Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Jaathiya

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. H'a Mim. Hizi ni harufi mbili katika harufi za kutamkwa, zimeanzia Sura hii kama ada ya Sura nyingi katika Qur'ani ambazo zimeanzia kwa harufi kama hivi ili kuashiria kuwa washirikina wameshindwa kuleta mfano wake, ijapo kuwa hii Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi wanazo zitumia katika maneno yao.
Rudi kwenye sura

* 2. Huu mteremsho wa Qur'ani umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Asiye shindika, Mwenye hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
Rudi kwenye sura

* 3. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi ni katika ufundi wa namna ya pekee wa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka ni dalili zenye nguvu kabisa katika Ungu wake na Upweke wake, ambao wanauamini wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu kwa maumbile yao yaliyo sawa.
Rudi kwenye sura

* 4. Na vile Mwenyezi Mungu kukuumbeni nyinyi, enyi watu, kama mlivyo, mna sura nzuri, na umbo la peke yenu, na mnavyo khitalifiana baina ya wanaadamu na wanyama na mkaenezwa ulimwenguni, na manufaa mbali mbali, bila ya shaka ni Ishara zenye nguvu na ziwazi kwa watu wanao tafuta yakini ya mambo yao kwa kuzingatia na kufikiri.
Rudi kwenye sura

* 5. Na katika kukhitalifiana usiku na mchana, kwa urefu na ufupi, na mwangaza na giza, na kupeana zamu kwa nidhamu iliyo thibiti, na katika mvua anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kufa kwake kwa ukame, na kuziendesha pepo pande mbali mbali nazo zinakhitalifiana kwa ubaridi na joto, na nguvu na udhaifu, ni alama zilizo wazi za kuonyesha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kufikiri kwa akili zao, wakafikilia yakini yao.
Rudi kwenye sura

* 6. Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo eleza uumbaji alio ufanya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu. Tunakusomea wewe katika Qur'ani kwa ulimi wa Jibrili, nazo Aya hizo ni za haki. Ikiwa hao hawaziamini hizi basi maneno gani watayasadiki baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Qur'ani na Aya zake
Rudi kwenye sura

* 7. Atapata maangamizo makubwa kila anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo mbaya, na mwenye kukithiri madhambi yake kwa kitendo hicho!
Rudi kwenye sura

* 8. Mzushi kama huyu husikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, nazo zinasema haki tupu. Kisha yeye huendelea na ukafiri wake kwa kutakabari, akaikataa Imani. Hali yake ni hali ya asiye pata kuzisikia Aya. Basi ewe Nabii! Mbashirie, kwa kumkejeli, kuwa atapata adhabu chungu kwa huko kushikilia kwake kitendo kitacho mletea adhabu hiyo.
Rudi kwenye sura

* 9. Na huyu mwenye inda, akijua kitu kidogo katika Aya za Mwenyezi Mungu huzifanya Aya zote za Mwenyezi Mungu ni kitu cha kufanyia maskhara na mzaha. Wazushi hao wingi wa madhambi watapata adhabu ya kuwadhalilisha kwa kiburi chao.
Rudi kwenye sura

* 10. Nyuma yao ipo Jahannamu inawangojea, na walicho kichuma duniani hakitawapunguzia hata chembe ya adhabu yake. Wala hiyo miungu ya uwongo walio ifanya ndio ya kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu, haitawakinga na chochote katika adhabu yake. Na wao watapata mateso makubwa, kwa kitisho chake na ukali wake.
Rudi kwenye sura

* 11. Hii Qur'ani ni ushahidi kaamili wa Haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na hao wanao zikataa hoja zilio kusanywa na Qur'ani zilizo toka kwa Muumba wao na Mlezi wao watapata adhabu kali mno miongoni mwa namna za adhabu.
Rudi kwenye sura

* 12. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ikutumikieni bahari ili marikebu zipate kwenda juu yake kwa idhini yake, na uwezo wake, zikikubebeni nyinyi na bidhaa zenu, na ili mtafute kutokana na fadhila za Mwenyezi Mungu mali ya baharini kwa kupata manufaa ya ujuzi, na biashara, na jihadi, na zawadi, na uvuvi, na kutoa vyombo, na ili mpate kushukuru neema zake kwa kumsafia Dini Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 13. Na akakudhalilishieni vyote viliomo mbinguni, nyota zenye kung'ara na sayari, na vyote viliomo kwenye ardhi, makulima, mifugo, maji, moto, hewa, na jangwa, vyote hivyo vinatokana na Yeye Mtukufu, ili akuenezeeni manufaa ya uhai. Hakika katika hizo neema zilizo tajwa zipo Ishara zenye kuonyesha kudra yake kwa watu wenye kuzingatia Ishara.
Rudi kwenye sura

* 14. Ewe Mtume! Waambie wanao msadiki Mwenyezi Mungu na wanakufuata wewe, wasamehe maudhi yanayo wafikia kutokana na watu ambao hawataraji kuja siku za Mwenyezi Mungu za kuwalipa watu kwa kheri na shari kwa mujibu walivyo.
Rudi kwenye sura

* 15. Mwenye kutenda mema atapata ujira wake na thawabu mwenyewe; na mwenye kutenda uovu basi dhambi za kitendo chake zitamuangukia mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Muumba wenu kwa ajili ya malipo.
Rudi kwenye sura

* 16. Ninaapa kwa hakika tumewapa Wana wa Israili Taurati, na hukumu iliomo ndani yake, na Unabii ulio funuliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na tumewaruzuku kheri namna mbali mbali, na tumewafadhilisha wao katika neema nyingi juu ya viumbe vyote.
Rudi kwenye sura

* 17. Na tumewapa dalili wazi katika mambo ya Dini yao. Basi haikutokea khitilafu baina yao ila baada ya kwisha wajia ujuzi wa hakika ya Dini na hukumu zake. Na hayo ni kwa uadui na uhasidi tu ulio baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atapambanua baina ya hao wanao khitalifiana Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wamekhitalifiana.
Rudi kwenye sura

* 18. Tena tukakujaalia wewe, ewe Muhammad, baada ya khitilafu za Watu wa Kitabu (yaani Mayahudi na Wakristo), kuwa ni Mtume wa kwenda Njia iliyo wazi katika mambo ya Dini tuliyo kuwekea wewe na walio kuwa kabla yako miongoni mwa Mitume. Basi ifuate Sharia yako ya Haki, yenye kuthibiti imara kwa hoja na dalili, wala usifuate matamanio ya watu wasio ijua Njia ya Haki.
Rudi kwenye sura

* 19. Hakika hao waongo wenye tamaa ya kuwa ati wewe utawafuata wao, hawatoweza kukuondolea hata chembe ya adhabu pindi ukiwafuata. Na hakika wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu husaidiana wao kwa wao katika upotovu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwasaidia wale wanao mcha, basi hao haitawafikia dhulma ya wenye kudhulumu.
Rudi kwenye sura

* 20. Hii Qur'ani ulio teremshiwa wewe ni dalili kwa watu kuwaonyesha Dini ya Haki, na uwongofu wa kuwaongoza kwenye njia za kheri, na neema kwa watu wenye kuyakinisha thawabu na adhabu za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 21. Bali wanadhani hao walio chuma yanayo chusha katika ukafiri na maasi kwamba tutawafanya kama walio muamini Mwenyezi Mungu na wakatenda vitendo vyema, na hivyo tuwafanye sawa baina ya makundi mawili hayo katika uhai na katika kufa? Hukumu yao ni mbaya mno, ikiwa wanahisi kuwa wao ni sawa na Waumini.
Rudi kwenye sura

* 22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa mujibu wa hikima na nidhamu, ili zidhihiri dalili za Ungu wake na uwezo wake, na apate kulipwa kila mtu kwa alilo tenda, ikiwa kheri au shari. Na wao hawatapunguziwa chochote katika malipo yao.
Rudi kwenye sura

* 23. Ewe Mtume! Umeangalia, ukamwona huyo mwenye kufanya matamanio yake ndiye mungu wake wa kumuabudu, akamnyenyekea, na akamt'ii, na akaiacha Njia ya Haki na hali anaijua, na akaziba masikio yake asisikie waadhi, na moyo wake asiamini Haki, na akabandika vitanga vya macho asione ya kuzingatiwa? Basi nani wa kumwongoa mtu huyu baada ya kwisha puuzwa na Mwenyezi Mungu? Je! Mnaacha kutazama ili msipate kukumbuka?
Rudi kwenye sura

* 24. Na walisema wenye kukanya kufufuliwa: Hapana uhai ila huu uhai wa duniani tu tulio nao sasa. Tunaishi na tunakufa. Na hapana nyuma ya hayo uhai baada ya kwisha kufa. Na hapana cha kututeketeza isipo kuwa kupita dahari, yaani zama na wakati. Wala wao hawasemi hayo kwa ujuzi na kuwa na yakini, bali ni kwa kudhania na kukisia tu.
Rudi kwenye sura

* 25. Na ukiwasomea Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi zenye kuonyesha uwezo wake wa kufufua, huwa hawana hoja ila kusema - kwa kuikimbia haki : Wafufueni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika kudai kuwa kupo kufufuliwa.
Rudi kwenye sura

* 26. Ewe Muhammad! Waambie: Mwenyezi Mungu amekupeni uhai duniani nanyi hamkuwa chochote, kisha anakufisheni unapo timia wakati wenu. Kisha atakukusanyeni Siku ya Kiyama, na hapana shaka ya kukusanywa huko. Lakini wengi wa watu hawaujui uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa sababu ya mapuuza yao kuzingatia dalili ziliopo. Na huyo Muweza wa hayo pia ni Muweza wa kuwaleta baba zenu.
Rudi kwenye sura

* 27. Na ni wa Mwenyezi Mungu pekee ufalme wa mbingu na ardhi, kwa kuumba, kumiliki, na kupanga. Na itapo fika Saa ya Kiyama, siku hiyo watakhasiri wenye kufuata upotovu.
Rudi kwenye sura

* 28. Ewe unaye semezwa! Utawaona siku itapo fika Saa watu wa kila dini wamekalia magoti kwa khofu waliyo nayo kungojea kuitikia wito. Kila umma utaitwa kwenye daftari la vitendo vyao, na wataambiwa: Leo mtalipwa sawa malipo ya mliyo kuwa mkiyatenda duniani.
Rudi kwenye sura

* 29. Na wataambiwa: Hichi hapa kitabu chetu tulimo sajili vitendo vyenu, nanyi mmekichukua kwa mikono yenu, kinataja juu yenu yale mliyo yatenda kwa ushahidi wa kweli. Hakika Sisi tulikuwa tukiwataka Malaika waandike, ili tupate kukuhasibieni yaliyo tokana nanyi.
Rudi kwenye sura

* 30. Basi ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia katika Pepo yake. Malipo hayo ndio kufuzu kulio bainika, kulio wazi.
Rudi kwenye sura

* 31. Na ama walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake wataambiwa kwa kuwahizi: Kwani hawakukujilieni Mitume wangu? Hamkusomewa Aya zangu, nanyi mkajiona bora hamfai kuikubali haki, na mkawa kaumu ya makafiri?
Rudi kwenye sura

* 32. Enyi mnao kanya kufufuliwa! Akikwambieni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba agano la Mwenyezi Mungu la kuwalipa ni haki yenye kuthibiti, na Saa haina shaka itakuja, nyinyi mkisema: Sisi hatujui chochote khabari ya hiyo Saa ya Kiyama, wala ukweli wake; na sisi ni dhana ya kudhania tu kuwa hiyo Saa itakuja, wala hatuna yakini kuwa itatokea.
Rudi kwenye sura

* 33. Na utawadhihirikia hawa makafiri ubaya wa vitendo vyao, na itawateremkia jaza ya maskhara yao waliyo kuwa wakizifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 34. Na wataambiwa hawa washirikina kwa kuwahizi: Leo hii tunakuacheni katika adhabu kama nyinyi mlivyo acha kujitayarisha kukutana na Mola wenu Mlezi katika siku hii kwa ut'iifu na vitendo vyema. Na pahala penu pa kukaa ni Motoni, na wala hamna wa kukunusuruni akakuokoeni na adhabu yake.
Rudi kwenye sura

* 35. Adhabu hiyo imekuteremkieni kwa sababu ya ukafiri wenu, na maskhara yenu kuzifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu, na mlivyo khadaika na maisha ya dunia kwa mapambo yake. Basi leo hapana yeyote awezaye kuwatoa hawa kwenye Moto, wala hawatakikani kumtaka radhi Mola wao Mlezi kwa kutafuta udhuru.
Rudi kwenye sura

* 36. Basi ni za Mwenyezi Mungu pekee sifa njema, Muumba mbingu na ardhi, na Muumba wa viumbe vyote. Kwani hivi kuwa ni Mola Mlezi wa kila kitu unawajibika uhimidiwe kwa neema zote.
Rudi kwenye sura

* 37. Na ni wake Yeye, Subhanahu, utukufu na utawala katika mbingu na ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, asiye shindika, Mwenye hikima, asiye kosea katika hikima yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani