Al Ah'qaaf maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Ah'qaaf

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Imeanzia Sura hii kwa baadhi ya harufi kama ilivyo ada ya Qur'ani katika Sura kadhaa wa kadhaa.
Rudi kwenye sura

* 2. Hii Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika ayatendayo.
Rudi kwenye sura

* 3. Hatukuziumba mbingu na ardhi na vyote vilio baina yake ila kufuatana na sharia zilizo thibiti, kwa makusudio yanayo ambatana na hikima, na kwa muda maalumu ambao baada yake utakwisha. Na wale wanao ukataa ukweli huu wanapuuza yale waliyo onywa kwayo, ya kuumbwa kupya siku watakapo fufuliwa watu kwa ajili ya malipo.
Rudi kwenye sura

* 4. Waambie hao wanao muomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Hebu nambieni hali ya hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu. Nijuvyeni wameumba nini katika ardhi, au wana ushirika wowote katika mbingu? Nileteeni Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, au mabaki yoyote kutokana na ilimu za watu wa zamani ambayo mnayategemea kwa madai yenu, ikiwa mnasema kweli.
Rudi kwenye sura

* 5. Na nani aliye zidi kupotea kuliko anaye muacha Mwenyezi Mungu akaiomba miungu mingine ambayo haitamjibu kitu mpaka mwisho wa dunia, na ambao hao hata hawana khabari ya maombi yao.
Rudi kwenye sura

* 6. Na watu wakikusanywa kwa ajili ya hisabu Siku ya Kiyama hawa wanao abudiwa kwa upotovu watakuwa ndio maadui wa walio kuwa wakiabudu, na watajitenga nao, na kuwakadhibisha kwa madai yao kwamba wao wanastahiki kuabudiwa. (Katika Injili ya Mathayo inasimuliwa wazi vipi Nabii Isa a.s. atavyo wakataa Wakristo wanao muabudu yeye. Tazama Mathayo 7.22-23. Yesu anasema: "Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.")
Rudi kwenye sura

* 7. Na washirikina wakisomewa Aya zetu zilizo wazi wao husema, kwa ule ukafiri wao na inadi yao, bila ya kuzingatia, kuzisema hizo Aya: Huu ni uchawi dhaahiri!
Rudi kwenye sura

* 8. Bali wanasema hawa makafiri: Muhammad ameizua hii na akamsingizia Mwenyezi Mungu! Sema kuwajibu: Ikiwa mimi nimeizua hii Mwenyezi Mungu atanipatiliza upesi upesi, wala nyinyi hamwezi kunilinda hata kwa chembe ya adhabu. Yeye peke yake ndiye Mwenye kujua kabisa hayo mnayo ropokwa katika kuzitia kombo Aya zake. Na Yeye anatosha kunishuhudia ukweli wangu, na kukushuhudilieni nyinyi kuwa mnanikadhibisha. Na Yeye pekee, ndiye Mkunjufu wa msamaha kwa mwenye kutubu, Mkubwa wa rehema, kwa kuwapa muhula wenye kuasi ili wadiriki kurejea.
Rudi kwenye sura

* 9. Waambie: Mimi sikuwa Mtume wa mwanzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata ndio muukatae ujumbe wangu. Wala mimi sijui Mwenyezi Mungu atanifanya nini na atakufanyeni nini nyinyi. Mimi sifuati ninayo sema au kutenda ila anayo nifunulia Mwenyezi Mungu. Wala mimi si chochote ila ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji.
Rudi kwenye sura

* 10. Sema: Hebu nambieni, ikiwa hii Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu na nyinyi mkaikataa, na hali ameshuhudia shahidi katika Wana wa Israili kuwa imeshuka mfano wa hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawa yeye kaamini na nyinyi mkatakabari, basi hapo nyinyi si mtakuwa ni wenye kupotea na wenye kujidhulumu wenyewe kuliko watu wote? Hakika Mwenyezi Mungu hamsaidii kuongoka mwenye kujidhulumu mwenyewe na akapanda kiburi kuikataa Haki.
Rudi kwenye sura

* 11. Na walio kufuru walisema kuwakhusu walio amini, kwa kejeli na majivuno juu yao: Ingeli kuwa aliyo kuja nayo Muhammad ni ya kheri, basi wasingeli tutangulia hawa katika kuyaamini. Kwani sisi ndio twenye ubwana, na akili bora! Na ilivyo kuwa hawakuyafuata basi wakaangukia kuyatoa kombo, wakisema: Huu ni uwongo wa zamani unatokana na hadithi za watu wa kale!
Rudi kwenye sura

* 12. Na kabla ya Qur'ani Mwenyezi Mungu aliteremsha Taurati kuwa ni uwongozi na rehema kwa wenye kuitenda. Na hii Qur'ani wanayo ikadhibisha inasadikisha Vitabu vilivyo kwisha tangulia. Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwa lugha ya Kiarabu iwe ni onyo jipya kwa wenye kudhulumu, na bishara kwa wenye kusimama sawa juu ya Njia.
Rudi kwenye sura

* 13. Hakika wanao sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu peke yake, kisha wakatengenea kwa kufanya vitendo vizuri, watu hao hawana khofu ya kushukiwa la karaha, na wala hawatahuzunika kwa kuyakosa wayatakayo.
Rudi kwenye sura

* 14. Hao wanao sifika kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na kusimama sawa, ndio walio khusika kuingia Peponi wakikaa humo milele. Mwenyezi Mungu amewapa hayo kuwa ni jaza yao kwa mema waliyo kuwa wakiyatenda.
Rudi kwenye sura

* 15. Na tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake awafanyie wema mkubwa. Kwani mama yake amechukua mimba yake kwa mashaka, na akamzaa kwa mashaka. Na muda wa kuchukuliwa mimba mpaka kuachishwa ziwa ni miezi thalathini. Muda wote huo mama kapitikiwa na kila namna ya machungu. Mpaka huyo mtu alipo fikilia ukamilifu wa nguvu zake na akili yake, na akafikia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Nijaalie niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nijaalie nitende vitendo vyema utavyo viridhi Wewe, na ujaalie huo wema wapate pia dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako kwa kila dhambi, na mimi ni miongoni wa Waislamu, yaani walio zisalimisha nafsi zao kwako. Uchache wa mimba ni miezi sita, kwa kauli yake Mtukufu: " Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini." Na kauli yake Mtukufu: "Na kumwachisha ziwa kwake ni miaka miwili", na kauli yake Mtukufu: "Na wazazi wa kike huwanyonyesha wana wao miaka miwili kaamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha." Basi ukitoa muda wa kuachisha ziwa kutokana na muda wa mimba na kunyonyesha inabakia muda wa mimba ni miezi sita. Na haya yanawafikiana na iliyo thibiti kwa ilimu za sayansi kwamba mtoto mchanga akizaliwa baada ya mimba ya miezi 6 anaweza kuishi.
Rudi kwenye sura

* 16. Hao walio sifika kwa sifa hizo ndio tutakao wapokelea a'mali zao njema, na tutawasamehe maovu yao miongoni mwa watu wa Peponi. Itawathibitikia miadi ya kweli walio kuwa wakiahidiwa duniani.
Rudi kwenye sura

* 17. Na waliwafyonya wazazi wao kwa kuchukia na kuchoka nao, walipo wataka waamini kufufuliwa, na wakawaambia: Mnaniambia tutatoka makaburini na mataifa mangapi yamepita kabla yangu na hapana hata mmoja aliye fufuliwa kutoka makaburini? Na hao wazazi wake wanaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu jinsi ya kuona ni makuu makosa ya mwana wao, wakisema kwa kumshikilia aamini: Utaangamia wewe kama hukuamini. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua ni kweli. Naye bado amekakamia kukadhibisha kwa kusema: Hayo mnayo yasema si chochote ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale!
Rudi kwenye sura

* 18. Hao wasemao hayo ndio iliyo wathibitikia kuwashukia adhabu sawa sawa na mataifa yaliyo kuwa kabla yao miongoni mwa majini na watu, kwa sababu hakika hao walikuwa ni wenye kukhasiri.
Rudi kwenye sura

* 19. Na wote, Waislamu na makafiri, wana vyeo vyao vinavyo lingana na vitendo vyao walivyo vitenda, ili uadilifu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana kati yao, na ili awalipe jaza ya 'amali zao, nao hawatadhulumiwa, kwa sababu wanastahiki hayo wanayo lipwa.
Rudi kwenye sura

* 20. Na siku watakapo simamishwa walio kufuru kwenye Moto waambiwe: Mmekwisha chukua fungu lenu la vitu vizuri katika maisha yenu ya duniani, na mkavionea raha. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya kufedhehesha kwa mliyo kuwa nayo duniani, ya kujivuna katika nchi bila ya haki, na kutoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 21. Mtaje Hud, mwenzao kabila ya A'di, alipo wahadharisha watu wake wanao kaa Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na Mitume kadhaa walikuja kabla yake na baada yake kwa maonyo kama yake ya kusema: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Mimi nakukhofieni isikupateni adhabu yenye vitisho vikuu. Maskani ya kabila hii ilikuwa huko Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na wapi hapo Ah'qaaf? Zipo khitilafu. Baadhi ya wanazuoni wa taarikh (historia) wanasema kuwa hapo ni baina ya Yaman na Oman mpaka Hadhramaut na Shihr, yaani mashariki ya kusini ya Bara Arabu. Na baadhi ya wachunguzi wa zama za karibu wanaona ni mashariki ya A'qaba, wakitegemea maandishi ya Nabat'ia waliyo yakuta katika magofu ya hekalu walilo livumbua katika mlima wa Arim. Walikuta pembezoni mwa mlima huo mabaki ya siku za Jahiliya za zamani. Wakasahihisha kuwa hapo ndipo ilipo Arim iliyo tajwa katika Qur'ani tukufu. Kisha kabila hiyo ikatoka hapo kabla ya Uislamu, na hapana kilicho baki chao isipo kuwa chemchem ya maji ambayo wafanyi biashara na watu wa misafara wakishukia hapo katika njia yao kwendea Shamu.
Rudi kwenye sura

* 22. Kaumu ya Hud walisema kwa kumkanya: Hivyo ndio umetujia ili utuachishe kuwaabudu miungu yetu? Basi tuletee hiyo adhabu ikiwa wewe hakika ni mwenye kusema kweli kwa ahadi hiyo.
Rudi kwenye sura

* 23. Hud akasema: Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua wakati wa kuileta adhabu yenu. Mimi nafikisha ujumbe tu nilio tumwa. Lakini naona kuwa nyinyi hamjui chochote katika mambo wanayo tumwa Mitume.
Rudi kwenye sura

* 24,25. Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda kote juu linaelekea mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili linatuletea mvua na kheri. Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza, nayo ni upepo wenye adhabu kali na chungu, itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza, yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kutenda kama makosa yao.
Rudi kwenye sura

* 24,25. Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda kote juu linaelekea mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili linatuletea mvua na kheri. Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza, nayo ni upepo wenye adhabu kali na chungu, itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza, yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kutenda kama makosa yao.
Rudi kwenye sura

* 26. Na tuliwaweka kabila la A'di kwa nafasi na nguvu sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi watu wa Makka. Na tuliwajaalia masikio, na macho, na nyoyo, lau wangeli taka kunafiika kwayo. Lakini hayakuwafaa hata kitu kidogo masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao, kwa sababu walikuwa wakizikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi hayo yakapinga baina yao na kunafiika kwa waliyo letewa. Na ile ile adhabu waliyo kuwa wakiifanyia maskhara ikawazunguka.
Rudi kwenye sura

* 27. Enyi watu wa Makka! Tumeiangamiza miji iliyo jirani zenu. Na Sisi tuliwawekea wazi dalili namna mbali mbali, ili wapate kurejea waache ukafiri. Hawakurejea.
Rudi kwenye sura

* 28. Basi kwani hao walio wafanya miungu badala ya Mwenyezi Mungu ili iwakaribishe kwa Mwenyezi Mtukufu imeweza kuwakinga na maangamizo? Hasha! Bali miungu hiyo iliwakimbia, na hali wao ndio wana haja nayo mno iwanusuru. Na hayo yaliyo wafika, ya kutupwa na miungu yao, na kuwapotea ndio matokeo ya uwongo wao na uzushi wao.
Rudi kwenye sura

* 29. Ewe Muhammad! Taja tulipo kuletea kikundi cha majini waje sikiliza Qur'ani. Walipo hudhiria ilipo kuwa ikisomwa, baadhi yao wakawaambia wenzao: Sikilizeni! Ilipo kwisha timia kusomwa wakarudi kwa haraka kwa wenzao, kuwahadharisha na ukafiri, wakiwataka waamini.
Rudi kwenye sura

* 30. Walisema: Enyi watu wetu! Hakika sisi tumekisikia Kitabu chenye shani kubwa. Kimeteremshwa baada ya Musa, na kinasadikisha Vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyo tangulia, kinaongoza kwenye itikadi ya haki, na sharia ya vitendo iliyo simama sawa.
Rudi kwenye sura

* 31. Enyi watu wetu! Muitikieni mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu anaye ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na msadikini Mwenyezi Mungu akusameheni madhambi yenu yaliyo tangulia, na akulindeni na adhabu kali iliyo chungu.
Rudi kwenye sura

* 32. Na asiye muitikia Mwenyezi Mungu basi hawezi kumshinda Mwenyezi Mungu asimtie mkononi hata akikimbia vipi katika ardhi. Na wala hana isipo kuwa Mwenyezi Mungu wa kumnusuru na kumkinga na adhabu yake. Hao wanao puuza wasimwitikie mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu wamo katika ubabaishi na dhaahiri wako mbali na Haki.
Rudi kwenye sura

* 33. Wameghafilika wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi, na wala hakushindwa kuziumba, ni Muweza wa kuwafufua maiti? Bali Yeye ni Muweza wa hayo, kwani Yeye Mtukufu ana uweza kaamili juu ya kila kitu.
Rudi kwenye sura

* 34. Na siku watakapo simamishwa walio kufuru Motoni wataambiwa kwa kukemewa: Adhabu hii si jambo la kweli linakubaliana na tuliyo kuonyeni nayo duniani? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, haya ni haki kweli. Atasema: Onjeni kila namna ya adhabu kali kwa kushikilia kwenu ukafiri na ukanushi.
Rudi kwenye sura

* 35. Ewe Muhammad! Wastahamilie makafiri kama walivyo stahamili Mitume wengine wenye nguvu na imara wakati wa shida. Wala usiwahimizie adhabu. Kwani hiyo itawafika tu, hapana hivi wala hivi, hata ikichukua muda mrefu. Siku watapo kiona kitisho chake watadhani kuwa hawakukaa kabla yake ila saa moja tu ya mchana. Haya uliyo watolea waadhi yatosha. Hawataangamizwa kwa adhabu isipo kuwa walio toka kwenye ut'iifu.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani