Al Qasas
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Qasas

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. T'a Sin Mim, harufi za kutamkwa kubainisha kuwa Qur'ani hii ni muujiza wa harufi hizi hizi za mazungumzo yenu, na ili kuwazindua wenye kusikia.
Rudi kwenye sura

* 2. Ewe Mtume! Aya hizi tunazo kufunulia wewe ni Aya za Qur'ani yenye kubainisha kwa uwazi, yenye kudhihirisha Haki iwe mbali na uwongo, na halali iwe mbali na haramu, na itoe ahadi ya kulipwa thawabu, na kuhadharisha na adhabu.
Rudi kwenye sura

* 3. Tunakusimulia baadhi ya khabari za Musa na Firauni kwa ukweli, ili wapate kuzizingatia Waumini.
Rudi kwenye sura

* 4. Hakika Firauni alipandwa na kiburi, na akapita mipaka katika udhalimu wake, na akatakabari mno katika nchi ya Misri. Akawafanya watu wa nchi hiyo makundi makundi, akiwanyanyua baadhi yao na akiwadhalilisha wenginewe, na khasa aliwadhoofisha Wana wa Israili. Akawa anawachinja watoto wao wanaume na akiwabakisha wanawake. Kwa hakika huyo alikuwa ni katika walio pita hadi katika ujabari na ufisadi.
Rudi kwenye sura

* 5. Na Mwenyezi Mungu akataka kuwafadhilisha alio wafanya wanyonge Firauni katika nchi, na awafanye ndio wa kuongoza katika njia za kheri, na awarithishe ufalme na madaraka ya nchi.
Rudi kwenye sura

* 6. Na tuwathibitishe katika nchi, na wawe na pahali pao humo. Na tuwathibitishie Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyo kuwa wakiyakhofu, nayo ni kuondoka ufalme wake kwa mkono wa mwenye kuzaliwa katika Wana wa Israili.
Rudi kwenye sura

* 7. Na Mwenyezi Mungu alimfahamisha mama yake Musa, alipo kuwa anamkhofia asichinjwe na Firauni kama alivyo kuwa akiwachinja watoto wanaume wa Bani Israili, kwamba amnyonyeshe kwa kituo na hatauliwa na Firauni. Ikiwa anaogopa asije kutambulikana amtie katika sanduku, na amtie katika mto wa Nile bila ya khofu wala huzuni. Kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu amedhamini kumhifadhi na kumrejeshea mwenyewe, na kumtuma kwa Wana wa Israili.
Rudi kwenye sura

* 8. Watu wa Firauni wakamchukua, ili aliyo kadiria Mwenyezi Mungu yatimie, yaani Musa apate kuwa Mtume mwenye kuwapinga wao, na mwenye kuwaletea huzuni, kwa kuitoa kombo dini yao na kuishambulia dhulma yao. Hakika Firauni na Hamana na wasaidizi wao walikuwa ni watu wenye madhambi, walio pindukia mipaka katika ujeuri na uharibifu.
Rudi kwenye sura

* 9. Mke wa Firauni alipo mwona mtoto alimwambia mumewe: Mtoto huyu atatuletea furaha mimi na wewe. Tumweke, tusimuuwe, kwa kutaraji kuwa atakuja tufaa kuendesha mambo yetu. Au tumfanye mwenetu wa kumlea. Na wao kumbe hawatambui aliyo mkadiria Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 10. Na mama yake Musa akawa hajitambui kwa dhiki iliyo muingia kwa kuwa mwanawe kaangukia mikononi mwa Firauni. Akawa anakurubia kujitambulisha kwamba yeye ndiye mama yake. Lau ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakuutia imara moyo wake kwa kusubiri, basi angeli tangaza kuwa huyo ni mwanawe, jinsi alivyo kuwa akimhurumia, na pia ili awe miongoni mwa Waumini wenye kutulia.
Rudi kwenye sura

* 11. Yule mama akamwambia dada yake Musa: Mfuatie upate kujua khabari zake. Basi akawa anamwona kwa mbali na anatahadhari asitambulikane, na Firauni na watu wake wakawa hawajui kama yule ni dada yake.
Rudi kwenye sura

* 12. Mwenyezi Mungu alimjaalia yule mtoto akatae ziwa la kila mnyonyeshaji kabla hawajamjia mama yake. Watu wa Firauni wakaingiwa na ghamu, na wakashughulishwa na hayo. Yule dada yake ndio akawaambia: Nikuongozeni kwenye ukoo utakao muangalia huyu mtoto, na kumnyonyesha, na kumlea, nao watamtazama vizuri?
Rudi kwenye sura

* 13. Wakaukubali uwongozi wake, na Mwenyezi Mungu akamrudisha kwa mama yake, ili nafsi yake itue, na afurahi kwa kurudi kwake, wala asihuzunike kwa kuwa mbali naye, na ili azidi kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo mpa kuwa atamrudishia imetimia wala hayendi kinyume. Lakini watu wengi walikuwa hawajui kurudi Musa kwa mama yake, kwani hayo yote yalifichikana kwao.
Rudi kwenye sura

* 14. Na Musa alipo kwisha kuwa mtu mzima, na akakamilika, Mwenyezi Mungu alimpa hikima na ilimu. Na hisani kama hii tuliyo mpa Musa na mama yake, tunawapa wema wote kwa ajili ya wema wao.
Rudi kwenye sura

* 15. Musa akaingia mjini Misri wakati walipo kuwa watu wake wameghafilika. Akawakuta watu wawili wanapigana. Mmoja ni katika Wana wa Israili, na mwengine katika kaumu ya Firauni. Yule Muisraili akamtaka msaada kumpiga khasimu yake. Naye Musa akamsaidia. Akampiga konde yule khasimu, akamuuwa bila ya kukusudia. Musa akajuta na akasema: Hakika mimi kuja kufanya kitendo hichi ni kazi ya Shetani. Hakika Shetani ni adui aliye wazi kwa uadui na kupoteza.
Rudi kwenye sura

* 16. Musa akasema kwa kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na majuto: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa niliyo yatenda. Basi nighufirie kitendo changu hichi. Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake na akamsamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa kusamehe, Mkunjufu wa rehema.
Rudi kwenye sura

* 17. Musa akasema kwa kunyenyekea: Ewe Mola wangu Mlezi! Kwa haki ya kunineemesha kwako kwa kunipa hikima, na ilimu, niwezeshe nitende kheri na yanayo faa. Ukiniwezesha hivyo basi kabisa sitakuwa msaidizi wa makafiri.
Rudi kwenye sura

* 18. Kulipo pambazuka asubuhi Musa alikuwapo mjini, Misri, naye yumo katika khofu, akitaraji kufikiwa na madhara kutokana na watu kwa sababu vile alivyo muuwa Mmisri. Akamwona yule Muisraili aliye mtaka msaada jana, naye akamtaka msaada mara ya pili katika ugomvi na Mmisri mwengine. Musa akamkemea kwa kumwambia: Hakika wewe mtu matata mno, na dhaahiri wewe ni mpotovu. Unafanya yale yale uliyo yafanya jana, na unaniita tena nikusaidie!
Rudi kwenye sura

* 19. Na Musa alipo taka kumtumilia nguvu Mmisri, ambaye ni adui wao wote wawili; kwa sababu ya uadui huu, yule mtu alidhani kuwa Musa atamuuwa, basi akasema: Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa muasi tu katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni wanao lingania maslaha na kheri.
Rudi kwenye sura

* 20. Akaja mtu mmoja Muumini katika kaumu ya Firauni kutoka mwisho wa mji, ilipo enea khabari ya Musa kumuuwa Mmisri. Yule mtu akamwambia Musa kwamba watu wanapanga kutaka kumuuwa. Akamwambia: Toka mji, ukimbie usije ukauliwa! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha.
Rudi kwenye sura

* 21. Musa akautoka mji naye amejaa khofu wasije maadui wakamdhuru, akimnyenyekea Mwenyezi Mungu amwokoe na udhalimu wa makafiri.
Rudi kwenye sura

* 22. Alipo elekea Madyana, kijiji cha Shuaibu - kwa kuwa huko iko amani - alimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu amwongoe njia ya kheri na ya kuokoka.
Rudi kwenye sura

* 23. Alipo yafikia maji ya Madyana wanapo nyweshea maji alikuta karibu na kisima kundi la watu wengi mbali mbali wanawanywesha wanyama wao wa mifugo. Na pahali pa chini kuliko hapo pao akawakuta wanawake wawili wanawazuia kunywa maji kondoo na mbuzi wao. Musa akawaambia: Mbona mko mbali na maji? Wakajibu: Hatuwezi kusukumana, na wala hatunyweshi sisi mpaka hawa wachunga wamalize wao kunywesha. Na baba yetu ni mkongwe, hawezi kuchunga wala kunywesha wanyama.
Rudi kwenye sura

* 24. Musa akajitolea kuwakhudumia akawanyweshea. Kisha akenda kuegemea mti akipumzika baada ya kuhangaika kule, naye akisema kwa unyenyekevu: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mwenye haja ya kheri yoyote na riziki yoyote utayo niletea.
Rudi kwenye sura

* 25. Mmmoja wa wale mabinti akaja na ujumbe kutoka kwa baba yake baada ya kwisha jua khabari za Musa na wao wale mabinti. Naye akaja na huku anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita ili akulipe ujira kwa ulivyo tunyweshea maji. Basi alipo kwenda kwake na akamsimulia kisa chake cha kutoka Misri, akasema yule mzazi wa mabinti: Usikhofu; umekwisha okoka kwa hao watu madhaalimu. Kwani Firauni hana madaraka juu yetu.
Rudi kwenye sura

* 26. Mmoja wa wale mabinti alisema: Ewe baba yangu! Mchukue umpe kazi ya kuchunga kondoo na mbuzi na kuwasimamia kwa haja zao. Hakika huyu ni mbora wa kumuajiri kwa sababu ya nguvu zake na uaminifu wake.
Rudi kwenye sura

* 27. Shuaibu a.s. akamwambia: Mimi nataka kukuoza mmoja wa hawa mabinti zangu kwa mahari ya kunifanyia kazi muda wa miaka minane. Ukitimiza kumi itakuwa ni khiari yako. Wala mimi sitaki kukulazimisha huo muda mrefu. Na Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mimi ni katika watu wema, wenye kwenda nawe kwa ihsani na kutimiza ahadi.
Rudi kwenye sura

* 28. Musa akasema: Hayo uliyo niahidi ni sawa sawa baina yangu na wewe. Muda wowote katika huo nitakao kufanyia kazi itakuwa nimekutimizia ahadi yako. Wala mimi sitaki zaidi kuliko hayo. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi kwa tunayo yasema.
Rudi kwenye sura

* 29. Musa alipo timiza muda wake walio patana, na akawa mume wa binti wa yule aliye mpokea, na akawa anarudi Misri, aliona njiani mwake katika upande wa Mlima wa T'uri moto unawaka. Akawaambia walio kuwa pamoja naye: Kaeni hapa. Mimi nimeuona moto, nimefurahi nao katika giza hili. Nitawendea nikuleteeni khabari ya njia, au nipate kijinga cha moto mpate walau moto wa kuota kujilinda na baridi.
Rudi kwenye sura

* 30. Musa alipo ufikia moto alio uona alisikia kutoka upande wa kulia kwenye mti wenye kumea katika eneo lilio barikiwa ubavuni mwa Mlima, wito wa juu ukisema: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana anaye stahiki kuabudiwa isipo kuwa Yeye, Mwenye kuumba viumbe vyote na ni Mwenye kuvilinda na kuvihifadhi na kuvilea.
Rudi kwenye sura

* 31. Na akanadiwa: Tupa chini fimbo yako. Akaitupa chini. Mwenyezi Mungu akaigeuza ikawa nyoka. Musa alipo iona inakwenda kama nyoka alikhofu, na akakimbia kwa kufazaika. Akaambiwa: Ewe Musa! Njoo, unaitwa urejee pahala pako, wala usiogope. Kwani wewe ni katika walio hifadhiwa na kila cha kuchukiza.
Rudi kwenye sura

* 32. Na uingize mkono wako kwenye uwazi wa nguo yako utatoka mweupe, bila ya ila wala maradhi. Na jiambatishe mkono wako ubavuni mwako katika nguo ukiwa una khofu. Wala usishituke kwa kuona fimbo imekuwa nyoka, na kuona mkono wako umekuwa mweupe. Kwani miujiza hii miwili inatokana na Mwenyezi Mungu ya kumkabili nayo Firauni na kaumu yake watapo ukabili Ujumbe wako kwa kuukadhibisha na hali wametoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 33. Musa akasema, kwa khofu na kuomba msaada: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimemuuwa mtu katika hao, na nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi.
Rudi kwenye sura

* 34. Na ndugu yangu, Harun, ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi. Basi mtume awe pamoja nami katika kufikisha Utume, kwani mimi nina khofu watanikanusha.
Rudi kwenye sura

* 35. Mwenyezi Mungu akasema, kuitikia ombi lake: Tutakutia nguvu kwa kumtuma Harun. Na tutakupeni nyinyi wawili madaraka, na tutakuungeni mkono kwa miujiza. Kwa hivyo hawatoweza kukuvamieni. Na nyinyi wawili na walio kufuateni na wakaongoka kwa msaada wenu, mtakuwa wenye kuwashinda hawa makafiri.
Rudi kwenye sura

* 36. Musa alipo wakabili kwa wito wake ulio tiliwa nguvu na miujiza iliyo wazi, waliyakanusha waliyo yaona, na wakasema: Haya si chochote ila ni uchawi unao mzulia Mwenyezi Mungu. Na hatukupata kusikia haya unayo tuitia kwa baba zetu wa zamani walio tangulia.
Rudi kwenye sura

* 37. Na Musa alisema kumjibu Firauni na kaumu yake: Mola wangu Mlezi anajua kwa hakika kuwa mimi nimeleta Ishara hizi zenye kuonyesha Haki na Uwongofu kutokana naye Yeye. Basi Yeye ndiye shahidi wangu kwa haya, ikiwa nyinyi mnanikadhibisha. Na Yeye anajua kuwa mwisho mwema ni wetu sisi watu wa Haki. Hakika makafiri hawapati kheri.
Rudi kwenye sura

* 38. Na Firauni alipo shindwa kuhojiana na Musa, na akaendelea na jeuri zake, alisema: Enyi wahishimiwa! Mimi sijui kama yupo mungu wenu mwenginewe isipo kuwa mimi. Na akamuamrisha waziri wake Haman amchomee matufali, na amjengee mnara mrefu apande, ende kumtazama huyo mungu anaye mlingania Musa.
Rudi kwenye sura

* 39. Firauni na majeshi yake wakaendelea wakifanya kiburi katika nchi ya Misri kwa upotovu. Na wakadhani kuwa kabisa hawato fufuliwa Akhera kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye sura

* 40. Tukamng'oa Firauni kwenye utawala wake, na tukawavutia taratibu yeye na majeshi yake mpaka baharini, na tukawazamisha na huku tunawatupia sababu ya dhulma yao. Basi zingatia, ewe Muhammad, na uwahadharishe watu wako watazame vipi unakuwa mwisho wa wenye kudhulumu katika dunia yao. Na hakika wewe ni mwenye kusaidiwa kupata ushindi juu yao.
Rudi kwenye sura

* 41. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Na tukawafanya hao ni wenye kuitia watu kwenye ukafiri, ambao khatima yake ni Moto. Na Siku ya Kiyama hawampati wa kuwanusuru na kuwatoa kwenye adhabu.
Rudi kwenye sura

* 42. Na tukawafanya katika dunia hii wenye kupata laana, yaani wenye kutolewa wasiipate rehema yetu; na Siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa walio angamizwa. Na yaliyo simuliwa katika Aya mbili hizi juu yao ni dalili ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 43. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu alimteremshia Musa Taurati, baada ya kuwahiliki wakanushao katika kaumu zilizo tangulia, ili iwe nuru ya nyoyo. Kwani nyoyo hizo zilikuwa gizani, haziijui Haki wala uwongozi mwema. Kwani hao walikuwa wakitangatanga tu katika upotovu, na hawaijui njia ya kupatia rehema kwa mwenye kutenda kwa ajili yake, na wakawaidhika kwa yaliyomo katika hiyo Taurati, na wakakimbilia kuzifuata amri, na kuyaacha yaliyo katazwa.
Rudi kwenye sura

* 44. Wala wewe Muhammad, hukuwa na Musa upande wa magharibi wa huo mlima, pale Mwenyezi Mungu alipo agana naye kumuamrisha Ujumbe. Wala hukuishi zama za Musa, wala hukushuhudia alipo fikisha Utume. Basi vipi hawa watu wako wanakanusha Utume wako na wewe unawasomea khabari za walio tangulia?
Rudi kwenye sura

* 45. Na lakini Sisi tumeziumba kaumu nyingi katika vizazi vilivyo pitiwa na zama ndefu, hata wakasahau maagano yaliyo chukuliwa kwao. Na wewe, ewe Mtume, hukuwa mkaazi wa Madyana hata ndio uwasimulie watu wa Makka khabari zao. Lakini Sisi tumekutuma wewe, na tumekupa khabari zao kwa njia ya wahyi (Ufunuo).
Rudi kwenye sura

* 46. Wala wewe, ewe Mtume, hukuwepo hapo kando ya mlima pale Mwenyezi Mungu alipo mwita Musa na akamteuwa kumpa Utume wake. Lakini Mwenyezi Mungu amekujuvya haya kwa njia ya wahyi (ufunuo), kutokana na rehema yake kwako na kwa umma wako, wapate kufikisha hayo kwa kaumu ambayo haikupata kufikiwa na Mtume kabla yako wewe, ili wakumbuke.
Rudi kwenye sura

* 47. Ingeli kuwa makafiri wanapo patwa na mateso kwa sababu ya ukafiri wao wakataka udhuru na wakadai wakisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Mbona hukutuletea Mtume tukamuamini na tukaikubali miujiza yake nasi tukawa miongoni mwa Waumini, basi usinge kuwepo Ujumbe wa Mitume.
Rudi kwenye sura

* 48. Na alipo ileta Mtume wa Mwenyezi Mungu Qur'ani kutokana na Mwenyezi Mungu, makafiri walisema: Laiti yeye angeli pewa miujiza ya kuonekana na kama aliyo pewa Musa, na Kitabu cha kuteremka mara moja kama Taurati! Na hali hao walimkataa Musa na Ishara zake, kama hivi leo wanavyo mkataa Muhammad na Kitabu chake, na wakasema: Sisi tunawakataa wote wawili. Basi kukataa ndiko kuliko pelekea kuikanya miujiza.
Rudi kwenye sura

* 49. Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa hamuiamini Taurati na Qur'ani basi leteni kitabu kingine kinacho toka kwa Mwenyezi Mungu kilicho na uwongofu bora kuliko hivyo, au kama hivyo, nami nikifuate pamoja nanyi, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika hayo madai yenu kwamba tuliyo kuja nayo ni uchawi.
Rudi kwenye sura

* 50. Na ikiwa hawaitikii wito wako kwa kuleta kitabu kiongofu zaidi, basi jua kuwa wamebanwa na hawakubakiliwa na hoja yoyote, na kwamba kwa hayo wanafuata pumbao zao tu. Na hapana aliye zidi kwa upotovu kuliko yule anaye fuata pumbao lake katika dini, bila ya uwongofu kutokana na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hamwafiki mwenye kuidhulumu nafsi yake kwa kufuata upotovu bila ya kuitafuta Haki.
Rudi kwenye sura

* 51. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu amewateremshia Qur'ani kwa utungo, baadhi yake ikifuatia baadhi kwa mujibu wa inavyo takikana na hikima, na kulingana na ahadi, na maonyo, na hadithi, na mazingatio, ili wapate kupima na kuyaamini yaliomo ndani yake.
Rudi kwenye sura

* 52. Wale ambao tuliwateremshia Taurati na Injili kabla ya kuteremka Qur'ani, na wakaviamini vitabu hivyo viwili, na wakasadiki yaliyo tajwa humo juu ya khabari za Muhammad na Kitabu chake, hao wanamuamini Muhammad na Kitabu chake.
Rudi kwenye sura

* 53. Na hao wakisomewa Qur'ani hufanya haraka kutangaza Imani yao, na husema: Tumeyaamini hayo, kwani hayo ni Haki inayo toka kwa Mola wetu Mlezi; na sisi tulimjua Muhammad na Kitabu chake hata kabla ya kuteremka kwake, nasi tukanyenyekea kabla ya kusomwa kwake.
Rudi kwenye sura

* 54. Hao ambao waliiamini Qur'ani na yaliyo teremshwa kabla yake, watapewa malipo yao maradufu - kwa ajili ya kuvumilia kwao mateso yaliyo wapata kwa ajili ya Imani, na wakakhiari vitendo vyema, na wakayakabili maovu kwa kusamehe na ihsani, na wakatoa katika njia ya kheri kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 55. Na wanapo sikia upotovu wa wajinga hujitenga mbali nao, kwa kujiepusha na kuondoka, na husema: Sisi tuna a'mali yetu na hatuiachi, na nyinyi mna a'mali yenu ya upotovu na madhambi yake yapo juu yenu. Na sisi tunakuacheni na mambo yenu, kwani sisi hatupendi kusuhubiana na majaahili.
Rudi kwenye sura

* 56. Ewe Mtume! Hakika wewe una pupa sana kutaka hawa watu wako waongoke. Lakini wewe huwezi kumuingiza katika Uislamu kila umpendaye. Lakini Mwenyezi Mungu humwongoa kuendea Imani yule anaye mjua kuwa ameelekea uwongofu na ameukhiari. Na Yeye ndiye Mwenye kujua, wala hapana ajuaye zaidi kuliko Yeye, nani atakaye ingia katika safu za wenye kuongoka.
Rudi kwenye sura

* 57. Na washirikina wa Makka walimwambia Mtume s.a.w. kwa kujitolea udhuru kwa kubakia kwao katika dini yao: Tukikufuata wewe katika dini yako Waarabu watatutoa katika nchi yetu, na watatushinda katika utawala wetu. Na hakika wao ni waongo katika kutoa udhuru wao huo. Kwani Mwenyezi Mungu alikuwa kawaweka imara na madhubuti katika nchi yao. Na akaifanya nchi takatifu yenye amani, hawashambuliwi wala hawauwawi, na hali wao ni makafiri. Na wanaletewa matunda na kheri nyengine za aina nyingi, ambazo Mwenyezi Mungu anawaletea kutoka kila upande. Basi huwaje awaondolee amani, na awaachilie wakinyakuliwa wakiongeza juu ya utakatifu wa Nyumba ya Alkaaba Imani kumuamini Muhammmad! Lakini wengi wao hawaijui Haki. Lau kuwa wanaijua wasinge khofu kunyakuliwa.
Rudi kwenye sura

* 58. Watu hawa hawazingatii yaliyo wapata kaumu zilizo kwisha tangulia. Iliangamizwa miji ya walio ghurika na neema za Mwenyezi Mungu, na kisha wakazikanusha na wakamkanusha Mwenyezi Mungu. Na haya majumba yao yamekuwa matupu, magofu, hayafai kukaliwa ila nadra tu kwa wapita njia. Na yamebaki hayana mwenye kuyamiliki baada yao ila Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na ukarimu.
Rudi kwenye sura

* 59. Na haikuwa katika hikima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - naye ndiye Mola wako Mlezi aliye kuumba na kukuteuwa - kuiangamiza miji mikubwa ila baada ya kuwapelekea watu wake Mtume mwenye miujiza iliyo wazi awasomee Kitabu kilicho teremshwa, na awabainishie sharia, na kisha wawe hawaamini. Wala Sisi hatuangamizi miji mikubwa ila wakiwa watu wake wanaendelea na udhalimu na uadui.
Rudi kwenye sura

* 60. Na kila kitu mlicho ruzukiwa katika starehe za dunia na mapambo yake kina ukomo wake kwa muda mfupi. Hayo yasikuzuieni kuamini na kutenda vitendo vyema. Kwani hakika yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu huko Akhera, nayo ni thawabu na neema za milele, yana nafuu zaidi, na yana dawamu kuliko hayo yote. Basi kwa nini hamtumii akili zenu badala ya pumbao zenu?
Rudi kwenye sura

* 61. Hawi sawa mwenye kuamini na akatenda mema na akastahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya malipo mema na Pepo, na akayapata kama alivyo muahidi Mwenyezi Mungu; kulingana huyu na yule aliye kanusha na akatenda vitendo viovu, na yakamzuga maisha ya dunia na mapambo yake, na kisha Siku ya Kiyama akawa katika walio hudhurishwa kwa ajili ya hisabu, na akawa katika wenye kuhiliki kwa adhabu.
Rudi kwenye sura

* 62. Ewe Mtume! Kumbuka siku watapo simama hawa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuhisabiwa, naye Subhanahu akawaita kwa kuwatahayarisha: Wako wapi hao miungu mlio dai kuwa ni washirika wangu, wapate kukuteteeni na kukuombeeni?
Rudi kwenye sura

* 63. Watasema waongozi wa makafiri katika walio stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na vitisho vyake: Ewe Mola wetu Mlezi! Hawa tulio waita kwenye shirki na tukawapambia upotovu tuliwapoteza. Kwa sababu wao walikhiari ukafiri na wakaupokea, kama sisi tulivyo ukhiari na tukaupokea. Leo sisi tunajitenga nao kwako na ukafiri walio ukhiari duniani. Hawakuwa wao wakituabudu sisi; bali wakiabudu pumbao zao, na wakit'ii matamanio yao.
Rudi kwenye sura

* 64. Na Mwenyezi Mungu kuwaamrisha makafiri ni kwa kuwatahayarisha tu, kwa vile kuwataka wawaite wale miungu ya ushirikina wawaokoe na adhabu yake, kama walivyo dai. Wakaitikia kwa unyonge, na wakawaita kwa kuwa hawana hila. Wasipate jawabu yoyote. Wakaiona adhabu walio ahidiwa iko mbele yao, na wakatamani lau kuwa katika dunia yao wangeli kuwa Waumini walio ongoka, jinsi ya adhabu iliyo wafikia.
Rudi kwenye sura

* 65. Na ewe Mtume! Taja vile vile siku washirikina watapo itwa na Mwenyezi Mungu kwa kutahayarishwa, na wakaambiwa: Mliwajibu nini Mitume wangu nilio watuma kwenu wakuiteni kwenye Imani, nao wakafikisha Ujumbe?
Rudi kwenye sura

* 66. Khabari hizo zikawapita hawazitambui kama kwamba ni vipofu. Ikawa hapana amuulizae mwenziwe, kwani wote walikuwa sawa sawa wameshindwa kujibu.
Rudi kwenye sura

* 67. Hii ndiyo hali ya washirikina. Ama mwenye kutubu kutokana na shirki yake, na akaamini Imani ya kweli, na akatenda mema, basi huyo hutaraji kuwa kwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa walio fuzu kuipata radhi ya Mwenyezi Mungu, na neema ya kudumu yenye kuendelea milele.
Rudi kwenye sura

* 68. Na Mola wako Mlezi anaumba atakalo kwa uwezo wake. Na anamkhitari amtakaye kwa hikima yake kumpa Ujumbe na ut'iifu kwa kujua kwake mwenyewe kufaa kwao. Wala hawawezi viumbe, na wala si haki, kumchagulia Mwenyezi Mungu walitakalo katika dini potovu, na miungu ya uwongo. Mtukufu ametakasika shani yake na washirika.
Rudi kwenye sura

* 69. Ewe Mtume! Mola wako Mlezi anajua baraabara yaliomo katika vifua vya washirikina ya uadui wao juu yako, na wanayo tangaza kwa ndimi zao ya kukushutumu na kukupinga kwa ulivyo teuliwa kupewa Utume.
Rudi kwenye sura

* 70. Na Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ndiye Mwenyezi Mungu wa Haki, ndiye pekee Mwenye Ungu, Mwenye kustahiki peke yake kuhimidiwa na waja wake katika dunia kwa neema zake na uwongofu wake, na katika Akhera kwa uadilifu wake na kulipa kwake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye hukumu, na kuamua baina ya waja wake. Na kwake Yeye ndiyo marejeo ya kwendea.
Rudi kwenye sura

* 71. Ewe Mtume! Sema: Enyi watu! Niambieni, Mwenyezi Mungu akikufanyieni usiku uendelee mfululizo bila ya mchana mpaka Siku ya Kiyama, je! Mnaye yeyote asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni mchana wenye mwangaza mkaweza kushughulikia maisha yenu na kuendesha mambo yenu ya dunia? Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamsikii kwa sikio la kuwaza na kuzingatia?
Rudi kwenye sura

* 72. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu akikujaalieni mchana mfululizo bila ya usiku mpaka Siku ya Kiyama, yupo asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni usiku mkapata kupumzika na kazi za mchana? Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamzioni Ishara za Mwenyezi Mungu, mkaamini na mkaongoka?
Rudi kwenye sura

* 73. Na miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake ni kuwa kawaumbia usiku na mchana, inayo fuatana, ili wapate kupumzika usiku, na washughulikie kutafuta riziki zao na manufaa yao mengine wakati wa mchana, na watambue fadhila za Mwenyezi Mungu juu yao wapate kumshukuru. "Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni? Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru." Hapana shaka kuwa kuumbwa kwa dunia kwa namna yake ilivyo sasa na ilivyo wekwa kwa mnasaba wa jua, na kuzunguka kwake wenyewe kwa wenyewe kila siku, na kulizunguka jua kila mwaka, hapana shaka kwamba haya yanaonyesha dhaahiri uwezo wa Mwenyezi Mungu na upweke wake. Na Aya tukufu inawazindua watu watambue ukweli ambao yawapasa wauelewe, nao ni kwamba Yeye Mtukufu lau kuwa aliumba dunia iwe na usiku wa milele, au iwe na mchana wa milele, basi hapanapo mungu mwengine anaye weza kuwaneemesha watu kwa mchana na usiku wa kufuatana kama hivi. Na hivyo ni kuwa lau kuwa dunia inazunguka juu ya msumari-kati wake na pia kulizunguka jua kwa kiwango kimoja kiasi ya siku 365 takriban, yangeli tokea mabadiliko makubwa mno. Miongoni mwao ni kudumu giza katika nusu ya dunia, na kudumu mwangaza katika nusu ya pili takriban. Na kwa hivi joto lingeli panda katika nusu yenye mwangaza kwa kiasi kisicho weza kuchukulika. Na nusu yenye giza ingeganda kwa barafu. Na pande zote mbili zisingeweza kuchukua kitu chochote chenye uhai. Ama huu mpango ulivyo sasa unapelekea kupishana usiku na mchana, na kwa hivyo kunapatikana mapumziko na utulivu wakati wa usiku, na kushughulika wakati wa mchana. Na hali ya hewa inasilihi uhai wa binaadamu, na wanyama, na mimea. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, ambazo zinapelekea tukubali uwezo wake, na tudumu kumshukuru.
Rudi kwenye sura

* 74. Na pia, ewe Mtume, kumbuka siku watapo itwa washirikina na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wito wa kuwatahayarisha, wakaambiwa: Wako wapi washirika ambao mkidai kuwa ni miungu wa kukunusuruni, au waombezi wa kukuombeeni?
Rudi kwenye sura

* 75. Na Siku ya Kiyama tutatoa kutoka kila umma shahidi, naye ndiye Nabii wao, wa kutoa ushahidi dhidi yao kwa waliyo kuwa wakiyafanya duniani. Hapo Sisi tutawaambia wakhalifu miongoni mwao: Nini hoja yenu kwa mliyo kuwa mkiyatenda ya ushirikina na maasi? Watashindwa kujibu, na watajua hapo kuwa Haki yote iko kwa Mwenyezi Mungu, tangu mwanzo mpaka mwisho. Na yatapotea, kama vinavyo potea vitu vilio potea, yote waliyo kuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 76. Sura hii inasimulia kisa cha Qaruni. Naye alikuwa katika kaumu ya Musa. Akapanda kiburi juu yao kwa kughurika kwa nafsi yake na mali yake. Na Mwenyezi Mungu alikuwa kampa khazina za mali mengi. Hata ikawa funguo zake tu zikiwaemea kundi la wanaume wenye nguvu! Na alipo ghurika na neema ya Mwenyezi Mungu juu yake, na akakufuru kwa sababu yake, watu walimpa nasaha, wakamwambia: Usidanganyike kwa mali yako, wala furaha kwa ajili yake isikusaliti hata ukaacha kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watu walio danganyika na wakasalitika. Na funzo la kisa hichi ni kuwa makafiri walio mkataa Muhammad s.a.w. walighurika na mali yao. Basi Qur'ani inawaelezea kuwa mali yao si chochote cha kutajika ukilinganisha na mali ya Qaruni.
Rudi kwenye sura

* 77. Na katika utajiri na neema alizo kupa Mwenyezi Mungu toa fungu kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, na tenda a'mali kwa ajili ya makaazi ya Akhera. Na wala usiinyime nafsi yako fungu lake kwa matumizi ya halali katika dunia. Na wafanyie wema waja wa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyo kufanyia wema wewe kwa neema zake. Wala usifanye uharibifu katika ardhi ukapita mipaka ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu hawafurahii mafisadi kwa vitendo vyao viovu. * 78. Basi Qaruni hakusikia nasaha ya watu wake, na akasahau fadhila ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yake. Na akajifanya hajui kwamba Mwenyezi Mungu alikwisha waangamiza wengi walio mzidi yeye sana katika uwezo na mazoezi ya kuchuma mali kwa njia mbali mbali za uchumi. Na wakosefu hawaulizwi madhambi yao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua. Basi wataingizwa Motoni bila ya hisabu. Kuulizwa kwao ni kwa ajili ya kutahayarishwa tu.
Rudi kwenye sura

* 78. Basi Qaruni hakusikia nasaha ya watu wake, na akasahau fadhila ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yake. Na akajifanya hajui kwamba Mwenyezi Mungu alikwisha waangamiza wengi walio mzidi yeye sana katika uwezo na mazoezi ya kuchuma mali kwa njia mbali mbali za uchumi. Na wakosefu hawaulizwi madhambi yao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua. Basi wataingizwa Motoni bila ya hisabu. Kuulizwa kwao ni kwa ajili ya kutahayarishwa tu.
Rudi kwenye sura

* 79. Na Qaruni hakujali nasaha za watu wake. Akawatokea naye kajipamba mapambo yake. Wakadanganyika naye wale walio kuwa wanapenda starehe za maisha ya dunia, na wakatamani nao wangeli kuwa nayo mali na hadhi kubwa ya maisha kama aliyo pewa Qaruni
Rudi kwenye sura

* 80. Ama wale ambao Mwenyezi Mungu amewaruzuku ilimu yenye manufaa hawakusalitika na hayo. Wakawaelekea walio danganyika kwa kuwanasihi wakiwaambia: Msiyatamani haya, wala msiiache Dini. Kwani yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ya thawabu na neema ni safi zaidi kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Na hiyo ni nasiha ya kweli ambayo hawaikubali ila wenye kuzipiga jihadi nafsi zao, na wakasubiri katika ut'iifu.
Rudi kwenye sura

* 81. Mwenyezi Mungu akamdidimiza katika ardhi, na ardhi ikammeza yeye na nyumba yake na vyote vilio kuwemo ndani yake, mali na mapambo yake. Hakuwa na wasaidizi wa kumkinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na wala yeye mwenyewe hakuweza kujinusuru nafsi yake.
Rudi kwenye sura

* 82. Na wale walio kuwa karibuni wakikitamani cheo chake cha duniani, wakawa wanatamka maneno ya masikitiko na majuto baada ya kuyafikiri yaliyo msibu yeye. Wakawa wanasema: Hakika Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake Waumini na wasio kuwa Waumini. Na humdhikisha amtakaye katika hao. Na wakawa wanasema kwa kushukuru: Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani kwa kutupa uwongofu tukafuata Imani, na akatuhifadhi tusiporonyoke angeli tutia katika mitihani kwa kutukubalia tuliyo kuwa tunayatamani, na akatufanyia kama alivyo mfanyia Qaruni. Hakika wanao ipinga neema ya Mwenyezi Mungu hawafanikiwi kwa kuokoka na adhabu yake.
Rudi kwenye sura

* 83. Hayo ndio makaazi ambayo umesikia khabari zake, ewe Mtume, na zikakufikia sifa zake, nayo ni Pepo. Tumeiweka makhsusi kwa ajili ya Waumini wat'iifu, wasio taka kujipa ubora na utukufu wa kidunia, na wala hawapotoki kuendea ufisadi na maasi. Na mwisho mwema ni wa wale ambao nyoyo zao zimejaa khofu ya Mwenyezi Mungu, na wanatenda yanayo mridhisha Yeye.
Rudi kwenye sura

* 84. Mwenye kuja na wema, nao ni Imani na vitendo vyema, atapata malipo marudufu kwa ajili yake. Na mwenye kuja na uovu, nao ni ukafiri na maasi, halipwi ila mfano wa vitendo vyake viovu.
Rudi kwenye sura

* 85. Hakika Mwenyezi Mungu aliye kuteremshia Qur'ani na akakulazimisha uifikishe kwa watu na ushikane nayo hapana shaka atakurudisha kwenye miadi, nako ni Siku ya Kiyama, ili apambanue baina yako na wale wanao kukadhibisha. Ewe Mtume! Waambie makafiri: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua kwa ujuzi usio pikuliwa na yeyote, nani aliye mpa uwongofu na uwongozi, na nani aliye tumbukia katika upotovu unao tambulikana na kila mwenye akili nzima.
Rudi kwenye sura

* 86. Ewe Mtume! Wewe hukuwa wewe ukitaraji na ukingojea uteremshiwe hii Qur'ani. Lakini Mwenyezi Mungu amekuteremshia kutoka kwake kwa kukurehemu wewe na umma wako. Basi ikumbuke neema hii, na shikilia kuifikisha. Wala usiwe wewe na wanao kufuata kuwa wasaidizi wa makafiri kwa wanayo yataka.
Rudi kwenye sura

* 87. Wala makafiri wasikuachishe kuzifikisha Aya za Mwenyezi Mungu na kuzitenda, baada ya kwisha teremka wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ukawa ndio Ujumbe wako. Na shikilia Wito kuwaitia watu kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu. Wala usiwe wewe wala wanao kufuata katika wasaidizi wa washirikina kwa kuwasaidia kwa wayatakayo.
Rudi kwenye sura

* 88. Wala usimwabudu mungu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Kwani hapana kabisa mungu wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye. Kila kitu isipo kuwa Mwenyezi Mungu kitaangamia na kwisha. Wa kudumu milele ni Yeye Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mwenye hukumu ya kutekeleza duniani na Akhera. Na kwake Yeye ndiyo yako marejeo ya viumbe vyote, hapana hivi wala hivi.
Rudi kwenye sura

Copyright ଵ 22 August 28997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani