Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Kahf

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kushukuriwa kwa wema, anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye amemteremshia mja wake, Muhammad, hii Qur'ani. Na wala hakujaalia kuwa ndani yake kipo chochote cha dosari, kilicho kwenda kombo na kuacha usawa. Bali ndani yake mna Haki tupu, isiyo na shaka yoyote.
Rudi kwenye sura

* 2. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia Qur'ani imesimama, imenyooka sawa sawa katika mafunzo yake ili kuwaonya wanao kufuru na kukataa, kuwa watapata adhabu kali itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na iwape bishara njema wanao isadiki, ambao wanatenda vitendo vyema, ya kwamba watapata malipo mazuri.
Rudi kwenye sura

* 3. Malipo hayo ni Pepo watakayo kaa humo milele.
Rudi kwenye sura

* 4. Na kiwaonye kwa njia makhsusi wale walio msingizia Mwenyezi Mungu kuwa ana mwana, na hali Yeye ametakasika kuwa kama viumbe, akawa mwenye kuzaa au akazaliwa mtoto wake.
Rudi kwenye sura

* 5. Wala wao hawana ujuzi wowote wa hayo wala baba zao hawakuwa nao huo. Ni uzushi mkubwa mno huu wa kutoa neno hili vinywani mwao! Wayasemayo ni uzushi, na wala hapana uzushi mkubwa kushinda huu.
Rudi kwenye sura

* 6. Ewe Nabii! Usijihiliki nafsi yako bure kwa kuhuzunika na kusikitika kwa kuacha kwao kuitikia Wito wako, na kuisadiki hii Qur'ani.
Rudi kwenye sura

* 7. Sisi tumewaumba kwa kheri na shari, na tumevifanya vilio juu ya ardhi ni pambo lake kwa ajili ya manufaa ya watu wake. Hivyo tunawatendea vitendo kama ni mtihani wapate kudhihiri kati yao wenye a'mali njema. Basi aliye pumbazwa na ulimwengu, na asiishughulikie Akhera, huwa amepotea. Na aliye iamini Akhera, huyo huwa ameongoka.
Rudi kwenye sura

* 8. Baada ya kumalizika dunia Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya dunia kama ardhi tambarare isio na mimea baada ya kuwa imeamirika kwa mazao ya kijani yenye uhai.
Rudi kwenye sura

*9. Walio pumbazwa na starehe za dunia wanakanya kufufuliwa, ilihali hakika ya mambo inathibitisha pana uhai baada ya usingizi mrefu. Na hichi kisa cha Watu wa Pangoni kwenye mlima na bao lilio andikwa majina yao baada ya kufa kwao hakikuwa ni ajabu ya pekee, tukaziacha ishara zote nyenginezo. Ijapo kuwa kisa hicho si cha kawaida, lakini hakikuwa ndio cha ajabu kushinda ishara zetu nyengine zenya kuonyesha uweza wetu.
Rudi kwenye sura

* 10. Taja pale walipo kwenda hao vijana kwenye pango, wakafanya hapo ndipo pahali pa kujificha baada ya kukimbia ushirikina na washirikina kuhifadhi Dini yao. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe maghfira kutoka kwako, na utulinde na adui yetu, na tusahilishie hidaya na tawfiki katika mambo yetu!
Rudi kwenye sura

* 11. Tukaipokea dua yao hiyo, tukawalaza kwa salama katika hilo pango kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
Rudi kwenye sura

* 12. Kisha Mwenyezi Mungu aliwaamsha baada ya kulala kwa muda mrefu, ili matokeo yake yawe ni kudhihirisha ujuzi wetu ni nani katika makundi mawili aliye sibu kukisia muda wa kulala kwao.
Rudi kwenye sura

* 13. Ewe Mtume! Sisi tunakusimulia khabari zao kweli kweli: Hakika hao walikuwa vijana katika zama zilizo pita ambao walikuwa wameshika Dini ya Haki. Walimuamini Mola wao Mlezi kuwa ni Mmoja tu, na ilihali wamezungukwa na washirikina. Na Sisi tukawazidisha wawe na yakini. yenu kwa njia za kukufaeni katika maisha yenu. Haijuulikani kwa hakika ni nani hao Ahlil Kahf, wala zama zao, wala hilo pango lipo wapi walilo kimbilia hao vijana. Pamoja na hayo hapana ubaya kuchunguza, huenda pakapatikana mwangaza japo kidogo juu yake. Ilivyo kuwa Qur'ani Tukufu imetaja kuwa hao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi basi hapana budi kuwa wao na watu wao waliteswa kwa sababu ya Dini, hata wakaona hao vijana wakimbilie pangoni kujificha. Na Taarikhi ya zamani inataja kuwa yalikuwako mateso ya dini katika nchi za Mashariki ya kale yaliyo tokea nyakati mbali mbali. Tutataja katika yafuatayo mateso mawili huenda moja wapo likaelekea na kisa hichi:- Ya kwanza yalitokea zama za mfalme wa Kisaluki, Antiokhus IV, aliye itwa kwa jina la kupanga Nabivanis (kiasi ya 176-84 K.K.). Huyo alipo shika ufalme wa Shamu, na akawa amemili mno kwenye ustaarabu wa Kigiriki na ilimu zake, aliwalazimisha Mayahudi wa Palistina, nayo ilikuwa chini ya Shamu tangu mwaka 194 K.K. washike dini ya Kigiriki, na akavunja sharia zao, na akanajisi Hekalu lao kwa kuweka humo sanamu la Zeus, mungu mkuu wa Magiriki, juu ya madhibahu (kibulani), na kumtolea mihanga ya nguruwe humo. Tena huyo mfalme aliteketeza kwa moto nakla za Taurati zote alizo zipata. Kwa mwangaza huu yaonekana kuwa hawa vijana walikuwa ni Mayahudi, na kwao ni popote katika Palastina, au khasa ni katika Yerusalemu. Na ikawa wakaamka mnamo mwaka 126 B.K. zama za utawala wa Warumi wa Mashariki. Yaani kabla ya kuzaliwa Mtume Muhammad s.a.w. (nako kulikuwa kiasi mwaka 571 B.K.) kwa kiasi ya miaka mia nne na arubaini na tano takriban. Ama mateso ya pili yalitokea zama za Mfalme wa Ufalme wa Kirumi, Hadriatus (117-138). Mfalme huyu aliwatenda Mayahudi kama alivyo watendea Antiokhus tuliye kwisha mtaja sawa sawa. Matokeo ya hayo ni kuwa Mayahudi walitangaza uasi dhidi ya utawala wa Kirumi mwaka 132. Wakawafukuza askari wa ulinzi wa Kirumi, wakaiteka Yerusalemu, na wakatoa sarafu yao ya makumbusho ya ugombozi wa Mji Mtakatifu. Wakashika khatamu za utawala kwa muda wa miaka mitatu. Mwishoni Hadriatus na jeshi lake wakagutuka, wakaushinda uasi, na wakairudisha Palastina chini ya ut'iifu, na wakairudisha Yerusalemu, na wakauvunjilia mbali uwananchi wa Kiyahudi kabisa. Viongozi wa Mayahudi wakauwawa na Mayahudi wakauzwa sokoni kuwa watumwa. Matokeo ya hayo ni kuwa mambo yote ya Kiyahudi aliyapiga marfuku Hadriatus na akapiga marfuku mafunzo ya Kiyahudi na sharia zao. Kwa mujibu wa mwangaza huu wa taarikhi yaonekana kuwa vijana hawa walikuwa ni Mayahudi, na pahala pao ni popote katika Mashariki ya kale, au katika Yerusalemu yenyewe. Yaonekana kuwa waliamshwa mnamo mwaka 435 B.K., yaani kabla ya kuzaliwa Mtume wetu s.a.w. kwa miaka mia na thalathini. Yaonekana kuwa yale mateso ya mwanzo yameelekeana zaidi na kisa hichi cha Watu wa Pangoni, kwa sababu yalikuwa ni ya shida zaidi. Ama mateso ya Kikristo hayaelekeani na kuzaliwa kwa Mtume s.a.w.
Rudi kwenye sura

* 14. Na tulizithibitisha nyoyo zao juu ya Imani na subira ya kuvumilia shida, pale walipo simama mbele ya watu wao wakasema kwa kujifunga kwa ahadi: Ewe Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye wa Haki, Mola Mlezi wa mbingu na ardhi! Sisi hatumuabudu mungu mwenginewe. Wala hatutoiwacha itikadi hii. Wallahi! Tukisema jenginelo basi itakuwa tunasema lilio mbali kabisa na kweli!
Rudi kwenye sura

* 15. Kisha wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Hawa watu wetu wamemshirikisha Mwenyezi Mungu. Lau kuwa wameleta hoja iliyo wazi ya kuthibitisha ungu wa hivyo wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Hakika watu hawa ni wenye kudhulumu kwa vitendo vyao hivyo. Wala hapana aliye zidi udhaalimu kuliko mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo kwa kumsingizia washirika.
Rudi kwenye sura

* 16. Na wakaambiana wao kwa wao: Maadamu sisi tumejitenga nao hao katika ukafiri wao na ushirikina wao, basi kimbilieni pangoni mlinde Dini yenu. Mola wenu Mlezi atakukunjulieni maghfira yake, na atakusahilishieni mambo * 16. Na wakaambiana wao kwa wao: Maadamu sisi tumejitenga nao hao katika ukafiri wao na ushirikina wao, basi kimbilieni pangoni mlinde Dini yenu. Mola wenu Mlezi atakukunjulieni maghfira yake, na atakusahilishieni mambo
Rudi kwenye sura

* 17. Na lile pango lilikuwa kwenye mlima, lina nafasi ndani. Lilielekea kaskazini, linapigwa na upepo mzuri. Jua likichomoza muanga wake huwa kuliani mwao, na miale yake huwa mbali nao; na likichwa huwa kushotoni mwao. Kwa hivyo lile jua halipigi ndani ya pango, na kwa hivyo walisalimika na joto la jua, na upepo wa kaskazi unawaingilia. Na yote hayo ni katika ishara za kudra ya Mwenyezi Mungu. Na anaye pata tawfiki ya Mwenyezi Mungu kuokoka basi huokoka, na aliye kosa tawfiki hatopata wa kumwongoa baada yake.
Rudi kwenye sura

* 18. Na wewe ukiwaona utadhani wamacho, nao kwa hakika wamelala. Na katika usingizi wao tulikuwa tunawageuza kulia na kushoto mara kwa mara ili kuwahifadhi miili yao isidhurike na ardhi wakafanya madonda. Na mbwa aliye wafuata alinyoosha miguu yake ya mbele mlangoni, naye kalala pia kama kwamba yu macho. Ungeli watokea nao wamo katika hali ile ungeli toka mbio na moyo umejaa khofu kwa walivyo kuwa wanatisha katika kulala kwao. Hapana anaye waona ila atatishika nao. Hayo ili wasikaribiwe na mtu, wala wasiguswe na mtu mpaka wishe muda wao.
Rudi kwenye sura

* 19. Kama tulivyo walaza tuliwaamsha wapate kuulizana wenyewe kwa wenyewe wamelala muda gani? Mmoja wao akasema: Umekupitieni muda gani katika usingizi? Wakasema: Tumelala muda wa siku au baadhi ya siku. Walivyo kuwa hawana yakini nayo hayo wakasema: Mwachieni mambo haya Mwenyezi Mungu; kwani Yeye ni Mjuzi zaidi wa haya. Na ende mmoja wenu mjini, na achukue hizi sarafu za fedha achague chakula kizuri kabisa akuleteeni mle. Na awe na mafahamiano mema. Wala mambo yenu yasijuulikane na mtu yeyote.
Rudi kwenye sura

* 20. Kwani hao watu wakikuoneni watakuuweni kwa kukupopoeni mawe, au watakurejesheeni katika ukafiri kwa nguvu. Nanyi mkirejea ukafirini basi hamtaongokewa kabisa duniani wala Akhera.
Rudi kwenye sura

* 21. Na kama tulivyo walaza na tukawaamsha tulikuja watambulisha kwa watu wa ule mji wapate kujua kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua wafu ni ya kweli. Na Kiyama hapana shaka kitakuja. Watu wa ule mji wakamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kisha Mwenyezi Mungu akawafisha wale vijana. Watu sasa wakazozana kwa mintarafu yao. Baadhi yao wakasema: Jengeni jengo kwenye mlango wa pango, na tuwaache wao na shani yao. Kwani Mola wao Mlezi anaijua vyema hali yao. Na wakasema wenye kusikilizwa miongoni mwao: Hapa pahala pao tutafanya msikiti kwa sababu ya ibada.
Rudi kwenye sura

* 22. Watasema kikundi fulani katika Watu wa Kitabu (Biblia) wanao jiingiza katika mzozano wa kisa cha Ahlil Kahf (Watu wa Pangoni) kwamba hao walikuwa watatu na wa nne wao ni mbwa wao. Na wengine wanasema: Walikuwa watano, na wa sita wao ni mbwa wao. Tena wengine wanasema: Wao ni saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Waambie hawa wanao khitalifiana: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi ambaye hapana wa kumshinda ujuzi wake kuijua idadi yao. Wala hapana wajuao ila watu wachache tu ambao Mwenyezi Mungu amewajuvya hisabu yao. Basi wewe usijadiliane na hao wanao khitalifiana juu ya mas-ala ya hao vijana, ila majadiliano ya juu juu ya upole, bila ya kujaribu kuwakinaisha. Kwani wao hawakinaiki. Wala msimuulize yeyote kati yao juu ya khabari zao. Wewe hakika imekwisha kujia iliyo kweli isiyo na shaka.
Rudi kwenye sura

* 23. Wala usiseme kabisa kwa jambo unalo azimia kulendea na kujihimu kulitenda: Mimi nitalifanya hilo baadae!
Rudi kwenye sura

* 24. Ila kusema huko kuambatane na kupenda kwa Mwenyezi Mungu kwa kusema: Inshallah, yaani Mwenyezi Mungu akipenda. Na ukisahau jambo, basi kimbilia kumtaja Mwenyezi Mungu; na useme unapo azimia kufanya jambo na kuliambatanisha na kupenda kwa Mwenyezi Mungu: Huenda Mola wangu Mlezi akaniwafikisha kwenye bora kuliko nililo azimia kufanya, na lenye kuongoka zaidi.
Rudi kwenye sura

* 25. Na hakika hao vijana walikaa katika pango lao nao wamelala kwa miaka mia tatu, na ikazidi tisa. Aya hii inaonyesha ukweli wa ilimu ya Falaki (Astronomy), nayo ni kuwa ni miaka 300 kwa mwendo wa jua, na miaka 309 kwa hisabu ya mwezi unao fuatwa na Waislamu. Aya hii imeitangulia ilimu ya Falaki.
Rudi kwenye sura

* 26. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua zama zao zote. Kwani Yeye Subhanahu ndiye aliye khusika kujua siri za mbingu na ardhi. Jinsi gani kulivyo tukuka kuona kwake kwa viumbe vyote! Na jinsi gani kulivyo tukuka kusikia kwake kwa kila cha kusikilizana! Na hapana katika wa mbinguni na wa katika ardhi wa kuendesha mambo yao isipo kuwa Yeye. Na wala hapana wa kumshiriki katika hukumu yake kiumbe chochote.
Rudi kwenye sura

* 27. Ewe Mtume! Soma uliyo funuliwa kwa wahyi katika Qur'ani. Na katika hayo yamo uliyo funuliwa ya khabari za hao vijana. Wala usisikilize hayo maskhara yao ya kutaka ubadilishe muujiza wa Qur'ani kwa muujiza mwingine. Kwani hakika hapana wa kuyageuza anayo simulia Mwenyezi Mungu maneno ya haki katika miujiza yake. Hakika hapana awezae kubadilisha hayo. Wala usende kinyume na amri ya Mola wako Mlezi, kwani hapo tena hutapata wa kumkimbilia kukuhifadhi naye.
Rudi kwenye sura

* 28. Ewe Mtume! Shikamana na usuhuba wa masahaba wako Waumini, wanao muabudu Mwenyezi Mungu peke yake asubuhi na jioni daima, huku wanataka radhi zake. Wala jicho lako lisiwawache hao kuwaangalia wapinzani wa kikafiri kwa kutaka kustarehe nao katika mapambo ya maisha ya dunia. Wala usikubali kuwafukuza Waumini mafakiri katika baraza yako kwa kumridhisha huyo tuliye mghafilisha moyo wake na kutukumbuka Sisi, kwa kuwa yeye mwenyewe hakuwa tayari kwa hayo, na akawa ni mtumwa wa pumbao lake, na mambo yake katika vitendo vyake vyote hayakufuata njia iliyo sawa. Na anapo katazwa Nabii, basi ndio wanakatazwa wengineo (yaani sote sisi). Na hakika Nabii s.a.w. hataki maisha ya dunia na pumbao lake. Lakini makatazo hayo anaelekezewa Nabii ili wenginewe watahadhari na kutaka pumbao la dunia. Kwani ikiwa yaweza kuwa kwake kutaka pumbao la kimwili, basi kila mwanaadamu yaweza kuwa katika nafsi yake. Kwa hivyo ajilinde.
Rudi kwenye sura

* 29. Sema ewe Mtume!: Hakika haya niliyo kuja nayo ni kweli tupu iliyo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye taka kuyaamini na ayaamini. Kwani hiyo ni kheri yake mwenyewe. Na anaye taka kuyakataa na akatae. Kwani huyo haidhulumu ila nafsi yake mwenyewe. Hakika Sisi tumekwisha muwekea tayari anaye jidhulumu nafsi yake kwa ukafiri Moto utao mzunguka kama khema. Na hao walio dhulumu wakiomba wasaidiwe kwa maji huko katika Jahannamu, wataletewa maji kama mafuta yaliyo tibuka yamoto mno, hubabua nyuso kwa uvukuto wake! Kinywaji hicho ni kibaya mno, na Jahannamu ni pahali paovu pa mapumziko yao!!
Rudi kwenye sura

* 30. Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Dini ya Haki uliyo funuliwa wewe, na wakatenda aliyo waamrisha Mola wao Mlezi, nayo ni vitendo vyema, basi Sisi hatuto wapotezea ujira wao wa vitendo vyema walivyo vitenda.
Rudi kwenye sura

* 31. Watu hao watakuwa na Mabustani ambayo watastarehe ndani yake daima dawamu. Kati baina ya miti na majumba yake inapita mito, na watapambiwa yanayo onekana ni ya starehe katika dunia, kama mapambo ya dhahabu, na mavazi yao ni nguo za kijani za hariri za kila namna, wakiegemea juu ya makochi na matakia na mapazia. Watapata malipo bora, na Bustani nzuri ya kudumu na kustarehe. Humo watapata kila wakitakacho.
Rudi kwenye sura

* 32. Ewe Mtume! Bainisha baina ya hali ya makafiri matajiri na Waumini mafakiri kwa kuwapigia mfano ulio tokea hapo zamani baina ya watu wawili: kafiri na Muumini. Huyo kafiri alikuwa na vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende kwa ajili ya pambo na faida pia. Na baina ya hivyo vitalu tukaweka makulima mengine yaliyo stawi na kutoa mazao.
Rudi kwenye sura

* 33. Na kila kitalu kikawa kinatoa mazao yake kwa wingi na kubaariki. Wala hapana kilicho tindikia. Na tukapasua mto unamiminika kati yao.
Rudi kwenye sura

* 34. Na huyo mwenye vitalu alikuwa na mali mengine yenye kutoa mazao yake pia. Basi ikamuingia ghururi kwa neema ile. Katika ile ghururi yake akamwambia mwenzie yule Muumini nao walikuwa wakijadiliana: Mimi nina mali mengi kuliko wewe, na ninakushinda kwa nguvu za jamaa zangu na wasaidizi.
Rudi kwenye sura

* 35. Kisha akaingia katika kitalu chake kimojapo pamoja na yule mwenzie Muumini, naye huku amejaa ghururi, akamwambia: Sidhani kabisa kuwa kitalu hichi kitapotea!
Rudi kwenye sura

* 36. Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na pindi ikawa nikirejea kwa Mola wangu Mlezi kwa kufufuliwa kama unavyo dai wewe, basi Wallahi! Hapana shaka nitapata bustani bora kuliko kitalu hiki huko Akhera. Kwani mimi ni mtu wa neema kwa kila hali. Yeye huyu anakisia hayo ya ghaibu kwa haya yaliyoko sasa. Wala hajui kuwa Akhera malipo yake ni kwa Imani na vitendo vya kheri.
Rudi kwenye sura

* 37. Mwenzie Muumini akamjibu: Unajiachilia kumkufuru Mola wako Mlezi aliye kuumba tangu asli yako ya Adam kutokana na udongo, kisha kutokana na tone ya maji-maji ya mbegu ya uzazi, kisha akakufanya mtu aliye kamilika? Ikiwa unajiona bora kwa mali yako na jamaa zako, basi mkumbuke Mola wako Mlezi na asli yako ya udongo.
Rudi kwenye sura

* 38. Lakini mimi ninasema: Hakika aliye niumba mimi na akaumba ulimwengu wote huu ni Mwenyezi Mungu Mola wangu Mlezi. Na mimi namuabudu Yeye peke yake, wala simshirikishi na yeyote.
Rudi kwenye sura

* 39. Na lau kuwa ungeli sema unapo ingia katika hii bustani yako ya duniani na ukaangalia viliomo ndani yake: Haya Mashaallah! Ndio aliyo yataka Mwenyezi Mungu. Wala mimi sina nguvu ya kuyapata haya bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu. Hayo inge kuwa ni shukrani za kupelekea kudumu neema yako. Tena akazidi kumwambia: Ikiwa umeniona mimi ni duni kuliko wewe kwa mali na watoto na wasaidizi...
Rudi kwenye sura

* 40....basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa bora kuliko hiyo bustani yako, hapa duniani au kesho Akhera, na akaipelekea bustani yako kudra yake aliyo ikadiria, kama radi mathalan kutoka mbinguni. Na ikawa ardhi kavu inayo teleza haimei kitu, wala unyayo hautulii juu yake.
Rudi kwenye sura

* 41. Au maji yake yakazama katika ardhi, yasipatikane, wala usiweze kuyachota kwa kumwagia katika shamba.
Rudi kwenye sura

* 42. Mwenyezi Mungu kampatiliza yule kafiri, akayateketeza mavuno yote ya kitalu chake, na hicho kitalu chenyewe akakiangamiza, na akang'oa hata mizizi yake. Yule kafiri akabakia akipindua pindua viganja vyake kwa kusikitikia gharama alizo zitoa katika kukiamirisha kitalu chake, na baadae kuja kikapatilizwa na uharibifu. Akatamani lau kuwa hakumshirikisha Mola wake Mlezi na yeyote.
Rudi kwenye sura

* 43. Katika balaa hii hakuwa na jamaa wa kuja mnusuru badala ya Mwenyezi Mungu kama alivyo kuwa akijitapa. Wala hakuwa anaweza kujisaidia nafsi yake.
Rudi kwenye sura

* 44. Kwani katika kila hali nusura iko kwa Mwenyezi Mungu wa Haki peke yake. Na Yeye Subhanahu ni Mwema kwa mja wake Muumini, humkirimu kwa malipo, na humfanyia mema matokeo yake.
Rudi kwenye sura

* 45. Ewe Mtume! Watajie watu mfano wa maisha ya duniani, vipi uzuri wake na kupendeza kwake, na mara hupotelea mbali. Ni kama mfano wa maji yanayo teremka kutoka mbinguni yakamwagiwa mimea ikanawiri, ikastawi. Kisha punde si punde ikakauka, ikawa vibua vikavu vilivyo katika katika vikipeperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuleta na kuondoa akitakacho.
Rudi kwenye sura

* 46. Mali na wana ni pambo na starehe kwenu katika uhai wa duniani, na pia ndio nguvu zenu. Lakini vyote hivyo havina dawamu. Hivyo vina mwisho wake, havibakii. Na vitendo vyema vyenye kubaki ni bora kwenu mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye hukumimieni kwa ukarimu thawabu zake, na hivyo ndio bora ya matumaini ya binaadamu.
Rudi kwenye sura

* 47. Na ewe Mtume! Waonye watu kwa Siku ambayo vyote viliopo vitaondoka. Milima itaondoka, na mtaiona ardhi tupu wazi imetanda, hapana chochote kilicho kuwapo cha kuisitiri. Na tutawafufua watu kwa ajili ya hisabu, na hatutamwacha hata mmoja kati yao.
Rudi kwenye sura

* 48. Na Siku hii watu watahudhurishwa kwa makundi wakipangwa kwa masafu kwa ajili ya hisabu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atasema: Tumekufufueni kutokana na mauti, kama tulivyo kuumbeni pale mara ya mwanzo. Na mmetujia peke yenu, mmoja, mmoja, bila ya mali, na bila ya wana. Na duniani mlikuwa mkikanusha kufufuliwa na kuhisabiwa.
Rudi kwenye sura

* 49. Na katika mkono wa kila mmojapo kitawekwa kitabu cha vitendo vyake. Waumini watakiona na watafurahi kwa yaliyomo humo. Na wakanushaji wataona nao wamejaa khofu kwa vitendo viovu viliomo humo. Watasema wakisha ona hayo: Hilaki gani hii! Tunastaajabia kitabu hichi hakikuacha hata dogo katika vitendo vyetu, wala kubwa, ila kimetuandikia! Na wataona malipo ya waliyo yatenda ni ya haki. Wala Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote katika waja wake.
Rudi kwenye sura

* 50. Ewe Mtume! Watajie mwanzo wa kuumbwa kwao, ili wajue kuwa wao wametokana na udongo, basi wasikae wakidanganyika na hayo waliyo nayo, wakamnyenyekea Iblisi, adui wa baba yao. Kwani yeye alikuwa katika majini, akajivuna, na akamuasi Mwenyezi Mungu. Basi yawaje baada ya kwisha jua khabari zake mkamfanya yeye na kizazi chake kuwa ndio wasaidizi wenu badala ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio adui zenu! Badala hii ni ovu kwa mwenye kuidhulumu nafsi yake na akamt'ii Shetani.
Rudi kwenye sura

*51. Mimi sikumwonyesha Iblisi wala dhuriya zake nilipo umba mbingu wala ardhi, wala sikuwashuhudisha baadhi yao nilipo waumba wenzao ili wanisaidie. Wala sikuwa nina haja ya msaidizi wowote, licha kuwa nikatafute wapotovu ndio wawe wasaidizi wangu. Basi yawaje mnakwenda mt'ii Shetani na mkaniasi Mimi?
Rudi kwenye sura

*52. Watajie siku atayo waambia Mwenyezi Mungu washirikina: Waiteni hao mlio kuwa mkidai duniani kuwa ni washirika wangu katika ibada ili wakuombeeni kwa mujibu wa madai yenu. Nao watawaita, na hao hawato waitikia. Nasi tumejaalia sasa hapana baina yao ila ni maangamio tu kwa makafiri, baada ya kuwa duniani walikuwa na mawasiliano ya ibada na mapenzi.
Rudi kwenye sura

*53. Na wakosefu watauona Moto na watayakinika kuwa hapana shaka watauingia tu. Wala hawatakuwa na pahala pengine badala yake.
Rudi kwenye sura

*54. Na Mwenyezi Mungu amewatajia watu katika Qur'ani hii, wanayo ikanusha na wakataka waletewe muujiza mwenginewe, mifano namna kwa namna, ili wapate kuwaidhika kwayo. Lakini mwanaadamu tabia yake ni kupenda kubishana. Akiwa kafiri basi atabisha hata kwa uwongo.
Rudi kwenye sura

*55. Na hapana lililo wazuia washirikina kuamini zilipo wafikia sababu za kuongoka, nazo ni huyu Mtume na Qur'ani, isipo kuwa ukaidi wao na kumtaka Mtume awaletee aliyo waletea Mwenyezi Mungu wale watu wa zamani, nayo ni kuangamizwa moja kwa moja kama kulio wapata hao wa kale, au awaletee adhabu ya dhaahiri hivi.
Rudi kwenye sura

*56. Lakini Mwenyezi Mungu hawatumi Mitume wake ila kwa ajili ya kutoa bishara njema na kuonya. Wala hawatumi kwa ajili ya hao wenye inda wawatake walete muujiza makhsusi. Lakini walio kufuru wanaacha hoja, na wanabishana na Mitume kwa upotovu ili waipotoe Haki. Na msimamo wao kwa Qur'ani na maonyo ni msimamo wa mwenye kejeli na maskhara ambaye hana makusudio ya kutafuta hakika ya mambo.
Rudi kwenye sura

* 57. Na hapana yeyote aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko huyo anaye waidhiwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi naye asizingatie, na akasahau nini matokeo ya maasi yake anayo yatenda! Hakika Sisi kwa sababu ya kuelekea kwao kwenye ukafiri tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao, basi nyoyo zao hazitambui wala haziingii mwangaza. Na masikioni mwao tumetia uziwi basi hawasikii la kuwafahamisha! Nawe, ewe Mtume! Ukiwaita kwenye Dini ya Haki hawato ongoka maadamu tabia yao ni hii.
Rudi kwenye sura

* 58. Na Mola wako Mlezi Mtukufu Mwingi wa kusamehe makosa ya waja wake, Mwenye rehema kunjufu kwa mwenye kumuelekea, lau angeli penda kuwatwaa kwa maovu wayatendayo basi angeli wapatiliza upesi upesi kama alivyo kwisha watangulizia wenginewe. Lakini hii ni hikima yake aliyo ikadiria. Anawaakhirisha mpaka ufike wakati atapo waonjesha adhabu kali kabisa. Na hapo hawatopata pa kukimbilia na kuwalinda.
Rudi kwenye sura

* 59. Na hii basi ndio miji ya kale tuliyo iteketeza pale watu wao walipo dhulumu kwa kuwakanusha Mitume wao. Na Sisi tukawawekea miadi ya kuwaangamiza isiyo na khitilafu. Hali kadhaalika itakuwa ya hao katika kaumu yako wanao kanusha, ikiwa hawaamini.
Rudi kwenye sura

* 60. Na hakika hapana mtu anaye jua ya Mwenyezi Mungu ila Yeye Mwenyewe anapo mpa kipawa hicho Nabii au mtu mwema. Ewe Mtume! Simulia kuwa Musa bin Amran alimwambia kijana wake, mtumishi wake, mwanafunzi wake: Sitoacha kwenda mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au basi nitaendelea kwenda tu muda mrefu.
Rudi kwenye sura

* 61. Basi Musa na kijana wake walipo fikilia pahala panapo kusanyika bahari mbili wakamsahau samaki wao walio kuwa wamemchukua kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Akatumbukia baharini, akashika njia yake katika maji!
Rudi kwenye sura

* 62. Musa na kijana wake walipo fika mbali na pahala pale, na wakaona njaa na machofu Musa akamwambia kijana wake: Tupe cha kukila. Hakika tumepata taabu na mashaka katika safari yetu hii.
Rudi kwenye sura

* 63. Kijana wake akasema: Unakumbuka? Pale tulipo pumzika kwenye lile jabali, basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha ila Shetani. Na hapana shaka samaki yule katumbukia baharini. Na mimi hakika najistaajabia kusahau kwangu huku.
Rudi kwenye sura

* 64. Musa akamwambia: Haya yaliyo tokea ndiyo tuliyo kuwa tunayataka kwa mujibu wa hikima anayo itaka Mwenyezi Mungu. Basi wakarejea nyuma kwa njia yao ile ile waliyo jia, wakizifuata nyayo zao.
Rudi kwenye sura

* 65. Mpaka wakafika kwenye lile jabali. Hapo wakamkuta mja miongoni mwa waja wangu walio wema, tuliye mpa hikima, na tukampa ujuzi mwingi kutokana kwetu.
Rudi kwenye sura

* 66. Musa akamwambia yule mja mwema: Je nende nawe upate kunifunza nami aliyo kufunza Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye sura

* 67. Akamwambia hutaweza kustahamili kufuatana nami.
Rudi kwenye sura

* 68. Na utawezaje kustahamilia jambo lisilo pata kukufika mfano wake?
Rudi kwenye sura

* 69. Musa akasema: Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mimi ni mwenye kusubiri, na mt'iifu kwako kwa yote utayo niamrisha.
Rudi kwenye sura

* 70. Yule mja mwema akasema: Basi ukinifuata na ukayaona usiyo yafahamu, usiingie kuniuliza mpaka nianze mimi kukusimulia.
Rudi kwenye sura

* 71. Wakatoka wakitambaa na mfukwe wa bahari mpaka wakakuta jahazi wakaipanda. Yule mja mwema akaitoboa jahazi ile nayo imo safarini. Musa akapinga kwa kusema: Umeitoboa makusudi upate kuwazamisha watu wake? Ama hakika umefanya jambo ovu!
Rudi kwenye sura

* 72. Yule mja mwema akasema: Mimi nilikwisha kwambia kuwa hakika wewe hutoweza kusubiri kuwa nami.
Rudi kwenye sura

*
Rudi kwenye sura

* 74. Na baada ya kutoka kwenye jahazi ile wakaingia kuendelea na safari yao. Njiani wakamkuta kijana. Yule mja mwema akamuuwa yule kijana! Musa akasema kwa kuchukia: Unakwenda muuwa mtu asiye na kosa lolote, na wala hakumuuwa mtu yeyote? Hakika umefanya jambo ovu kweli kweli!
Rudi kwenye sura

* 75. Mja mwema akamwambia Musa: Mimi nalikwambia kwamba wewe hutaweza kustahamili ukanyamaza kimya usiniulize.
Rudi kwenye sura

* 76. Musa akasema: Nikikuuliza lolote baada ya mara hii basi usifuatane nami, kwani umekwisha fikilia kiwango cha kupata udhuru wa kutokuwa nami.
Rudi kwenye sura

* 77. Wakenda hata wakafika kwenye mji. Wakawataka watu wake wawape chakula, wakakataa kuwakirimu. Wakakuta ukuta umeinama wakaribia kuanguka. Yule mja mwema akaudiriki. Akaujenga mpaka akausimamisha sawa. Musa akasema: Ungeli taka ungeli weza kudai ujira kwa kazi uliyo ifanya.
Rudi kwenye sura

* 78. Mja mwema akasema: Huku kutaaradhi kwako mara kwa mara kwa niyatendayo mimi ndio sababu ya kufarikiana mimi nawe. Sasa basi nitakueleza hikima ya yote haya ambayo wewe huyajui undani wake, wala hukuweza kuyasubiria yaliyo fichikana ukangojea kujua hakika yake na siri yake.
Rudi kwenye sura

* 79. Ama ile jahazi niliyo itoboa ilikuwa ni ya watu wanyonge wenye haja, ambao kazi yao ni ya baharini wakitafuta riziki yao. Basi mimi nikataka kukitia ila chombo chao kisitakikane. Kwani nyuma yao yuko mfalme mtindo wake ni kupokonya kila jahazi nzima. (Kughusubu, kupokonya, hata kukiitwa "kutaifisha" ni dhambi kubwa kabisa kwa Mwenyezi Mungu, kwani ni dhulma.)
Rudi kwenye sura

* 80. Ama yule kijana niliye muuwa, baba yake na mama yake walikuwa ni Waumini. Tulikuwa tunajua kuwa angeli ishi angeli kuwa ndio sababu ya ukafiri wao.
Rudi kwenye sura

* 81. Basi tukataka kwa kumuuwa huyo mtoto Mwenyezi Mungu awape badala yake aliye bora zaidi kwa dini, na mwema zaidi, na mwenye huruma.
Rudi kwenye sura

* 82. Ama ule ukuta nilio usimamisha, bila ya ujira, ulikuwa wa vijana wawili mayatima katika watu wa ule mji. Na chini yake ilikuwako khazina walio achiwa na baba yao. Naye alikuwa ni mtu mwema. Basi Mwenyezi Mungu alitaka kuwahifadhia khazina yao ile mpaka wakue wawe na akili zao, na wajitolee wenyewe khazina yao kuwa ni rehema kwao, na kumtukuza baba yao kwa kupitia dhuriya zake. Nami sikufanya niliyo yafanya kwa jitahada ya nafsi yangu. Bali nimefanya hayo kwa kuongozwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni tafsiri ya hayo yaliyo fichikana kwako wewe Musa, nawe usiweze kuyavumilia.
Rudi kwenye sura

* 83. Ewe Mtume! Baadhi ya makafiri wanakuuliza khabari za Dhul-Qarnaini. Waambie nitakusimulieni baadhi ya khabari zake.
Rudi kwenye sura

* 84. Tumemtilia nguvu amri yake katika ardhi, akiendesha humo mambo kwa mazingatio yake na utawala wake. Na tukampa ujuzi mwingi kwa njia ambazo kwazo akiweza kuongoza mambo.
Rudi kwenye sura

* 85. Kwa kutumia njia hizo aliweza kueneza madaraka yake katika ardhi, na akafuata njia mpaka akafika huko magharibi kunako kuchwa jua.
Rudi kwenye sura

* 86. Akenda mpaka akafika pahala mbali huko upande wa magharibi, akalikuta jua kwa linavyo onekana kwa macho kama kwamba linazama pahala penye chemchem ya maji ya moto na matope meusi. Na karibu ya chemchem hii Dhul- Qarnaini aliwakuta watu makafiri. Mwenyezi Mungu akamtia moyoni mwake afanye mojapo ya mambo mawili: Ama awaite kwenye Imani, na hili kwa hakika ni jambo zuri; au awapige vita ikiwa hawakuitikia wito wa Imani.
Rudi kwenye sura

* 87. Dhul-Qarnaini akawatangazia: Katika wao aliye jidhulumu nafsi yake kwa kubakia katika ushirikina, basi amestahiki adhabu ya duniani kutokana naye, na kisha atarejea kwa Mola wake Mlezi. Naye atamuadhibu adhabu kali wasio ijua.
Rudi kwenye sura

* 88. Na ama mwenye kumuitikia, na akamuamini Mola wake Mlezi, na akatenda mema, basi atapata malipo mazuri Akhera, na hapa duniani tunamchukulia kwa upole na wepesi.
Rudi kwenye sura

* 89. Kisha Dhul-Qarnaini akaendelea vile vile huku akiomba tawfiki ya Mwenyezi Mungu, na akafuata njia ya kufikilia matokea jua upande wa mashariki.
Rudi kwenye sura

* 90. Hata akafika linapo chomoza jua, kwa ionekanavyo kwa macho, mwisho wa majenzi. Akawaona watu wanaishi katika ushenzi kabisa. Hawana hata cha kuwasitiri na joto.
Rudi kwenye sura

* 91. Na kama Dhul-Qarnaini alivyo waita watu wa magharibi waje kuamini basi kadhaalika aliwaita hawa, na akenda nao mwendo ule ule wake wa mwanzo.
Rudi kwenye sura

* 92. Kisha akaendelea vile vile akitumia mbinu alizo msahilishia Mwenyezi Mungu za kumpa tawfiki, akishika njia baina ya mashariki na magharibi.
Rudi kwenye sura

* 93. Mpaka akafika - katika safari yake ya tatu - pahala mbali baina ya milima miwili mirefu...Na huko akakuta watu ambao hawafahamu wanalo ambiwa ila kwa uzito na mashaka. Hiyo ngome au boma baina ya milima miwili iliyo tajwa katika maelezo ya juu ni milima ya Azarbajan na Arminia, na kauli nyingine ni kaskazini ya mwisho katika jimbo la Turkistan.
Rudi kwenye sura

* 94. Walipo ziona nguvu zake na uwezo wake wakamtaka awasimamishie ngome ya kuwalinda na Juju-wa-maajuju. Nao hao ni watu wanao waonea maya, na wanawafisidia na kuwaharibia nchi yao. Na wao walikuwa watayari wamlipe ujira kwa kazi hiyo.
Rudi kwenye sura

* 95. Akawajibu kwa kuwaambia: Mali na madaraka aliyo nijaalia Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko hayo mnayo taka kunipa. Akaanza kusimamisha hiyo ngome, na akawataka wamsaidie kama wawezavyo kwa watu na zana ili awatimizie wayatakayo.
Rudi kwenye sura

* 96. Akawataka wamkusanyie vipande vya chuma. Wakakusanya kama alivyo taka. Akajenga kwa hivyo ngome ndefu iliyo lingana na kingo za milima hiyo miwili. Kisha akawaamrisha wawashe moto, wakauwasha, mpaka chuma kikayayuka. Tena akamimina juu yake shaba iliyo kwisha yayushwa; ikawa ngome madhubuti, haipitiki.
Rudi kwenye sura

* 97. Basi wale mahasidi hawakuweza kulikwea lile boma, jinsi lilivyo kwenda juu, wala kulitoboa kwa ugumu wake.
Rudi kwenye sura

* 98. Dhul-Qarnaini alipo kwisha jenga ile ngome alisema kumshukuru Mwenyezi Mungu: Ngome hii ni rehema iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi kwa ajili ya waja wake. Na itabaki hivi hivi imesimama mpaka ije amri ya Mwenyezi Mungu kuiteketeza. Hapo tena itakuwa sawa sawa na ardhi. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima itimie bila ya muhali.
Rudi kwenye sura

* 99. Na tangu kujengwa boma hilo Juju-wa-maajuju wakabaki nyuma yake wakipambana wenyewe kwa wenyewe, na wengine wakasalimika na shari yao. Ikifika Siku ya Kiyama likapulizwa baragumu Mwenyezi Mungu atawakusanya viumbe wote kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye sura

* 100. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaonyesha wazi makafiri Jahannamu iwatie kitisho na awatumbukize humo.
Rudi kwenye sura

* 101. Na hayo ni kwa kuwa macho yao walipo kuwa duniani yalikuwa yameghafilika hayaoni Ishara za Mwenyezi Mungu kama kwamba yamezibwa na pazia; na walikuwa kwa upotovu wao hawawezi kusikia Wito wa Haki, kama mtu aliye kuwa kiziwi. "Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia": Ni wale ambao macho yao yameghafilika na kunizingatia Mimi katika mbingu na ardhi. Na kwa hivyo hii Aya tukufu inazindua watu wazingatie yote yalio wazunguka yanayo onyesha Ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 102. Je, macho ya makafiri yamepofuka hata wakadhani kwamba kuwafanya watumwa wangu, Malaika na Isa, kuwa ni miungu, wakiwaabudu badala yangu Mimi, kutawapa manufaa na kuwakinga na adhabu? Hakika Sisi tumewaandalia Jahannamu ndio pahali pao pa kukaa wapate huko malipo wanayo yastahiki.
Rudi kwenye sura

* 103. Ewe Mtume! Waambie hawa makafiri: Je, nikutajieni watu watao pata khasara mno kwa vitendo vyao na watao kosa thawabu?
Rudi kwenye sura

* 104. Ni hao vilio haribika vitendo vyao katika maisha ya duniani kwa kuharibika itikadi yao, na hali wao wanaitakidi kuwa ndio wanafanya vitendo vyema!
Rudi kwenye sura

* 105. Hao ndio walio zikataa dalili za uwezo wa Mwenyezi Mungu, na wakaikanusha Siku ya kufufuliwa na kuhisabiwa. Basi vitendo vyao vimepotea bure, na Siku ya Kiyama watastahiki kudharauliwa na kupuuzwa, kwani hawana a'mali ya kutiwa maanani!
Rudi kwenye sura

* 106. Hayo ndiyo tuliyo yabainisha na tukayapambanua, hali ya hawa; na malipo yao kwa hayo ni Jahannamu kwa sababu ya kufuru zao na kuzifanyia maskhara Ishara za Mwenyezi Mungu alizo ziteremsha, na Mitume alio watuma.
Rudi kwenye sura

* 107. Hakika walio thibiti katika Imani na wakatenda mema, malipo yao ni Bustani za Firdausi watazo ziingia.
Rudi kwenye sura

* 108. Wataneemeka milele, wala hawatataka badala yake chochote.
Rudi kwenye sura

* 109. Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika ujuzi wa Mwenyezi Mungu umekusanya kila kitu. Na lau kuwa maji ya baharini ni wino wa kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu yanayo onyesha ujuzi wake na hikima yake, basi wino huo ungeli malizika, na hata ungeli ongezwa wino mwingine kama huo, kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu!
Rudi kwenye sura

* 110. Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika mimi ni mtu tu kama nyinyi, nimetumwa kwenu, nikufunzeni aliyo nifunza Mwenyezi Mungu. Nimefunuliwa (yaani nimepewa Wahyi) ya kwamba Mungu wenu ni Mmoja, hana mshirika wake. Anaye tumai kukutana na Mwenyezi Mungu na kupata malipwa yake, basi naatende vitendo vyema kwa usafi wa niya, na ajitenge mbali na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote katika ibada.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani