Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Hijr

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Hizi ni Aya za Kitabu cha kusomwa, chenye kubainisha, chenye kuweke wazi.
Rudi kwenye sura

* 2. Watapenda, na watatamani sana makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 3. Lakini sasa wamo katika kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye sura

* 4. Na ikiwa wao wanataka wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati wake maalumu.
Rudi kwenye sura

* 5. Hawatangulii wala hawataakhari.
Rudi kwenye sura

* 6. Na uovu wa hali yao na wingi wa kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha, hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
Rudi kwenye sura

* 7. Na hadi ya ukafiri wao walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
Rudi kwenye sura

* 8. Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
Rudi kwenye sura

* 9. Na hakika, kwa ajili ya kuwa Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote mpaka kusimama Kiyama.
Rudi kwenye sura

* 10. Na ewe Mtume Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
Rudi kwenye sura

* 11. Wala mtindo wao hao walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa wapotovu!
Rudi kwenye sura

* 12. Kama tulivyo itia Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
Rudi kwenye sura

* 13. Wakhalifu hao hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
Rudi kwenye sura

*14. Watu hao wanataka wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa. Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
Rudi kwenye sura

* 15. Bado wasingeli amini, na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo zao zimeenea ukafiri.
Rudi kwenye sura

* 16. Na Sisi tumeweka mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
Rudi kwenye sura

* 17. Lakini Sisi tumezihifadhi na kila shetani anaye stahiki kupigwa vimondo na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Rudi kwenye sura

* 18. Na yeyote katika hao mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo onekana wazi.
Rudi kwenye sura

* 19. Na tumekuumbieni ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
Rudi kwenye sura

* 20. Na tumekujaalieni katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
Rudi kwenye sura

* 21. Na hapana chochote cha kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu, kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
Rudi kwenye sura

* 22. Na Sisi tulipeleka pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani "Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides" na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko. Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
Rudi kwenye sura

* 23. Na ni Sisi tu peke yetu ndio tunavipa vitu vyote uhai, kisha tunavipelekea mauti, kwani uumbaji wote ni wetu.
Rudi kwenye sura

* 24. Na kila mmoja wenu ana muda wake alio pimiwa. Sisi ndio tunao ujua. Tunawajua walio tangulia kwa kufa na kuwa hai, na pia wanao taakhari.
Rudi kwenye sura

* 25. Na hakika walio tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake. Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. * 26. Na Sisi katika kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
Rudi kwenye sura

* 26. Na Sisi katika kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
Rudi kwenye sura

* 27. Na makhaluku wengine ni majini, ambao tuliwaumba mbele, alipo umbwa asili yake Iblisi kutokana na moto mkali mno unao toka katika tundu za mwili wa mtu.
Rudi kwenye sura

* 28. Ewe Nabii! Kumbuka asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote, kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
Rudi kwenye sura

* 29. Nikisha kamilisha kumuumba, na nikampulizia roho ambayo ninaimiliki, basi teremkeni kwa nyuso zenu mkimsujudia, kwa kumwamkia na kumhishimu.
Rudi kwenye sura

* 30. Wakasujudu wote kwa kuit'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 31. Lakini Iblisi alijivuna na akakataa kuwa pamoja na Malaika waliyo it'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 32. Hapo basi Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: Ewe Iblisi! Kitu gani kilicho kupelekea hata ukaasi na usiwe pamoja na wanyenyekevu walio sujudu?
Rudi kwenye sura

* 33. Iblisi akasema: Si shani yangu mimi kumsujudia mtu uliye muumba kwa udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umegeuka rangi, wenye kutiwa sura.
Rudi kwenye sura

* 34. Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ukiwa wewe umekuwa a'asi, umetokana na ut'iifu wangu, basi tokelea mbali kwenye Bustani hii! Kwani hakika wewe umefukuzwa kwenye rehema yangu na pahala pa hishima.
Rudi kwenye sura

* 35. Na Mimi nimekwisha kuhukumia ubaidike na rehema na utukufu mpaka Siku ya Kiyama, Siku ya Hisabu na Malipo. Na hapo ndipo utapo pata adhabu, wewe na wanao kufuata .
Rudi kwenye sura

* 36. Iblisi akasema, hali naye kesha kuwa ni mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu: Ewe Muumba wangu! Nipe muhula, nibakishe usinitwae mpaka Siku ya Kiyama, Siku watapo fufuliwa watu wakawa hai baada ya kufa kwao.
Rudi kwenye sura

* 37. Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Wewe utabakishwa, umepewa muhula,
Rudi kwenye sura

* 38. Mpaka wakati niliyo ukadiria, ninao ujua Mimi. Na kama utavyo kuwa mrefu una kikomo.
Rudi kwenye sura

* 39. Akasema Iblisi, mkhalifu, a'asi: Ewe Muumba wangu unaye nibakisha! Umenitakia upotofu, nami nikatumbukia ndani yake. Basi kwa sababu hiyo nahakikisha kuwa nitawapambia wanaadamu maovu wayaone mazuri, na nitafanya kila juhudi kuwapotoa wote!
Rudi kwenye sura

* 40. Wala hawatoepukana na upotovu wangu ila wale waja wako walio kufanyia ikhlasi Wewe na nisio weza kuzimiliki nyoyo zao kwa zilivyo kuwa imara kwa kukumbuka Wewe.
Rudi kwenye sura

* 41. Hakika usafi wa waja walio isafia niya Dini yao ndio Njia Iliyo Nyooka, na haki yangu nisiikiuke, kwani hao siwezi kuwapotoa. (Tafsiri hii yaonyesha maneno hayo ni ya Iblisi. Lakini Tafsiri nyengine zinasema maneno hayo ni ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano ya Abdulla Saleh, Abdulla Yusuf, Pickthall, Razi, Baidhawi, Qurtubi, Zamakhshari, Ibn Kathir, Assad.)
Rudi kwenye sura

* 42. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Hakika waja wangu walio nisafia Mimi Dini yao wewe huna uwezo wa kuwapoteza. Lakini wapotovu, walio zama katika upotovu, walio kufuata wewe, basi hao ndio unayo madaraka juu ya nyoyo zao.
Rudi kwenye sura

* 43. Na hakika Moto mkali mno ndio wameahidiwa hao wote kuwa ndiyo adhabu ya kutia uchungu.
Rudi kwenye sura

* 44. Wala huo Moto mkali hauna mlango mmoja tu, bali una milango saba kwa ajili ya wingi wanao stahiki kuingia humo. Na kila mlango una kundi lake makhsusi. Na kila kundi una cheo chake maalumu cha kulingana na uovu wake.
Rudi kwenye sura

* 45. Haya ni malipo ya wanao mfuata Shetani. Ama wale ambao Shetani kashindwa kuwapotoa, kwa kuwa wameweka kinga baina yake na nyoyo zao, hao watapata Mabustani yaliyo bora, na chemchem zinazo pita .
Rudi kwenye sura

* 46. Mola wao Mlezi atawaambia: Ingieni katika Bustani hizi kwa utulivu na amani. Kwani hapana khofu juu yenu, hamhuzunikii nyakati zenu.
Rudi kwenye sura

* 47. Na hakika watu wa Imani wataishi katika kheri hii na nafsi zao zimetua. Kwani tumezitoa chuki zilizo kuwamo katika nafsi hizo. Wote hao watakuwa ndugu waketi juu ya viti vya enzi zikitazamana nyuso zao kwa furaha na mahaba, wala hawawi mmoja nyuma ya mwenzie wakichunguliana visogoni.
Rudi kwenye sura

* 48. Hawapatwi na machofu huko. Na hiyo ni neema ya daima, wala hawatotoka humo milele.
Rudi kwenye sura

* 49. Ewe Nabii muaminifu! Wape khabari waja wangu wote kwamba Mimi ni Mwingi wa kughufiria na kusamehe kwa mwenye kutubu, akaamini, na akatenda mema. Na kwamba Mimi ni Mwingi wa kuwarehemu.
Rudi kwenye sura

* 50. Na wape khabari kwamba adhabu ninayo wateremshia wenye kuasi na kukufuru ni adhabu yenye kutia machungu kweli, na adhabu yoyote nyengineyo haihisabiwi kuwa ina machungu mbele ya hii.
Rudi kwenye sura

* 51. Ewe Nabii! Waambie pia, katika kubainisha rehema yangu makhsusi katika dunia na adhabu yangu kwa wenye kuasi humo, khabari ya Malaika walio mfikia Ibrahim kama wageni.
Rudi kwenye sura

* 52. Ewe Muaminifu! Watajie pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
Rudi kwenye sura

* 53. Wakasema: Usiogope, na tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa Ibrahim na Sara.
Rudi kwenye sura

* 54. Akasema: Vipi mnanibashiria mtoto na hali mimi nimekwisha patikana na udhaifu wa ukongwe. Kwa njia gani, basi, mnanibashiria jambo hili la ajabu?
Rudi kwenye sura

* 55. Wakasema: Sisi tunakubashiria jambo lilio thibiti, ambalo halina shaka kabisa. Basi usiwe katika wanao kata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 56. Ibrahim akasema: Mimi sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
Rudi kwenye sura

* 57. Alivyo kuwa kaanza kuzoeana nao, alisema: Ikiwa mmenibashiria khabari hii nzuri, je mna jambo gani jenginelo mlilo nalo baada ya haya, enyi wajumbe mlio tumwa na Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye sura

* 58. Wakasema hakika sisi tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
Rudi kwenye sura

* 59. Wala hakusalimika na huo ukhalifu na adhabu yake ila ahli zake yeye Luut'i. Basi hao Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha tuwaokoe wote.
Rudi kwenye sura

* 60. Na hatoangamia katika ahli zake ila mkewe, kwani yeye hakumfuata mumewe, bali yu pamoja na hao wakosefu ambao wanao stahiki adhabu.
Rudi kwenye sura

* 61. Wale Malaika walio tumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuteremsha yaliyo ahidiwa, walipo fika nchi ya Luut'i na watu wake,
Rudi kwenye sura

* 62. Luut'i aliwaambia: Watu nyinyi sikujuini, na nafsi yangu inatishika nanyi. Naogopa msituletee balaa.
Rudi kwenye sura

* 63. Wakasema: Usituogope, kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha, nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
Rudi kwenye sura

* 64. Nasi tumekujia kwa amri iliyo thaabiti isiyo na shaka, nayo ni kuiteremsha adhabu. Na kutimiza ahadi ni katika sifa yetu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 65. Ilivyo kuwa adhabu itawateremkia, basi wewe na ahli zako mlio andikiwa kuokoka, tokeni baada ya kwisha ingia usiku.
Rudi kwenye sura

* 66. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki hata mmoja wao.
Rudi kwenye sura

* 67. Asubuhi kulipo pambazuka waliwaona Malaika kwa sura ya binaadamu wazuri. Wao wale wakawafurahia, wakaja ili wafanye nao vitendo vyao viovu, vya kuwaingilia wanaume.
Rudi kwenye sura

* 68. Luut'i akaogopa wasije wakatenda vitendo vyao viovu. Akasema: Hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe kwa vitendo vyenu vibaya.
Rudi kwenye sura

* 69. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu Mtukufu! Msifanye uchafu wenu, mkanipatisha hizaya na madhila mbele yao!
Rudi kwenye sura

* 70. Wale wakhalifu wakasema: Kwani si tulikukataza wewe usimkaribishe mtu yeyote, na hivi sasa tena unatuzuia tusifanye nao tunayo yatamani?
Rudi kwenye sura

* 71. Ili kuwanabihisha njia ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
Rudi kwenye sura

* 72. Ewe Nabii Muaminifu! Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu, wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
Rudi kwenye sura

* 73. Na walipo kuwa wao wamo katika ulevi wao wa mghafala nyoyo zao na akili zao zikachotwa na ukelele mkali mno wa kutisha, wakati jua lilipo chomoza.
Rudi kwenye sura

* 74. Mwenyezi Mungu Aliye takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua. Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo wakawa wamezungukwa kila jiha.
Rudi kwenye sura

* 75. Haya yaliyo washukia kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
Rudi kwenye sura

* 76. Na mabaki ya mji huu yapo yamesalia. Nayo yapo njiani katika njia inayo pitiwa na watu. Anaye taka kuwaidhika kwayo anaweza kuwaidhika.
Rudi kwenye sura

* 77. Kwa kuwa mabaki yake yapo kwenye njia iliyo wazi ni dalili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutimiza onyo lake, na Waumini wenye kut'ii Haki wanatambua hayo.
Rudi kwenye sura

* 78. Kama kaumu ya Luut'i walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na maingiliano yao.
Rudi kwenye sura

* 79. Tukawateremshia nakama yetu. Na mabaki yao yapo njiani yanaonekana, na mpita njia akiwa ni mtu wa Imani basi anaweza kuzingatia kwayo.
Rudi kwenye sura

* 80. Na kama walio tangulia hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
Rudi kwenye sura

* 81. Tuliwabainishia hoja zenye kuonyesha uwezo wetu, na Utume wa Mtume wetu, nao wakayapuuza, wala wasiyafikiri.
Rudi kwenye sura

* 82. Nao walikuwa watu wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi zao na mali yao.
Rudi kwenye sura

* 83. Walipo kufuru na wakakanya, zikawajia sauti za kutisha, za kuonya kuteketea kwao, wakahiliki wakati wa asubuhi.
Rudi kwenye sura

* 84. Wala mali waliyo yachuma na majumba waliyo yajenga hayakuwalinda na hilaki iliyo wateremkia.
Rudi kwenye sura

* 85. Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama, na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
Rudi kwenye sura

* 86. Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu aliye kuumba na akakulea, ni Mwenye viumbe vyote, na anajua hali yako na yao. Yeye anastahiki umtegemezee mambo yako na yao. Naye anajua maslaha yako na yao.
Rudi kwenye sura

* 87. Ewe Nabii Muaminifu, tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika kila Sala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili. Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
Rudi kwenye sura

* 88. Ewe Mtume! Usivitazame kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki, na watu wa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 89. Ewe Nabii! Waambie makafiri wote: Mimi nakuonyeni na adhabu kali, na nakubainishieni maonyo yangu kwa hoja za kukata.
Rudi kwenye sura

* 90. Haya ni kama maonyo ya walio igawanya Qur'ani wakaifanya ati ni mashairi, na ukohani, na hadithi za kale na mengineyo. Nao wasiiamini juu ya kusimama hoja juu yao.
Rudi kwenye sura

* 91. Hao waliifanya Qur'ani vipande mbali mbali, nayo hali kuwa haikubali kugawika kwa umuujiza wake na ukweli wake.
Rudi kwenye sura

* 92. Ikiwa hiyo hali yao, basi Wallahi kwa Aliye kuumba akakulinda na akakulea, hapana shaka tutawahisabu wote Siku ya Kiyama,
Rudi kwenye sura

* 93. Kwa vitendo vyao vya kuudhi, na kufuru, na kejeli.
Rudi kwenye sura

* 94. Basi wewe tangaza wito wa Haki, wala usishughulike na wayatendao washirikina na maneno yao.
Rudi kwenye sura

* 95. Na hao washirikina wanao ukejeli wito wako hawatokushinda, wala hawatoweza kukuingilia kati baina yako na wito wako.
Rudi kwenye sura

* 96. Hao washirikina mawazo yao yamedhoofika, ndio wakafanya kuwa Mwenyezi Mungu anao miungu mingine ya masanamu. Na watakuja jua matokeo ya ushirikina wao itapo wateremkia adhabu chungu.
Rudi kwenye sura

* 97. Nasi tunajua dhiki ya moyo inayo kupata kwa wanayo yasema ya ushirikina na kejeli na dharau.
Rudi kwenye sura

* 98. Ikikupata dhiki hiyo mkimbilie Mwenyezi Mungu Mtukufu umwelekee, na umt'ii na umnyenyekee, na utake msaada kwa Sala, kwani humo ndio imo poza.
Rudi kwenye sura

* 99. Na shikilia ibada ya Mwenyezi Mungu aliye kuumba, akakulinda, mpaka ifike amri ya yakini, nayo ni Kiyama na miadi.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani