughulisha akamsahaulisha kutaja kisa cha Yusuf kwa Mfalme. Basi Yusuf akabaki gerezani kwa miaka isiyo pungua mitatu.
Rudi kwenye sura

* 43. Mfalme akasema: Nimeota usingizini kuna ng'ombe saba wanene wanaliwa na wengine saba walio konda madhaifu. Na nimeota mashuke saba mabichi, na mengine saba makavu. Enyi wakuu wanazuoni na wenye maarifa! Nitoleeni fatwa ya hizi ndoto zangu, ikiwa ni kweli nyinyi mnajua tafsiri za ndoto na mnaweza kuzitolea fatwa.
Rudi kwenye sura

* 44. Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo korogeka ovyo, na wasiwasi wa kuzuka tu katika nafsi ya mtu! Na sisi si wenye kujua tafsiri ya ndoto za ovyo ovyo.
Rudi kwenye sura

* 45. Akasema yule mtu aliye okoka katika wawili alio kuwa nao Yusuf gerezani, na akakumbuka wasia wa Yusuf, baada ya kupita muda mrefu: Mimi nitakwambieni tafsiri ya ndoto aliyo itaja mfalme. Nipelekeni kwa huyo mwenye ilimu ya kuifasiri.
Rudi kwenye sura

* 46. Yule mtumishi wa kumletea mfalme ulevi akenda kwa Yusuf, akamwita: Yusuf! Ewe uipendaye kweli! Tueleze nini maana ya ndoto ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na ndoto ya mashuke saba mabichi na mengine makavu? Nataraji kurejea kwa watu nami nina fatwa yako, ili nao wapate kujua maana yake, na waujue ujuzi wako na fadhila yako.
Rudi kwenye sura

* 47. Yusuf akasema: Tafsiri ya ndoto hizo ni kuwa mtalima katika ardhi ngano, na shairi kwa muda wa miaka saba mfululizo kwa ukulima wa juhudi. Mtacho vuna kihifadhini, mkiache katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtacho kila katika miaka hiyo, kwa uangalizi mzuri. Aya hii inawafikiana na ilimu za kisasa kuwa kuweka punje katika mashuke yake inakuwa ni hifadhi zisiharibike kwa hali ya hewa na mengineyo, na juu ya hivyo faida yake ya chakula inabaki kwa ukamilifu zaidi.
Rudi kwenye sura

* 48. Kisha baada ya miaka hii ya neema itakuja saba ya ukame. Mtakula kile mlicho weka akiba, isipo kuwa kidogo mtacho kificha na kukihifadhi, ili kiwe mbegu ya kupandia baadae
Rudi kwenye sura

* 49. Kisha baada ya miaka hiyo ya ukame utakuja mwaka watu watasaidiwa kwa mvua, na watakamua zabibu na zaituni, na kila cha kukamuliwa.
Rudi kwenye sura

* 50. Mfalme akamwona Yusuf atakuwa na faida naye kwa ule uwezo wake kuifasiri ndoto yake, na akaazimia amwite. Akawaamrisha wasaidizi wake wamlete. Alipo mfikia mjumbe akamwabia kuwa mfalme anamtaka, khabari hiyo haikumpapatisha, juu ya kuwa ina bishara ya kufunguliwa kwake. Wala kule kutamani kutoka kwa mfungwa kwenye dhiki za jela na taabu zake hakukuitikisa subira yake. Akakhiari angoje mpaka idhihirike kuwa hana makosa kuliko kufanya haraka kutoka na huku yale aliyo tuhumiwa bado yamemganda. Akamwambia mjumbe: Rejea kwa bwana wako umtake ayaangalie tena yale mashtaka niliyo shitakiwa, awaulize wale wanawake walio kusanywa na mke wa Mheshimiwa kwa kunifanyia hila mimi, wakababaika na wakajikata mikono yao: Je! Walipo toka kwenye yale majaribio walikuwa wanaamini kuwa mimi sina makosa na safi, au waliniona ni mchafu na mzinifu? Mimi nataka haya ipate kuonekana hakika katika macho ya watu. Ama Mola wangu Mlezi anavijua vyema vitimbi vyao!
Rudi kwenye sura

* 51. Mfalme akawakusanya wale wanawake, na akawauliza: Ilikuwa vipi hali yenu pale mlipo jaribu kumkhadaa Yusuf aghafilike na wema wake na usafi wa nafsi yake? Je, mlimwona amemili kwenu? Wakamjibu: Mwenyezi Mungu ametakasika! Hakumsahau mja wake hata uchafuke usafi wake. Sisi hatukuona kwake lolote la kumtia dosari. Hapo basi wema ukapata nguvu katika moyo wa Zuleikha (mke wa Mheshimiwa) akaingia kusema: Sasa kweli imedhihiri! Ni mimi ndiye niliye mkhadaa, na nikajaribu kumzaini kinyume na nafsi yake kwa kumghuri. Lakini yeye alishikilia usafi wake! Na sasa nahakikisha kuwa yeye ni katika watu wa kweli. Na ni haki tupu alipo nirudishia tuhuma mimi na kunitia makosani!
Rudi kwenye sura

* 52. Haya mimi naungama kwa kweli ninayo itoa, apate kuwa na yakini Yusuf kuwa mimi sikuchukua fursa ya kuto kuwepo alipo kuwa gerezani nikaendelea na khiyana, na nikamdhulumu kwa kumtuhumu. Na kwa kuwa hakika Mwenyezi Mungu haijaalii kufanikiwa mipango ya makhaini.
Rudi kwenye sura

* 53. Wala sidai kuwa nafsi yangu haitelezi; kwani ni tabia ya nafsi kumili kwenye matamanio, na kupendelea maovu na shari. Isipo kuwa nafsi aliyo ilinda Mwenyezi Mungu na akaiweka mbali na maovu. Na hakika mimi ninatumai rehema ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake, kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe dhambi za wenye kutubu, na yu karibu wa kuwarehemu waja wake walio kosa.
Rudi kwenye sura

* 54. Usafi wa Yusuf ulipo dhihiri kwa mfalme, aliazimu amwite. Akawatuma watu wake wamlete awe wake yeye mwenyewe wa kumsafia niya. Basi alipo hudhuria na yakapita baina yao mazungumzo, mfalme akaathirika na utukufu wa Yusuf kwa usafi wa nafsi yake, na ubora wa rai zake! Akamwambia: Sasa wewe kwangu utakuwa na cheo cha hishima kilicho thibiti. Na wewe ni muaminifu kwangu ninaye kuamini.
Rudi kwenye sura

* 55. Mfalme akajua kwake Yusuf kuwa yeye ni muangalizi mwema na mweza wa kazi yake. Na Yusuf akahisi hayo. Hapo akataka amfanye waziri akamwambia: Nitawalishe juu ya khazina zote za mamlaka yako, na ghala za nchi yako. Kwani mimi kama ulivyo yakinika mwenyewe naweza kuendesha mambo ya serikali, nami ni mlinzi, na najua kupanga na kuendesha mambo.
Rudi kwenye sura

* 56. Mfalme alilikubali ombi lake, akamfanya waziri wake. Hivyo basi Mwenyezi Mungu alimneemesha Yusuf kwa neema nzuri, akampa madaraka na uwezo katika nchi ya Misri, akienda humo atakapo. Na hii ndiyo shani yake Mwenyezi Mungu kwa waja wake, humpa neema yake amtakaye katika wao, wala hawanyimi thawabu zao, bali huwapa ujira wao wa wema wautendao kwa kuwalipa mema hapa hapa duniani.
Rudi kwenye sura

* 57. Na malipo yao ya Akhera ni bora zaidi na yanalingana zaidi na hao wanao msadiki Yeye na Mitume wake, na ikawa wanaingojea Siku ya Hisabu na wanaikhofu.
Rudi kwenye sura

* 58. Ukame ukazidi kushtadi katika nchi jirani na Misri. Ikawapata watu wa Yaa'qub shida vile vile kama ilivyo wapata wengineo. Watu walikwenda Misri kutoka kila pande baada ya kujua matengenezo ya Yusuf ya kuweka akiba chakula, na kujitayarisha kwake kwa miaka ya ukame. Yaa'qub aliwatuma wanawe wende kutafuta chakula, lakini akabaki naye nduguye Yusuf kwa mama kwa kumkhofia. Wale watoto wake walipo fika Misri wakenda moja kwa moja kwa Yusuf, naye akawatambua, lakini wao hawakumjua.
Rudi kwenye sura

* 59. Yusuf akaamrisha wakaribishwe ugeni, na wapewe mahitaji wanayo yataka. Wakapewa hayo. Akaingia kuzungumza nao na kuwauliza hali zao kama mtu asiye wajua! Naye anawajua vyema. Nao wakamwambia kuwa wamemwacha ndugu yao mmoja kwa baba yao, kwani hapendi kuachana naye. Naye huyo ni Bin-yamini nduguye Yusuf kwa baba na mama. Basi yeye akasema: Mwacheni ndugu yenu aje nanyi, wala msiogope chochote. Nyinyi mmekwisha ona vipi ninavyo kutimizieni vipimo vyenu, na ninavyo kukirimuni.
Rudi kwenye sura

* 60. Mkitomleta ndugu yenu huyu, basi hampati chakula kwangu, wala msijaribu kunijia tena.
Rudi kwenye sura

* 61. Nduguze wakasema: Tutajaribu kusema na baba yake ageuze rai yake, iondoke khofu yake juu ya mwanawe. Na sisi tunakuhakikishia kuwa hatutokasiri wala kulegalega katika hayo.
Rudi kwenye sura

* 62. Walipo taka kuondoka aliwaambia wafwasi wake: Watilieni thamani ya bidhaa yao waliyo kuja nayo humo humo pamoja na mizigo yao, ili waione watakapo rudi kwa watu wao, wapate kurejea tena kwa kutumai kupewa chakula kwa kuamini kuwa tunatimiza ahadi, na wawe na imani ya usalama wa ndugu yao, na baba yao azidi kutua nafsi yake.
Rudi kwenye sura

* 63. Walipo rejea kwa baba yao walimsimulia kisa chao na Mheshimiwa wa Misri, na upole wake kwao, na kwamba amewaonya kuwa atawanyima kuwapimia chakula baadae ikiwa hatokuwa nao Bin-yamini; na kwamba amewaahidi kuwatimizia kipimo na atawatukuza pindi wakirudi na ndugu yao. Wakamwambia baba yao: Mwache ende nasi ndugu yetu, kwani ukimpeleka yeye tutapimiwa chakula cha kutosha tunacho kihitajia. Nasi tunakuahidi ahadi ya nguvu ya kwamba tutafanya juhudi kumlinda.
Rudi kwenye sura

* 64. Yaa'qub yalimtibuka moyoni mwake yale ya zamani, akayaunganisha na haya mapya. Akawaambia wanawe: Nikikukubalieni itakuwa hali yangu ni ya ajabu; kwani nikikuaminini kwa huyu ndugu yenu haitakuwa ila mfano wa pale nilipo kuaminini kwa Yusuf. Mkamchukua kisha mkarudi mkisema: Kaliwa na mbwa mwitu! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye anaye nitosheleza katika kumlinda mwanangu. Wala mimi simtegemei mtu ila Yeye, kwani Yeye ndiye Mlinzi aliye na nguvu kuliko wote, na rehema yake ni kunjufu mno, hatonipa tena machungu ya ndugu yake baada ya yale ya Yusuf.
Rudi kwenye sura

* 65. Na wale nduguze Yusuf hawakujua kuwa Yusuf aliwatilia bidhaa zao katika mizigo yao. Walipo ifungua wakakuta mali yao, na wakaona hisani aliyo wafanyia Yusuf, wakaitumia hiyo kuzidi kumpoza moyo Yaa'qub, na kumkinaisha awakubalie kwa aliyo yataka Mheshimiwa. Wakazidi kumshikilia akubali, wakamkumbusha makhusiano yao yalio wafunga kwa baba mmoja. Wakasema: Ewe baba yetu! Unataka wema gani zaidi kuliko haya, na hayo yatayo kuwa? Haya mali yetu tumerudishiwa bila ya kuchukuliwa chochote. Basi natusafiri na ndugu yetu, na tuwaletee watu wetu mahitaji, nasi tutamchunga ndugu yetu, na tutaongeza mahitaji shehena ya ngamia kuwa ni haki ya ndugu yetu! Kwani yule Mheshimiwa kapanga kuwa kila mtu humpa shehena ya ngamia.
Rudi kwenye sura

* 66. Waliweza wana wa Yaa'qub kumkinaisha baba yao, na maneno yao yakampata palipo. Akaacha kushikilia kumzuia mwanawe asende Misri na nduguze. Lakini moyo wake haukuwacha kuwa na haja ya kuzidi kutuzwa. Kwa hivyo aliwaambia: Sitomwacha ende nanyi ila baada ya kunipa dhamana ya nguvu. Niahidini kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtanirudishia mtapo rudi. Na wala msiache kumrudisha ila mkiangamia nyinyi au ikawa adui amekuzungukeni akakushindeni. Wakamkubalia na wakampa ahadi aliyo itaka. Na hapo tena akamshuhudisha Mwenyezi Mungu ahadi yao na viapo vyao kwa kusema: Mwenyezi Mungu anayashuhudia na kuyaona yote haya yanayo pita baina yetu.
Rudi kwenye sura

* 67. Yaa'qub alitua kwa ahadi ya watoto wake. Kisha huruma ilimpelekea kuwausia kuwa watapo ingia Misri waingie kupita milango mbali mbali, ili watu wasiwapige kijicho, huenda wakadhurika. Akasema: Wala mimi sina uwezo wa kukulindeni na madhara. Kwani mwenye kuzuia madhara ni Mwenyezi Mungu tu, na hukumu ni yake Yeye pekee. Mimi nimemtegemea Yeye, na mambo yangu na yenu yote nimemwachia Yeye. Na juu yake Yeye peke yake wategemee wote wanao tegemeza mambo yao, kwa kumuamini Yeye.
Rudi kwenye sura

* 68. Wale vijana wakapokea wasia wa baba yao, wakapitia milango mbali mbali. Wala hayo si kama ndiyo ya kuwazuilia madhara walio kwisha andikiwa na Mwenyezi Mungu! Na Yaa'qub akijua hayo, kwani yeye alikuwa na ilimu tuliyo mfundisha. Lakini wasia wake ulikuwa ni kwa haja aliyo kuwa nayo nafsini mwake tu, nayo ni huruma ya baba kwa wanawe ambayo ameidhihirisha katika huu wasia. Na hakika watu wengi hawana ujuzi kama alio kuwa nao Yaa'qub wakamwachia mambo yao Mwenyezi Mungu awalinde.
Rudi kwenye sura

*69. Walipo ingia kwa Yusuf aliwapokea kwa hishima, na khasa yule nduguye kwa baba na mama ndio akamchukua na akampa siri kwa kumwambia: Usitie shaka mimi ni nduguyo Yusuf. Basi usihuzunike kwa waliyo kufanyia wewe na waliyo nifanyia mimi.
Rudi kwenye sura

*70. Basi baada ya kuwakirimu kwa kuja kwao, na kuwapimia chakula, na kuwazidishia shehena ya nduguye, aliwafungia mizigo yao kwa ajili ya safari. Tena akawaamrisha wasaidizi wake watumbukize chombo cha kunywea katika mzigo wa Bin-yamini. Kisha mmoja wa wasaidizi wa Yusuf alinadi: Enyi wasafiri! Ngojeni! Nyinyi ni wezi!
Rudi kwenye sura

*71. Wakashituka nduguze Yusuf kwa kutangaziwa yale, wakawaelekea wale wenye kunadi wakawauliza: Mmepoteza nini, na mnatafuta nini?
Rudi kwenye sura

*72. Wale wasaidizi wakajibu: Tunatafuta kikopo, nacho ni chombo anacho nywea mwenyewe mfalme. Na malipo yake kwa mwenye kukileta ni shehena nzima ya chakula anayo ibeba ngamia. Yule mkubwa wao alitilia mkazo hayo kwa kusema: Na mimi ninadhamini kutimiza ahadi hii.
Rudi kwenye sura

*73. Nduguze Yusuf wakasema: Hakika kututuhumu sisi kwa wizi ni jambo la ajabu mno! Na tunahakikisha kwa kiapo ya kwamba nyinyi wenyewe mmeona katika mwendo wetu na tunavyo ishika dini yetu katika mara mbili tulipo kuja hapa kuwa mmejua yakini kuwa sisi hatutaki kuleta uharibifu katika nchi yenu. Wala si katika tabia yetu kuwa ni wezi.
Rudi kwenye sura

*74. Na Yusuf alikwisha waamrisha wafwasi wake wawaache nduguze waamue nini malipo anayo stahiki kupata yule atakaye onekana nacho kile kikopo, ili apate kumchukua nduguye kwa hukumu yao wenyewe, na iwe hukumu yao ndiyo ya kukata shauri, isiwepo njia ya kumwombea. Basi watu wa Yusuf wakawaambia wale nduguze: Nini malipo ya wevi kwenu wanapo gundulikana ni katika nyinyi?
Rudi kwenye sura

* 75. Na kwa kuwa wana wa Yaa'qub walikuwa na yakini kuwa wao hawakukiba kile kikopo walisema bila ya kusitasita: Malipo ya mwenye kuchukua hicho kikopo ni kushikwa huyo na afanywe mtumwa. Ndio hivi sisi tunavyo walipa wenye kudhulumu wakachukua mali ya watu.
Rudi kwenye sura

* 76. Shauri ikaishia ipekuliwe mizigo, na ikawa lazima kufanya mambo baraabara ili isionekane kuwa kuna mpango ulio pangwa. Yusuf mwenyewe ndiye aliye fanya uchunguzi, baada ya kwisha tengeza mambo. Akaanza kupekua mizigo ya wale ndugu kumi, kisha ndio akaingia kuupekua mzigo wa nduguye. Humo akakitoa kile kikopo, na kwa hivyo hila yake ikafuzu. Akawa na haki kwa hukumu ya nduguze kumshika Bin-yamini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyo mpangia mambo Yusuf. Hakuwa anaweza yeye kumshika nduguye kwa mujibu wa sharia ya mfalme wa Misri tu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Naye alitaka. Basi tulimpangia mambo Yusuf, na tukamwezesha kuzirekibisha sababu na mipango baraabara na hila nzuri. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu, ambaye humtukuza katika vyeo vya ujuzi amtakaye. Na juu ya kila mwenye ilimu yupo mwenye kumzidia katika ujuzi!
Rudi kwenye sura

* 77. Kule kugunduliwa kikopo katika mzigo wa ndugu yake kwa ghafla kuliwashangaza nduguze na kukawababaisha. Kwa hivyo wakataka kujivua kuwa wao wote hawana makosa ila huyo na Yusuf, na kusema kuwa tabia ya wizi wameirithi kwa mama yao. Wakasema: Si ajabu kuwa huyo kaiba, kwani nduguye khalisa aliwahi kwiba vile vile! Na Yusuf akatambua kijembe chao wanacho mpigia, na yakamuudhi hayo. Lakini aliyaficha, na akawawekea jawabu moyoni mwake lau kuwa amesema wazi jawabu yenyewe inge kuwa hivi: Nyinyi mko katika hali ovu zaidi, na nyinyi ni duni zaidi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, na kutambua ukweli wa maneno yenu ya kumsingizia nduguye fedheha ya wizi.
Rudi kwenye sura

* 78. Wakawa hawana budi kujaribu kumvua ndugu yao au kumtolea fidia kwa kutaka kutimiza ile ahadi yao waliyo mpa Yaa'qub. Wakaingia kutaka kumlainisha moyo Yusuf kwa kumtajia uzee wa baba yao, wakamwambia: Ewe Mheshimiwa! Huyu ndugu yetu ana baba mtu mzima sana. Basi mfanyie huruma umchukue mmoja wetu mwenginewe awe badala ya mwanawe huyu ambaye ndiye anaye mpenda moyoni mwake. Matarajio yetu ni kuwa utatukubalia mambo yetu. Kwenu tumekwisha ona tabia yako ya ukarimu, na tumehakikisha mwendo wako wa kupenda kufanya hisani na kutenda mema.
Rudi kwenye sura

* 79. Wala haikufalia kwa Yusuf kuvunja mpango alio mkubalia Mwenyezi Mungu, na kumwachia nduguye atoke mkononi mwake. Kwa hivyo maombi yao hayakumlainisha kitu. Akawajibu jawabu mkato, kwa kuwaambia: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu isije nafsi yangu ikadhulumu kwa kumzuia yeyote yule isipo kuwa yule yule tuliye mkuta nayo mali yetu. Tukimchukua mwenginewe kwa kumuadhibu tutakuwa katika hao walio vuka mipaka kwa kumshika asiye na makosa kwa madhambi ya mwovu.
Rudi kwenye sura

* 80. Ilipo katika tamaa yao, wakavunjika moyo kukubaliwa maombi yao, wakenda pembeni peke yao wakishauriana juu ya msimamo wao na baba yao. Ilipo ishia shauri kwa mkubwa wao mwenye kupanga mambo yao, aliwaambia: Haikufalieni kuisahau ahadi ya kiapo mliyo mpa baba yenu ya kuwa mtamhifadhi ndugu yenu mpaka mrudi naye, wala mlivyo fungana naye kabla yake kuwa mtamlinda Yusuf, na hayo mkayavunja! Kwa hivyo mimi nitabaki Misri wala sitotoka ila afahamu baba yetu ukweli wa hali hii, na akaniachilia nirejee kwake, au Mwenyezi Mungu anihukumie kurejea kwa hishima, na akanisahilishia njia kwa sababu yoyote ile. Na Yeye ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
Rudi kwenye sura

* 81. Rejeeni nyinyi kwa baba yenu, na msimulieni kisa chote hichi. Na mwambieni: Mkono wa mwanao ulikunjuka akakiiba kikopo cha mfalme, na kimekutikana katika bahasha yake. Kwa huo wizi wake ndio ameshikwa. Nasi hatukwambii ila tuliyo yaona, na wala sisi hatukuwa tunajua yaliyo fichikana katika hukumu ya Mwenyezi Mungu pale tulipo kutaka nawe ukatupa tumhifadhi na turejee naye kwako kama tulivyo ahidiana na tukafungana. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
Rudi kwenye sura

* 82. Na ikiwa wewe una shaka na haya tunayo kwambia mtume mtu akuletee ushahidi wa watu wa Misri. Na pia wewe mwenyewe waulize wasafiri wenzetu tulio rudi nao, ipate kudhihiri kuwa sisi hatuna lawama. Nasi tunakuhakikishia kuwa sisi ni wakweli katika haya tuyasemayo.
Rudi kwenye sura

* 83. Wakarejea wana walio baki kwa Yaa'qub. Wakamueleza kama alivyo wausia kaka yao mkubwa. Khabari ile ikamtibua huzuni zake, zikazidi kwa kumpoteza mwanawe wa pili. Wala hakutua nafsi yake kwa kuwa wao hawana makosa ya kusabibisha kupotea kwake, naye angali na machungu kwa waliyo mfanyia Yusuf. Akapiga ukelele kwa kuwatuhumu akiwaambia: Niya yenu haikusalimika katika kumhifadhi mwanangu, lakini nafsi zenu zimekuchocheeni mumpoteze kama mlivyo mpoteza nduguye. Lau kuwa nyinyi hamkutoa fatwa ya kuwa mwizi ashikwe afanywe mtumwa kuwa ndiyo adabu ya mwizi huyo Mheshimiwa asingeli mshika mwanangu, wala asingeli baki kaka yenu huko Misri. Lakini mimi sina hila ila kustahamili katika msiba wangu kwa maliwaza mema, huku nikitaraji kwa Mwenyezi Mungu anirudishie wanangu wote. Kwani Yeye ndiye Mwenye ujuzi ulio zunguka hali yangu na hali zao. Na Yeye ndiye Mwenye hikima yenye kushinda, na kwa hiyo ndio hunitendea na hunipangia.
Rudi kwenye sura

* 84. Akadhikika kwa waliyo yasema, akajitenga nao, kashughulika na msiba wake na huzuni kumkosa Yusuf. Macho yake yakafanya kiza kwa wingi wa huzuni, naye akiificha sana. Huzuni kubwa huleta ugonjwa wa macho unao itwa GLOKOMA, na weupe huzidi mpaka mtu mwisho anakuwa kipofu.
Rudi kwenye sura

* 85. Siku zikapita na Yaa'qub kazama katika majonzi yake. Wanawe wakaogopa isije kuwa khatari. Wakamkabili kumtaka apunguze huzuni yake, nao wako baina ya kumwonea huruma na kuchukia kuwa bado yu ngali akimkumbuka Yusuf wakamwambia: Kama hukujipunguzia nafsi yako hapana shaka kumkumbuka Yusuf kutakuzidishia machungu yako yakukondeshe mpaka ukaribie kufa, au ufe khasa!
Rudi kwenye sura

* 86. Maneno yao hayakumuathiri hata chembe. Akawajibu kwa kusema: Mimi sikukushitakieni, wala sikukutakeni mnipunguzie machungu yangu! Mimi sina ila Mwenyezi Mungu tu wa kumnyenyekea na kumshitakia dhiki zangu nzito na nyepesi. Wala siwezi kumficha hayo wala lolote nisilo liweza, kwani mimi natambua wema wake wa kutenda na ukunjufu wa rehema yake, jambo ambalo nyinyi hamlijui!
Rudi kwenye sura

* 87. Na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu ndio huhuisha matumaini. Kwa hivyo zile dhiki za moyo hazikuondoka kwa matarajio ya Yaa'qub kumrudia wanawe, na yakamtia katika moyo wake kuwa wangali wahai, na kwamba wakati wa kukutana nao ndio umefika. Akawaamrisha wanawe wende wakawatafute, akawaambia: Enyi wanangu! Rejeeni Misri muwe na kaka yenu, na mumtafute Yusuf na nduguye, muulize khabari zao kwa upole bila ya watu kujua. Wala msikate tamaa kwa Mwenyezi Mungu kuturehemu kwa kuwarudisha. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa wale wanao kanya.
Rudi kwenye sura

* 88. Nduguze Yusuf walimwitikia baba yao kwa matakwa yake. Wakatoka kwenda Misri, na wakajaribu kukutana na mtawala wake ambaye baadae ikadhihiri kuwa ndiye Yusuf! Walipo ingia kwake walisema: Ewe Mheshimiwa! Sisi na watu wetu tumepata shida ya njaa na madhara ya mwili na nafsi. Na tumekuletea mali chache ndio bidhaa yetu. Nayo ni ya kukataliwa kwa kuwa ni kidogo na mbaya, wala haitoshi kwa hayo tunayo taraji kwako. Lakini sisi tunataraji kwako utupimie kwa ukamilifu na utacho tuzidishia kiwe ni sadaka unayo tupa. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa wenye kutoa sadaka thawabu njema kabisa.
Rudi kwenye sura

* 89. Yusuf akaingiwa na huruma ya udugu ambayo inasamehe maovu. Akaanza kuwafunulia khabari zake kwa kuwaambia kwa lawama: Je! Mmejua ule uovu mlio mfanyia Yusuf kwa kumtumbukiza kisimani, na maudhi mlio mfanyia nduguye, mkafanya hayo kwa ujinga ulio kusahaulisheni huruma na udugu?
Rudi kwenye sura

* 90. Kuzinduliwa huku kwa furaha kuliwatambulisha kwamba huyu ndiye Yusuf. Wakamtazama kisha wakasema kwa yakini: Hakika wewe ndiye kweli Yusuf! Na Yusuf mwenye ukarimu aliwaambia kwa kuwakubalia: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufadhili kwa kutuvua kwa salama tusihiliki, na kwa kutupa hadhi na madaraka! Na hayo yamekuwa ni malipo ya Mwenyezi Mungu kwa usafi wangu na wema wangu. Na hakika Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa mtendaji mema na akaendelea nao.
Rudi kwenye sura

* 91. Wakasema: Uliyo sema ni kweli, na tunakuhakikishia kwa kiapo kwamba hapana shaka Mwenyezi Mungu amekutukuza kwa uchamngu, na subira, na sera njema. Na amekupa pia utawala na cheo cha juu. Na sisi hakika tulikuwa wenye kutenda dhambi kwa tuliyo kutendea wewe na nduguyo. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu ametudhalilisha kwako, na ametulipa malipo ya wenye kutenda dhambi.
Rudi kwenye sura

* 92. Yule Nabii mtukufu akawajibu kwa kusema: Hapana lawama kwenu leo, wala kusutana. Lenu kutoka kwangu ni msamaha ulio mwema kwa fadhila ya nasaba na haki ya udugu. Na namuomba Mwenyezi Mungu akusameheni na akughufirieni. Na Yeye ndiye Mwenye rehema kuu.
Rudi kwenye sura

* 93. Kisha Yusuf akawauliza khabari za baba yao. Walipo mwambia kuwa hali yake ni mbaya na hawezi kuona kwa wingi wa hamu na majonzi, aliwapa kanzu yake, na akawaambia: Rejeeni kwa baba yangu, na hii kanzu mwekeeni usoni pake. Kwa hivyo atakuwa na yakini kuwa mimi nimo katika salama, na moyo wake utajaa furaha, na Mwenyezi Mungu atamjaalia iwe ni sababa ya kurejea kuona kwake. Hapo tena njooni naye kwangu, na ahali zenu wote pamoja.
Rudi kwenye sura

* 94. Wakaondoka na ile kanzu. Na moyo wa Yaa'qub ulikuwa umezama kungojea nini litalo leta safari ya wanawe. Na Mwenyezi Mungu alikuwa yu pamoja naye katika kungojea huko, ikawa roho yake imeshikamana na roho zao. Basi ule msafara wao ulipo toka nchi ya Misri katika njia yake kumwendea yeye, aliwaambia ahali zake hayo kwa kusema: Mimi naihisi harufu ninayo ipenda ya Yusuf inanijaa. Na lau kuwa sikhofu kwamba mtanituhumu kwa niyasemayo ningeli kwambieni mengi ya Yusuf kuliko hizi hisiya na mawazo.
Rudi kwenye sura

* 95. Wale ahali zake wakamjibu jawabu kali wakiapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye yu ngali kuropokwa kwake na kupiswa kwake kwa uzee! Basi akajitayarisha alivyo jitayarisha kwa mapenzi yake yaliyo pita kiasi ya kumpenda Yusuf, na kuendelea kwake kumkumbuka na kutaraji kukutana naye.
Rudi kwenye sura

* 96. Akashikilia tamaa yake akingojea rehema ya Mwenyezi Mungu, na ahali zake wakashikilia kumdhania dhana mbovu mpaka alipo fika mtu aliye chukua kanzu na kumbashiria kwamba Yusuf yupo salama salmina. Ilipo wekwa kanzu usoni kwa Yaa'qub akainusa harufu yake, moyo wake ulijaa furaha, macho yake yakarejea kuona. Yule mjumbe alipo msimulia hali ya Yusuf, na kwamba anamtaka yeye asafiri ende pamoja na ahali zake, aliwageukia walio kuwa naye akiwakumbusha ule utabiri wake, na akiwakaripia kwa vile walivyo mkadhibisha. Akawataka wakumbuke yale aliyo wahakikishia pale punde kwamba yeye anaijua rehema ya Mwenyezi Mungu na fadhila yake wasio ijua wao.
Rudi kwenye sura

* 97. Hapo wakamkabili kwa kumtaka msamaha, wakimtaraji awasamehe, na awatakie kwa Mwenyezi Mungu maghfira kwa madhambi yao. Kwani wao walimhakikishia katika kule kutubu kwao kwamba wao walikuwa ni wenye kutenda madhambi.
Rudi kwenye sura

* 98. Akasema Yaa'qub nitaendelea kutaka msamaha kwa Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu. Na hakika Yeye peke yake ndiye mwenye maghfira ya milele na rehema ya daima.
Rudi kwenye sura

* 99. Yaa'qub akasafiri kwenda Misri pamoja na ahali zake mpaka akafika huko. Walipo ingia kwa Yusuf, naye alikuwa kawapokea kwenye milango ya Misr, huruma na shauku ilimpeleka kwa haraka kwa baba na mama yake! Akawakaribisha na akawataka wao na ahali zake wakae Misri kwa amani na salama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 100. Msafara ukenda ndani ya nchi ya Misri mpaka ukafika kwenye nyumba ya Yusuf. Wakaingia, na Yusuf akawatanguliza wazazi wake akawaweka kwenye kochi. Yaa'qub na ahali zake wakajaa furaha kwa uzuri wa mapokezi aliyo watengezea Mwenyezi Mungu katika mikono ya Yusuf. Kwani kwa hayo ukoo wote umekusanyika hapo baada ya mfarakano, na umetukuka makamu makubwa ya utukufu na hishima. Wakamuamkia maamkio yaliyo zowewa na watu tangu zamani ya kuwaamkia maraisi na watawala. Wakaonyesha unyenyekevu kwa utawala wake. Yale yalimkumbusha Yusuf ile ndoto yake ya utotoni. Akamwambia baba yake: Hii ndio tafsiri ya ndoto niliyo iota na nikakusimulia ya kwamba nimeota usingizini kuwa nyota kumi na moja na jua na mwezi zinanisujudia; ni hivi basi Mola wangu Mlezi ameitimiza, na amenitukuza na amenifanyia hisani. Amedhihirisha kuwa sina makosa, na akanitoa kifungoni, na akakuleteni kutoka jangwani tukutane, baada ya Shetani kutufisidi baina yangu na ndugu zangu, akawachochea dhidi yangu. Na haya yote yasinge kuwa bila ya Mwenyezi Mungu kuyafanya. Yeye ndiye wa kupanga na kuyafanya mambo yatimie kama atakavyo. Na Yeye ndiye Mwenye kuzunguka kila kitu kwa ujuzi wake, ambaye hukumu yake ni yenye kushinda katika kila jambo na kadhiya.
Rudi kwenye sura

* 101. Yusuf akamwelekea Mwenyezi Mungu akimshukuru kwa kuzihisabu neema zake juu yake, na akimwomba amzidishie fadhila zake, kwa kusema: Ewe Mola wangu Mlezi! Neema zako kwangu ni nyingi mno, na bora mno! Umenipa utawala, na nakuhimidi kwa hayo. Ukanitunukia ilimu ya kufasiri ndoto kama ulivyo nitunukia! Ewe Muumba mbingu na ardhi! Wewe ndiye uliye miliki mambo yangu yote, na Mtawala wa neema za uhai wangu na baada ya kufa kwangu! Nifungamanishe nawe kwa ulivyo waridhia Manabii wako katika Dini ya Kiislamu, na uniingize katika kundi la ulio waongoa kwenye wema miongoni mwa baba zangu, na waja wako walio wema, walio safika.
Rudi kwenye sura

* 102. Ewe Nabii! Haya tuliyo kusimulia ni katika khabari zilizo pita za kale. Hazikukufikia ila kwa wahyi ulio toka kwetu. Wala wewe hukuwapo pale nduguze Yusuf walipo kuwa wakipanga njama. Wala wewe hukuwa unavijua vitimbi vyao ila kwa kusimuliwa nasi.
Rudi kwenye sura

* 103. Na wapo wengi ambao tabia zao zina maradhi zinazo wazuia wasisadiki haya unayo funuliwa, hata moyo wako ukiwa una shauku namna gani waamini, au nafsi yako ikafanya juhudi gani waongoke.
Rudi kwenye sura

* 104. Wala hatukusudii kwa hadithi za uwongofu unazo waeleza kuwa ndio upate malipo au manufaa. Ikiwa hawaongoki hawa usiwahuzunikie. Mwenyezi Mungu atawaongoa watu wengineo. Kwani Sisi hatukuwateremshia wao tu peke yao. Na haya si chochote ila ni mawaidha, na mazingatio kwa kila aliye umbwa na Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi.
Rudi kwenye sura

* 105. Na dalili ni nyingi mno za kuonyesha kuwepo Muumba, na Upweke wake, na Ukamilifu wake, ziliomo katika mbingu na ardhi, ambazo wanaziona watu wako, na wanazipuuza kwa inda, hawataki kuzizingatia.
Rudi kwenye sura

* 106. Na kati yao wapo wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu, wanamkubali kuwa ni Mola Mlezi, na kwamba Yeye ni Muumba wa kila kitu. Lakini imani ya wengi wao haikusimama juu ya msingi madhubuti wa Tawhid! Basi hawaukubali Upweke wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya usafi. Lakini katika nafsi zao umo mchanganyiko wa imani unao wapelekea katika njia za washirikina, mapagani.
Rudi kwenye sura

* 107. Kwani wamechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, wakadhaminika isiwapate adhabu ya kuwagubika kwa nakama yake, kama ilivyo wafanyia walio watangulia kabla yao? Au Kiyama kisiwajie kwa ghafla, kikawatesa nao wameshikamana na ushirikina na ukafiri na kisha mwisho wao uwe Motoni?
Rudi kwenye sura

* 108. Ewe Muhammad! Wazindue mwisho wa uwezo wako, na waonyeshe hadi ya juhudi yako, uwaambie: Huu ndio Mwendo wangu na Njia yangu. Nawaita watu wafuate Njia ya Mwenyezi Mungu. Na mimi nimethibiti katika hili jambo langu, na kadhalika anayaitia hayo kila mwenye kunifuata na akaiamini sharia yangu. Na namtakasa Mwenyezi Mungu Subhanahu na kila kisicho kuwa laiki yake. Wala mimi simshirikishi Yeye na kitu chochote.
Rudi kwenye sura

* 109. Wala Sisi hatukuacha mtindo wetu katika kuwateuwa Mitume tulipo kuteuwa wewe, ewe Nabii! Wala hali ya kaumu yako haikuwa mbali na hali ya kaumu nyengine zilizo tangulia. Kwani hatukuwateuwa Malaika kabla yako, bali tuliwateuwa wanaume wanaadamu katika watu wa mijini, ukawateremkia Ufunuo, yaani Wahyi. Tukawatuma kuwa ni wabashiri na waonyaji. Wenye kuongoka wakawaitikia, na wapotovu wakawafanyia inda! Je, watu wako wameghafilika na kweli hii? Je, wamekalishwa kitako wasiweze kutembea wakaona hao wa kale tulivyo wateketeza duniani? Na mwisho wao ni Motoni; wakaamini wenye kuamini tukawaokoa na tukawanusuru duniani. Na malipo ya Akhera ni bora kwa wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu, wasimshirikishe wala wasimuasi. Zimeharibika akili zenu, enyi wakaidi, hata hamwezi kufikiri wala kuzingatia!
Rudi kwenye sura

* 110. Ewe Muhammad! Wala usione nusura yangu inakawia, kwani nusura yangu ipo karibu na hakika inakuja. Na Sisi tuliwatuma kabla yako Mitume, na kwa mujibu wa hikima yetu msaada wetu ulikawilia. Na wao wakawa wanaendelea kukanywa na watu wao, mpaka nafsi zilipo tikisika, wakahisi kukata tamaa, nusura yetu ikawadiriki; tukawaneemesha kwa kuwaokoa na kuwaletea amani wale walio stahili kutaka uwokofu kwetu, nao ni Waumini. Tukawageuzia maovu wale walio tenda dhambi kwa inadi na wakashikilia ushirikina. Wala hapana awezae kuizuia adhabu yetu isiwafikie watu wakosefu.
Rudi kwenye sura

* 111. Na Sisi tumekufunulia tuliyo kufunulia katika visa vya Manabii ili kuuthibitisha moyo wako, na iwe ni hidaya kwa watu wako. Na tumetengeneza mazingatio na waadhi wa kuwanawirisha wenye akili na busara, na wanao tambua kuwa Qur'ani ni haki na kweli. Hizi hazikuwa ni hadithi za kutunga, wala nganu za kuzua. Bali hakika ni kweli na ufunuo, wahyi, wenye kuhakikisha ukweli wa yaliyo pita katika Vitabu vya mbinguni, na walio kuja nayo Mitume wengine! Na zinabainisha yanayo hitaji kufafanuliwa katika mambo ya Dini, na zinaongoa kwendea katika Haki na Njia Iliyo Nyooka, na zinafungua milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu ili aongoke mwenye kufuata uwongofu wake, na akawa miongoni mwa Waumini wa kweli.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani