AzZumar maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suurat Azzumar

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

*1. Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu, ambaye hana wa kumshinda kwa atakayo; Mwenye hikima katika vitendo vyake na utungaji wa sharia zake.
Rudi kwenye sura

*2.Hakika Sisi tumekuteremshia wewe, Muhammad, Qur'ani hii yenye kuamrisha Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia ibada Yeye tu peke yake.
Rudi kwenye sura

*3.Jueni na mtambue kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Dini isiyo kuwa na ila. Na washirikina walio wafanya wenginewe kuwa ni wasaidizi wa kuwanusuru, wanasema: Sisi hatuwaabudu hawa kwa kuwa ni waumbaji, bali tunawaabudu wapate kutukaribisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa mkaribisho wa kutuombea sisi kwake Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina ya hawa washirikina na Waumini wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja katika yale wanayo khitalifiana katika matatizo ya shirki na Tawhidi. Hakika Mwenyezi Mungu hamjaalii afikie Haki mtu ambaye mtindo wake ni uwongo na kukanya.
Rudi kwenye sura

*4.Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, kama wasemavyo Wakristo kwa Masihi, na washirikina kwa Malaika, basi angeli jichagulia amtakaye katika viumbe vyake, la sio kama mtakavyo nyinyi. Mwenyezi Mungu ametakasika na upungufu wa kuhitajia mwana. Yeye ni Mwenyezi Mungu asiye kuwa na mfano kama Yeye. Mtenda kama apendavyo, ukomo wa kutenda.
Rudi kwenye sura

*5.Ameumba mbingu na ardhi kwa kushikamana na Haki na kuwa sawa kwa kufuatana na sharia zilizo thibiti. Usiku unaufunika mchana, na mchana unaufunika usiku kwa mfululizo. Na amedhalilisha jua na mwezi kwa mujibu atakavyo na kwa mujibu wa maslaha ya waja wake. Kila kimojapo katika hivyo vinakwenda katika njia yake mpaka ufike wakati aliyo uwekea Yeye, nao ni Siku ya Kiyama. Jueni basi kuwa Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye kushinda kila kitu. Basi hapana kitu chochote kilicho tokana na atakavyo Yeye, ambaye amefikilia ukomo wa kuwasamehe wenye kutenda madhambi katika waja wake.
Aya hii tukufu inaonyesha kuwa ardhi ina sura ya mviringo kama mpira, na inazunguka wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake. Kwani kule kutumiwa neno Yukawwiru katika Kiarabu na ikafasiriwa Hufunika, maana yake ni kufunika kitu kwa kitu kwa namna ya kufuatana, kukariri, mara kwa mara. Na lau kuwa ardhi haina sura ya mpira, kwa mfano kuwa batabata tu, usiku ungeli enea kote kwa ghafla, au mchana ungeli angaza dunia nzima kwa mara moja.
Rudi kwenye sura

*6.Enyi watu! Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na nafsi moja, naye ni Adam, baba wa watu wote. Na amemuumba kutokana na nafsi hiyo mkewe, Hawa. Na amekuteremshieni kwa ajili ya maslaha yenu namna nane za nyama hoa, wanyama wa mifugo, madume na majike. Nao ni ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi. Naye anakuumbeni matumboni mwa mama zenu kwa kukua na kugeuka geuka, katika viza vitatu, navyo ni kiza cha tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio. Huyo aliye kuneemesheni kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu, Mlezi wenu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Ni Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye utawala wa pekee. Hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi yawaje hata wanaacha kumuabudu Yeye wakenda kuwaabudu wenginewe?
Huzuka yai katika mwahala pa kufanyika mayai kwa mwanamke, hata likisha kuwa tayari hutumbukia katika mojapo ya paipu za Filopia likapita humo mpaka kufikia kwenye tumbo la uzazi Rahimi (Womb). Halifiki huko ila kupita siku kidogo, na huenda kijidudu cha manii (Sperm) ya mwanamume kikaliingia hilo yai, na hapo huanza viwango vya kugeuka na kukua kwa mwanzo. Na katika tumbo la uzazi hubaki mtoto muda wa mimba, na hujifanyia vifuniko viwili, na sehemu ya funiko moja hufanyika zalio, placenta. Na funiko jingine ndio humfunika yule mtoto khasa.
Yapo maoni mbali mbali juu ya hivyo "viza vitatu" kama ilivyo tajwa katika Aya hii tukufu. Katika hayo ni
(1) Tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio, yaani mfuko unao mfunika mtoto.
(2) Tumbo la uzazi, na ile mifuniko miwili.
(3) Tumbo na mgongo na tumbo la uzazi.
(4) Panapo toka mayai (Mabiidh, au Ovaries), na paipu ya kupitia mayai, Fillopian tube, na tumbo la uzazi (Rahimi au Womb).
Na dhaahiri ni kuwa hii ya mwisho ndiyo rai yenye nguvu zaidi, kwa sababu ni mahala patatu mbali mbali. Ama zile rai nyengine zinaonyesha kwa hakika kiza kimoja katika pahala pamoja palipo zungukwa na t'abaka kadhaa. Na Muumbaji Mtukufu ameashiria katika Kitabu chake ukweli huu wa kisayansi katika zama walipo kuwa watu hawajavumbua hayo mayai ya mwanamke na mwendo wake katika mwili ulio kuwa hauwezi kuonekana kwa macho.
Rudi kwenye sura

*7.Enyi watu! Mkizikataa neema za Mwenyezi Mungu, basi Yeye hakika si mhitaji wa imani yenu na shukrani zenu. Lakini Yeye hapendi waja wake wakufuru, kwa sababu hayo yanawadhuru wenyewe. Na mkimshukuru kwa ajili ya neema zake, Yeye huwa radhi nanyi kwa shukra hiyo. Wala mtu mwenye madhambi hayabebi madhambi ya mwenginewe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, na hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda duniani. Hakika Yeye anayajua mnayo yaficha katika nyoyo zenu ziliomo vifuani.
Haya yaliomo katika Qur'ani Tukufu yanaweka wazi msingi wa kutoa adhabu, kama ilivyo vile vile katika Surat Yusuf katika kauli yake Mtukufu: "Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali sisi kumshika yeyote ila tuliye yakuta mali yetu kwake; hivyo basi tutakuwa madhaalimu." Na haya katika Qur'ani ni kusimamisha msingi ulio kwisha tajwa, nao ni msingi ambao haukuthibiti katika kanuni (sharia) za kutungwa na binaadamu ila katika zama za karibuni. (Haya ni kinyume cha ilivyo katika imani aliyo itumbukiza Paulo katika Ukristo, kwamba wanaadamu wamerithi dhambi ya Adam, wanayo ita "Dhambi ya asili", na kwamba Nabii Isa, Yesu, kafa msalabani kwa kubeba dhambi za wanaadamu. Biblia yenyewe inapinga haya. Tazama: Jeremiah 31:29-30; Ezekieli 18 Kwa nadhariya ya Paulo Mungu amedhulumu mara mbili:
1. Kutubandika wanaadamu wote dhambi za Adam,
2. Kumbebesha "mwanawe" Yesu dhambi za walimwengu wote!)
Rudi kwenye sura

*8.Na mtu akifikiwa na shida yoyote katika shida za dunia humwomba Mola wake Mlezi, na hurejea kwake, baada ya kuwa akimpuuza. Kisha Mola wake Mlezi akimpa neema kubwa husahau zile taabu alizo kuwa akimwombea Mola wake Mlezi amwondolee na amfarijie kabla hajamneemesha kwa neema hizo. Na humfanyia Mwenyezi Mungu miungu washirika walio sawa na Yeye kwa kuwaabudu. Huyo mtu hufanya haya ili ajipoteze yeye na wenginewe waiache Njia ya Mwenyezi Mungu. Ewe Muhammad! Mwambie huyo mwenye sifa hizi kwa kumwonya: Starehe na huko kuzikanya kwako neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe ni katika watu wa Motoni.
Rudi kwenye sura

*9.Je! Mwenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu nyakati za usiku anao upitisha na hali yeye yumo kusujudu na kusimama, akiiogopa Akhera, naye anataraji rehema ya Mola wake Mlezi, ni kama anaye mwomba Mola wake Mlezi wakati wa shida na akamsahau wakati wa neema? Ewe Muhammad! Waambie: Ati wanakuwa sawa wenye kujua haki za Mwenyezi Mungu wakamuabudu Yeye tu peke yake, na wale wasio jua wakapuuza kuziangalia Ishara? Hakika wenye akili nzuri ndio wanao waidhika.
Rudi kwenye sura

*10.Ewe Nabii! Sema kwa kufikisha Ujumbe unao toka kwa Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu mlio niamini! Jikingeni na ghadhabu za Mola wenu Mlezi. Mwenye kutenda mema atalipwa mema, duniani kwa kusaidiwa, na Akhera kwa Pepo. Wala msikae katika unyonge, kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu ina wasaa. Na subirini kwa kufarikiana na nchi zenu na wapenzi wenu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye kusubiri ujira wao mara zisio ingia katika hisabu za wanao hisabu.
Rudi kwenye sura

*11.Sema: Mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ibada yangu isiwe na shirki ndani yake wala riya ya kujionyesha kwa watu.
Rudi kwenye sura

*12.Na nimeamrishwa amri iliyo tokana naye Mtukufu, amri ya nguvu, ya kwamba niwe wa mwanzo wa kufuata amri zake.
Rudi kwenye sura

*13.Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku Kubwa yenye vitisho ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.
Rudi kwenye sura

*14.Ewe Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo dhaahiri.
Rudi kwenye sura

*15.Ewe Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo dhaahiri.
Rudi kwenye sura

*16.Hawa walio khasirika watakuwa na mat'abaka ya Moto yalio rindikwa juu yao, na chini yao hali kadhaalika. Kwa namna ya adhabu hiyo ndio Mwenyezi Mungu anawahadharisha waja wake. Enyi waja wangu! Basi yaogopeni mateso yangu.
Rudi kwenye sura

*17.Na wale wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika.
Rudi kwenye sura

*19.Na wale wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika.
Rudi kwenye sura

*20.Je! Unaweza kuniingilia katika Ufalme wangu? Iliyo kwisha pita juu yake hukumu ya kumuadhibu, je, wewe unaweza kuizuia? Unayo nguvu hiyo wewe? Je! Unaweza kuwaokoa na Moto baada ya kwisha wathibitikia?
Rudi kwenye sura

*21.Lakini wenye kumkhofu Mola wao Mlezi watapata vyeo vya juu Peponi na majumba yake ya fakhari, yenye kupitiwa chini yake na mito. Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu haendi kinyume na ahadi yake.
Rudi kwenye sura

*22.Ewe usemezwaye! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, akayapitisha kwenye mito na chemchem za katika ardhi, kisha kwa maji hayo akaotesha mimea ya namna mbali mbali. Kisha baada ya kustawi kwake hiyo mimea, ikayabisika ukaiona imekuwa rangi ya manjano baada ya kustawi kwake. Kisha akaifanya imevurugika na kukatika vipande vipande. Hakika kutoka kwenye hali moja na kuingia hali nyengine ni mazingatio kwa wenye akili zilizo nawirika.
Huku kuzunguka maji katika maumbile kutoka mbinguni na kufika kwenye ardhi na huko yakenda chini na kutimbuka katika chemchem, hakukuwa kunajuulikana kabla ya katikati za karne ya nane tangu kuzaliwa Nabii Isa a.s. Fikra iliyo zagaa kabla ya hapo ni kuwa maji ya chemchem na mito yanatimbuka kutoka chini ya ardhi kutoka kwenye mashimo na visima katika vina vya bahari.
Rudi kwenye sura

*23.Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kufunguliwa kifua chake na Mwenyezi Mungu kwa Uislamu kwa kupokea mafunzo yake, na akawa na utambuzi unao tokana na Mola wake Mlezi, huyo basi ni kama yule anaye kataa kuangalia Ishara zake? Basi hao ambao nyoyo zao zimekuwa ngumu hata hawamkumbuki Mwenyezi Mungu watapata adhabu kali! Hao wenye nyoyo ngumu wameitupa Haki iliyo wazi.
Rudi kwenye sura

*23.Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, nayo ni Kitabu ambacho zimeshabihiana maana zake na matamko yake kwa kufikilia ukomo wa kuwashinda watu kuleta mfano wake, na hukumu zake. Mawaidha na hukumu zinakaririwa, kama kunavyo kaririwa kusomwa kwake. Kinapo somwa Kitabu hicho na kikasikiwa maonyo yake, ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi hukunjika, na kisha hulainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hicho Kitabu kilicho kusanya sifa hizi ni Nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo humwongoa amtakaye, ikamwezesha kufikilia kumuamini Yeye. Na anaye achwa na Mwenyezi Mungu apotee kwa kumjua kuwa tangu hapo ataiacha Haki, basi hapati mwongozi wa kumwokoa na upotofu wake.
Rudi kwenye sura

*24.Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kuikinga adhabu ovu, kali, kwa uso wake Siku ya Kiyama baada ya kuwa mikono yake imetiwa pingu, ni kama anaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Na wenye kudhulumu wataambiwa: Onjeni laana ya vitendo vyenu!
Rudi kwenye sura

*25.Walikanusha walio kuja kabla ya washirikina hawa, ikawajia adhabu kutoka upande wasio utaraji.
Rudi kwenye sura

*26.Mwenyezi Mungu akawaonjesha unyonge katika maisha ya duniani. Ninaapa: Hakika adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi kuliko ya duniani, lau kwamba walikuwa ni watu wa kujua na kuangalia!
Rudi kwenye sura

*27.Na bila ya shaka tulikwisha wabainishia watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano wa kuwakumbusha Haki, kwa kutaraji kuwa watakumbuka na watawaidhika.
Rudi kwenye sura

*28.Tumeiteremsha Qur'ani ya Kiarabu kwa ulimi wao, haina upungufu, kwa kutaraji kuwa watamcha na watamwogopa Mola wao Mlezi.
Rudi kwenye sura

*29.Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mshirikina kama mtumwa aliye milikiwa na watu kadhaa wenye kushirikiana, na wenye kumgombania. Na mfano wa mwenye kuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kama mtu ambaye amemilikiwa na mtu mmoja tu. Je hao wanakuwa sawa? Alhamdulillahi kwa kusimama hoja mbele ya watu. Lakini watu wengi hawaijui Haki.
Rudi kwenye sura

*30.Hakika wewe, Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi.
Rudi kwenye sura

*31.Hakika wewe, Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi.
Rudi kwenye sura

*32.Basi hapana aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye msingizia Mwenyezi Mungu lisio kuwa lake, na akaikanusha Haki bila ya kufikiri wala kuzingatia pale inapo mjia kwa ndimi za Mitume. Kwani katika Jahannamu sio makaazi ya makafiri walio ghurika hata wakamfanyia jeuri Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye sura

*33.Na wale walio ileta Haki na wakaisadiki ilipo wajia, hao ndio wachamngu kweli, wala si wengineo.
Rudi kwenye sura

*34.Wachamngu hao watapata kutoka kwa Mola wao Mlezi kila wakipendacho. Fadhila hiyo ni malipo ya kila mwenye kufanya vizuri katika itikadi yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye sura

*35.Mwenyezi Mungu amewakirimu wachamngu kwa alivyo wakirimu, ili awafutie vile vitendo vyao viovu kabisa, na awalipe ujira wao kwa bora ya vitendo vyao walivyo vitenda duniani.
Rudi kwenye sura

*36.Mwenyezi Mungu, peke yake, ni Mwenye kuwatosheleza waja wake kwa kila lilio wakhusu. Na ati hao makafiri wa Kikureshi wanakutisha, ewe Muhammad, kwa miungu yao wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu. Na hayo ni katika upotovu wao. Na mwenye kupotozwa na Mwenyezi Mungu, kwa kumjua kuwa huyo amekhiari upotovu kuliko uwongofu, basi hatakuwa na mwongozi wa kumwongoza.
Rudi kwenye sura

*37.Na mwenye kuongozwa na Mwenyezi Mungu kuendea Haki, na akamwezesha kuifikia, kwa kujua kwake kuwa huyo amekhiari uwongofu kuliko upotovu, basi hatokuwapo wa kumpotoa akaiacha Njia ya Uwongofu. Kwani Mwenyezi Mungu si ndio Yeye ambaye hashindiki kwa kila upande, ambaye ni Mwenye kulipiza kwa ukali? Na kwa hivyo huwalinda vipenzi vyake na maadui wake?
Rudi kwenye sura

*38.Na ninaapa, lau ungeli wauliza, wewe Muhammad, hawa washirikina: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka wangeli sema: Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba. Ewe Muhammad, waambie: Mmezingatia mkawaona hao miungu mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu, wanaweza kuniondolea madhara ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kunidhuru? Au wanaweza kunizuilia rehema yake akitaka inifikie? Ewe Muhammad! Waambie: Anaye nitosheleza kwa kila kitu ni Yeyey peke yake, si mwenginewe, ndiye Yeye wanaye mtegemea wote wanao tegemea na kumwachilia kila kitu.
Rudi kwenye sura

*39.Waambie, kwa kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi. Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?
Rudi kwenye sura

*40.Waambie, kwa kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi. Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?
Rudi kwenye sura

*41.Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani Tukufu hii kwa watu wote, nayo imekusanya Haki iliyo thibiti. Basi mwenye kuongoka kwa sababu yake basi manufaa hayo ni kwa nafsi yake, na mwenye kuipotea njia yake basi balaa ya upotofu wake itamrejea mwenyewe. Wala wewe, Muhammad, si mwenye kuwakilishwa uwongofu wao. Jukumu lako ni kufikisha ujumbe, nao umeufikisha.
Rudi kwenye sura

*42.Mwenyezi Mungu huzitakabadhi roho zinapo kufa. Na huzipokea roho zisio kufa zinapo lala. Basi huzizuia zilizo kwisha hukumiwa kufa, zisirudi kwenye miili yao, na huzirudisha nyenginezo ambazo hazijafikilia bado ajali yao, wakati wa kuamka, mpaka itakapo fika ajali yao ilio wekewa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara wazi kwa watu wanao zingatia.
Rudi kwenye sura

*43.Bali washirikina wakawafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni waombezi wao wa kuwakurubisha kwake. Waambie, ewe Muhammad: Mnafanya haya ijapo kuwa hawa mnao wafanya "waombezi" hawanacho wanacho kimiliki, wala hawana wanacho kifahamu?
Rudi kwenye sura

*44.Ewe Muhammad! Waambie: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake! Hapana anaye upata ila aridhie Yeye. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake Yeye tu. Na kisha mtarejeshwa kwake, akuhisabieni vitendo vyenu.
Rudi kwenye sura

*45.Na pindi akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake, bila ya kutajwa miungu yao, nyoyo za wasio yaamini maisha ya Akhera hukunjana na kukasirika. Na wakitajwa miungu yao wanayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu wao huwa wepesi kufurahi na kustarehe.
Rudi kwenye sura

*46.Ewe Muhammad! Sema, nawe umemwelekea Mola wako: Ewe Mwenyezi Mungu! Ewe Muumba mbingu na ardhi bila ya mithali! Ewe Mjuzi wa siri na dhaahiri! Wewe peke yako, ndiye wa kuhukumu baina ya waja wako katika hayo wanayo khitalifiana katika mambo ya dunia na Akhera. Basi hukumu baina yangu na hawa washirikina!
Rudi kwenye sura

*47.Na lau kuwa hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ushirikina wanamiliki vyote viliomo duniani na mara mbili kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kuwa ni fidia ya kujigombolea nafsi zao na adhabu waliyo andaliwa Siku ya Kiyama. Nao watakuja iona adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu ambayo haikupata kuwapitikia katika mawazo yao.
Rudi kwenye sura

*48.Na katika Siku hii ya leo utawadhihirikia uovu wa vitendo vyao, na itawazunguka adhabu ya yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhaara duniani.
Rudi kwenye sura

*49.Na mtu yakimpata madhara hutuomba kwa unyenyekevu; kisha tukimpa neema kwa kumfadhili, mtu huyo huyo husema: Sikupewa neema hizi mimi ila kwa ujuzi wangu nilio nao wa kujua kuchuma. Naye mtu huyu kasahau kuwa mambo si hivyo kama asemavyo, bali neema hizo alizo mneemesha Mwenyezi Mungu ni kama majaribio tu, ni mtihani, ili amdhihirishe nani mwenye kut'ii na nani mwenye kua'si. Lakini wengi wa watu hawatambui kama hayo ni majaribio na fitna.
Rudi kwenye sura

*50.Maneno kama haya waliyasema walio kuwa kabla ya washirikina hawa, na hayakuwalinda na adhabu hayo mali na starehe waliyo yachuma.
Rudi kwenye sura

*51.Yakawasibu makafiri walio tangulia malipo ya madhambi ya vitendo vyao, na madhaalimu miongoni mwa hawa wanao semezwa hivi sasa yatawapata vile vile malipo ya madhambi ya vitendo vyao. Wala hawa hawataiepuka adhabu.
Rudi kwenye sura

*52.Je! Hawa wanasema wayasemayo, wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humpa kwa kadiri atakacho kwa mujibu wa hikima yake? Hakika katika haya bila ya shaka ni mazingatio kwa watu wanao amini.
Rudi kwenye sura

*53.Ewe Muhammad! Sema kwa kufikisha kutokana na Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu walio jizidishia juu ya nafsi zao maasi, msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi yote. Hakika Yeye, peke yake, ndiye Mkuu katika kusamehe kwake na kurehemu kwake.
Rudi kwenye sura

*54.Enyi mlio jidhulumu nafsi zenu, rejeeni kwa Mwenye kuyamiliki mambo yenu yote, na Mlezi wenu. Na mfuateni Yeye kabla haijakujieni adhabu, tena hapo hapatakuwepo wa kukunusuruni na Mwenyezi Mungu na kukulindeni na adhabu yake.
Rudi kwenye sura

*55.Na fuateni yaliyo bora kabisa katika mliyo teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi, nayo ni Qur'ani Tukufu, kabla ya kukujieni adhabu kwa ghafla, na bila ya kujitayarisha, na hali nyinyi hamjui kuja kwake.
Rudi kwenye sura

*56.Rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na Msilimu kwake, na mfuate mafunzo yake, ili nafsi yenye dhambi isisema itapo iona adhabu: Ee msiba wangu kwa niliyo yawacha upande wa Mwenyezi Mungu na katika haki zake, na kwamba mimi nilikuwa duniani miongoni mwa walio kuwa wakiifanyia maskhara Dini yake.
Rudi kwenye sura

*57.Au iseme ile nafsi yenye dhambi, kutafuta udhuru: Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli niwezesha kufuata uwongofu bila ya shaka ningeli kuwa duniani katika wale walio jilinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa Imani na vitendo vyema.
Rudi kwenye sura

*58.Au iseme nafsi ile yenye dhambi itapo ona adhabu: Laiti ningeli rejeshwa duniani, nikawa katika wanao tengeneza imani yao na vitendo vyao!
Rudi kwenye sura

*59.Utayapata wapi, ewe mwenye majuto! Mafunzo yangu yalikujia katika ndimi za Mitume, nawe ukayakanusha, na ukajiona bora, ukakataa kuyafuata, na ukawa katika dunia yako miongoni mwa wenye kushikilia ukafiri.
Rudi kwenye sura

*60.Na Siku ya Kiyama utawaona walio mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, wakamkhusisha yasiyo kuwa yake, nyuso zao zimesawjika kwa huzuni na majonzi. Hakika Jahannamu ndio makaazi ya wenye kiburi wakaikataa Haki.
Rudi kwenye sura

*61.Na Mwenyezi Mungu atawaokoa alio wajaalia ulinzi isiwapate adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa vile alivyo kwisha wajua kuwa wamefuzu, kwa walivyo ukhiari uwongofu kuliko upotofu. Na siku hii basi uovu hautawagusa, wala hawatahuzunika kwa kuzikosa neema walizo kuwa wakizitaraji.
Rudi kwenye sura

*62.Mwenyezi Mungu Muumba kila kitu - naye peke yake - ndiye Mlinzi wa kila kitu. Anaendesha mambo yake kwa mujibu wa hikima yake.
Rudi kwenye sura

*63.Maendesho ya mambo ya katika mbingu na ardhi yako kwa Mwenyezi Mungu. Hayaendeshi hayo isipo kuwa Yeye. Na makafiri kwa hoja za Mwenyezi Mungu na ushahidi wake ndio wao, peke yao, ndio wenye kukhasiri, mwisho wa kukhasiri!
(Injili ya Mathayo 16:16-20 imedai kuwa Yesu kampa funguo za mbingu na ardhi Petro, na hivyo ndiyo Papa wa Roma amerithi funguo hizo na kuanzisha Kanisa la Kikatoliki, na uwezo wa kufutia watu dhambi na kuwaangamiza Motoni. Marcello Craveri, mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana ameandika katika kitabu chake Maisha ya Yesu (sahifa 227-28 Panther Edn.) kuwa Mathayo 16:16-20 imeongezwa na ametoa hoja 7 kwa wazo hilo. Licha ya kuwa Yesu hakumpa Petro hizo funguo za mbingu na ardhi, yeye mwenyewe Yesu hakuwa nazo.)
Rudi kwenye sura

*64.Ewe Muhammad! Sema: Je! Baada ya kuweka wazi Ishara zote kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja wa kuabudiwa, mnaniamrisha nimuabudu mwenginewe, enyi wajinga, majaahili?
Rudi kwenye sura

*65.Na ninaapa: Bila ya shaka, umepewa Wahyi, wewe, Muhammad na Mitume walio kuwa kabla yako, kwamba bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote kile basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atazibat'ilisha a'mali zako, na utakuwa katika watu walio khasirika ukomo wa kukhasiri.
Rudi kwenye sura

*66.Ewe Mtume! Usiwakubalie kwa hayo wanayo kutaka, bali muabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na uwe katika wanao mshukuru Yeye kwa neema zake.
Rudi kwenye sura

*67.Washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki utukufu wake, wala hawakumjua kama anavyo stahiki kujuulikana, kwa kuwa wamemshirikisha pamoja naye wenginewe, na wakamtaka Mtume naye aingie katika ushirikina, na hali ardhi yote ni milki yake Siku ya Kiyama, na mbingu zitakuwa zimekunjwa, kama zinavyo kunjwa nguo, katika mkono wake wa kulia. Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu, na ametukuka vikubwa mno na vyote hivyo wanavyo mshirikisha naye.
Rudi kwenye sura

*68.Na litapulizwa barugumu kwa yakini (1), na watakufa walioko mbinguni na katika ardhi ila anaye mtaka Mwenyezi Mungu kumuakhirisha mpaka wakati mwengine. Kisha litapulizwa mara nyengine, na hapo wote watainuka kutoka makaburini mwao, wakingojea watafanywa nini?
(1) Hilo barugumu (S'ur) kilugha, ni tarumbeta, mbiu, siwa, parapanda. Barugumu inalo tusimulia Qur'ani ni katika mambo ya ulimwengu usio onekana, hatujui lilivyo na hakika yake.
Rudi kwenye sura

*69.Na ardhi itang'ara siku hiyo kwa nuru ya Muumba wake na Mmiliki wake. Na kitatayarishwa Kitabu kilicho sajiliwa ndani yake vitendo vyao, na watahudhurishwa Manabii na mashahidi wapate kuwashuhudia viumbe vyote, na wapambanuliwe baina ya viumbe kwa uadilifu, na wala hawatadhulumiwa kwa kupunguziwa thawabu wala kuzidishiwa adhabu.
Rudi kwenye sura

*70.Na kila nafsi itapewa malipo ya a'mali yake, na Mwenyezi Mungu ni mbora wa kujua vitendo vyao.
Rudi kwenye sura

*71.Na makafiri watahimizwa kwenda kwa nguvu kuendea Jahannamu kwa makundi makundi. Na hata watapo fika milango yake itafunguliwa, na walinzi wake watawaambia kwa kuwakebehi: Kwani hawakuja kwenu Wajumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu wa jinsi yenu, wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi, na wakakuhadharisheni na mkutano wenu huu? Makafiri watasema kwa kukiri: Kwani! Walitujia Mitume. Lakini neno la adhabu limekwisha wajibikia juu ya makafiri, kwa kuwa wao wamekhiari ukafiri kuliko Imani.
Rudi kwenye sura

*72.Wataambiwa: Iingieni milango ya Jahannamu mliyo jaaliwa mkae humo milele. Jahannamu ni pahala paovu mno pa kukaa wenye kutakabari na wakakataa kuikubali Haki.
Rudi kwenye sura

*73.Na wachamngu watahimizwa kwenda Peponi kwa hishima makundi makundi, mpaka wakifika kwenye milango yake, wataambiwa na walinzi wake: Amani kubwa juu yenu! Mmet'ahirika duniani na uchafu wa maasi, na mmet'ahirika Akhera katika nafsi zenu kwa neema mlizo zipata. Basi ingieni Peponi mliko jaaliwa kukaa milele. Kwani nyinyi mna neema zisio pita akilini.
Rudi kwenye sura

*74.Na wachamngu watasema: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, ambaye ametutimizia aliyo tuahidi kwa ndimi za Mitume wake, na akatumilikisha ardhi ya Peponi tunashukia tutakapo humo. Ama hakika bora ya ujira wa wenye kutenda mema ni Pepo.
Rudi kwenye sura

*75.Na utaona, ewe mwenye kuona, Malaika wakiizunguka A'rshi, wakimtakasa Mwenyezi Mungu na kila upungufu, kwa utakaso unao fuatana na kumhimidi Muumba wao na Mlezi wao, na akapambanua baina ya viumbe vyote kwa uadilifu, na ulimwengu wote ukatamka kwa kusema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani