Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul H'ashri

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio laiki naye. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi na kitu. Mwenye hikima katika mipango yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye sura

* 2. Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nnadhir, kutoka kwenye majumba yao wakati wa kuwatoa mara ya kwanza katika Bara Arabu. Enyi Waislamu! Hamkudhania kuwa watatoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na wao wenyewe walidhani kwamba ngome zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea katika upande wasio utarajia, na akawatia katika nyoyo zao fazaa kubwa, wakawa wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya Waumini wapate kuzivunja zile ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika haya yaliyo washukia hawa.
Rudi kwenye sura

* 3. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwahukumia kuwatoa majumbani kwao kwa sura hii ya kuchusha, basi hapana shaka angeli waadhibu katika dunia kwa shida zaidi kuliko huko kuwatoa. Na Akhera, wao watapata adhabu ya Moto, mbali huku kutolewa majumbani kwao duniani.
Rudi kwenye sura

* 4. Hayo yaliyo wapata duniani na yanayo wangojea Akhera ni kwa sabau ya kuwa wamemfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake, uadui mkubwa mno. Na mwenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu basi hawezi kupenya kuikimbia adhabu yake. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Rudi kwenye sura

* 5. Enyi Waislamu! Mitende yoyote mliyo ikata au mkaiacha imebaki kama ilivyo kuwa, basi ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hapana lawama juu yenu katika hayo, ili awape nguvu Waumini, na awahizi wapotovu walio ziacha sharia zake.
Rudi kwenye sura

* 6. Na aliyo yaleta Mwenyezi Mungu na akayarudisha kwa Mtume wake katika mali ya Banu Nnadhir hamkuyapigia mbio nyinyi kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa madaraka Mitume wake kwa awatakao katika waja wake bila ya kupigana vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mtimilivu wa uweza juu ya kila kitu.
Rudi kwenye sura

* 7. Alicho rudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake katika mali ya watu wa vijiji hivi bila ya kuwatimua farasi au ngamia, vitu hivyo ni vya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri. Haya ni hivyo ili yasiwe mali yakizunguka katika mikono ya matajiri peke yao katika nyinyi. Na anacho kupeni Mtume katika hukumu basi kishikeni, na anacho kukatazeni basi kiwacheni. Na jilindeni na kughadhibika kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Rudi kwenye sura

* 8. Na hivyo yale mali ya watu wa vijiji aliyo yarudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake wapewe mafakiri katika Wahajiri, walio kimbilia Madina, ambao wametolewa majumbani kwao na mali yao huko Makka. Wao wanataraji ziada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika riziki zao na radhi. Na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa nafsi zao na mali yao. Hao ndio Waumini wa kweli.
Rudi kwenye sura

* 9. Na Ma-ansari, watu wa Madina walio mnusuru Mtume na Wahajiri, ambao wamekaa Madina katika maskani zao, na Imani yao ikawa safi kabisa kabla ya kufika Wahajiri, wanawapenda wale wageni Waislamu walio hamia kwao, na wala hawahisi ubaya wowote katika nafsi zao kwa walicho pewa Wahajiri katika ngawira. Bali wanawakadimisha Wahajiri kuliko nafsi zao, ijapo kuwa wakiwa wao nao ni wahitaji. Na mwenye kuhifadhika, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, asione ubakhili katika nafsi yake, basi watu kama hao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
Rudi kwenye sura

* 10. Na Waumini walio kuja baada ya Wahajiri na Ansari husema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu, sisi na ndugu zetu walio tutangulia katika Imani. Wala usijaalie kuwa katika nyoyo zetu husda kuwahusudu walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe umefika ukomo katika upole na kurehemu.
Rudi kwenye sura

* 11. Hebu huwaangalii hao wanaafiki ukastaajabu? Kazi yao ni kuwakariria kauli ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu - nao ni hao Banu Nnadhir - kuwaambia: Wallahi! Mkilazimishwa kuihama Madina, basi hapana shaka na sisi tutatoka pamoja nanyi. Wala hatutamt'ii katika jambo lenu mtu yeyote daima dawamu. Na pindi ikiwa Waislamu watakupigeni vita, basi hapana shaka sisi tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hakika wanaafiki hapana shaka ni waongo katika hizo ahadi zao wanazo zitoa.
Rudi kwenye sura

* 12. Wakitolewa Mayahudi, wanaafiki hawatatoka pamoja nao. Na wakipigwa vita hawatawanusuru. Na pindi wakiwasaidia basi hapana shaka watatoka mbio warudi kinyume nyume, wala hawatawanusuru.
Rudi kwenye sura

* 13. Hakika, enyi Waislamu, mna kitisho zaidi katika vifua vya wanaafiki na Mayahudi kuliko wanavyo mwogopa Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa sababu hakika wao ni watu wasio jua ukweli wa Imani.
Rudi kwenye sura

* 14. Mayahudi hawapigani vita nanyi kwa pamoja ila wawe katika miji iliyo jengewa ngome, au wajifiche nyuma ya kuta. Vita vyao baina ya wao kwa wao ni vikali. Utawadhani kuwa wameshikamana, wote ni wamoja. Kumbe hakika nyoyo zao zimefarikiana mbali mbali. Wao ni wenye sifa hizo, kwa sababu hao ni watu wasio zingatia nini utakuwa mwisho wa mambo.
Rudi kwenye sura

* 15. Mfano wa Bani Nnadhir ni kama mfano wa walio kufuru kabla yao karibuni. Hao walionja hapa hapa duniani matokeo ya ukafiri wao na kuvunja kwao mapatano. Na Akhera watapata adhabu ya uchungu mkali.
Rudi kwenye sura

* 16. Mfano wa wanaafiki kuwashawishi Banu Nnadhir wamuasi Mtume wa Mwenyezi ni kama mfano wa Shetani pale anapo mghuri mtu aiache Imani, akamwambia: Kufuru! Na alipo kufuru akasema: Mimi niko mbali nawe, kwani mimi ninamkhofu Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Rudi kwenye sura

* 17. Ikawa basi marejeo ya Shetani na huyo anaye mzaini ni kuishia Motoni wabaki humo milele. Na kudumu humo dawamu ni malipo ya wenye kuasi wakaikiuka Njia ya Haki.
Rudi kwenye sura

* 18. Enyi mlio amini! Jiwekeeni kinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kumt'ii Yeye. Na kila nafsi izingatie a'mali gani ya kuikadimisha kwa ajili ya Kesho. Na jilazimisheni kumcha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari vilivyo kwa yote myatendayo. Naye atakulipeni kwa hayo.
Rudi kwenye sura

* 19. Enyi Waumini! Msiwe kama wale walio sahau haki za Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao, kwa kuwajaribu kwa mitihani, na wakawa hawajui linalo wafaa na linalo wadhuru. Hao ndio walio toka wakaacha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 20. Hawawi sawa watu wa Motoni wanao teswa, na watu wa Peponi wanao neemeshwa. Watu wa Peponi peke yao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
Rudi kwenye sura

* 21. Lau tungeli iteremsha hii Qur'ani juu ya mlima wenye nguvu basi ungeli uona huo mlima, juu ya nguvu zake, unanyenyekea na unapasuka kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu. Na hiyo ni mifano tunawaelezea watu ili wapate kuzingatia matokeo ya mambo yao.
Rudi kwenye sura

* 22. Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana wa kuabudiwa kikweli isipo kuwa Yeye peke yake, Mwenye kujua lilio pita na lilioko sasa. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Rudi kwenye sura

* 23. Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye, Mwenye kumiliki kila kitu kwa hakika, Aliye safika na kila upungufu, Aliye takasika na kila lisio mwelekea, Mwenye kusalimika na yote ya upungufu, Mwenye kuwaamini na kuwasadiki Mitume wake aliyo wapa nguvu kwa miujiza, Mlinzi Mwenye kuangalia kila kitu, Mwenye kushinda basi hashindwi na chochote, Mkubwa wa shani katika nguvu na utawala, Mwenye kutukuka na kila kisicho kuwa laiki na uzuri wake na utukufu wake, Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo.
Rudi kwenye sura

* 24. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye kuviumba vitu vyote tangu mwanzo bila ya ruwaza ya kuigia iliyo tangulia, Mwenye kuvipa sura kama vilivyo kwa mujibu wa atakavyo Yeye. Yeye ndiye Mwenye Majina Mazuri, Mwenye kutakaswa na kila kisicho kuwa laiki yake na kila kilichoko katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda, asiye shindwa na kitu. Mwenye hikima katika kupanga kwake na sharia zake.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani