Al Mumtah'inah maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Mumtah'inah

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Msiwafanye maadui wangu na maadui wenu kuwa ni wenzenu mkiwapa mapenzi ya kweli, na hali wao wameyakataa yaliyo kujieni nyinyi ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu chake. Wamemtoa Mtume na wamekutoeni nyinyi kwenu kwenye majumba yenu, kwa sababu ya Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Mnapotoka makwenu kwenda pigana Jihadi katika Njia yangu na kutaka radhi yangu, basi msifanye urafiki na adui zangu, mkawapa mapenzi kisirisiri. Na Mimi nayajua vyema yote mnayo yaficha na mnayo dhihirisha. Na yeyote mwenye kumfanya adui wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiye rafiki yake basi ameikosea Njia Iliyo Nyooka.
Rudi kwenye sura

* 2. Wakikutana nanyi na wakakuwezeni, uadui wao kwenu unadhihiri, na wanakunyoosheeni mikono yao na ndimi zao kukudhuruni. Na wanatamani muwe makafiri kama wao.
Rudi kwenye sura

* 3. Hawatakufaeni kitu jamaa zenu wala watoto wenu mlio wafanya kuwa ni marafiki, na hali wao ni adui wa Mwenyezi Mungu na adui zenu. Katika Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atakutengeni mbali mbali. Atawatia maadui zake Motoni na marafiki zake Peponi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote myatendayo.
Rudi kwenye sura

* 4. Nyinyi mna kiigizo kizuri cha kukiiga katika Ibrahim na walio amini pamoja naye, pale walipo waambia watu wao: Hakika sisi tunajitenga nanyi, na tunajitenga na hiyo miungu ya uwongo mnayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Sisi tunakukataeni, na umekwisha dhihiri uadui na kuchukiana baina yetu na nyinyi. Hayo hayataondoka kabisa mpaka mumuamini Mwenyezi Mungu peke yake. Lakini kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Nitakutakia maghfira, na similiki kwa Mwenyezi Mungu kitu chochote - kauli hiyo si ya kufuatwa. Kwani hayo yalikuwa kabla hajajua huyo baba yake kashikilia kuwa adui wa Mwenyezi Mungu wala hageuki. Ilipo dhihiri kwake kuwa hakika huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu alijitenga naye. Enyi waumini! Semeni: Mola wetu Mlezi! Kwako Wewe ndio tunategemea, na kwako Wewe tunarejea, na kwako Wewe ndio mwisho wetu Akhera.
Rudi kwenye sura

* 5. Mola wetu Mlezi! Usitujaalie tukawa katika hali ya kuwa katika fitina za walio kufuru. Na tusamehe madhambi yetu, ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu usiye shindika, Mwenye hikima katika kutasarafu kwake.
Rudi kwenye sura

* 6. Enyi Waumini! Bila ya shaka katika Ibrahim na walio kuwa pamoja naye, kipo kiigizo kizuri kwenu kwa vile walivyo wafanyia uadui maadui wa Mwenyezi Mungu. Kiigizo hicho ni kwa mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kupuuza kufuata haya basi kajidhulumu nafsi yake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa mwenginewe. Yeye ni Mwenye kustahiki peke yake sifa zote njema.
Rudi kwenye sura

* 7. Asaa Mwenyezi Mungu akajaalia yawepo mapenzi baina yenu na hao makafiri walio ni maadui zenu, kwa kuwapa tawfiki, kuwawezesha, kuingia katika Imani. Na Mwenyezi Mungu ana uweza ulio timia, ni Mkunjufu wa maghfira kwa mwenye kutubu, ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
Rudi kwenye sura

* 8. Mwenyezi Mungu hakukatazini kwa makafiri wasio kupigeni vita wala kukufukuzeni makwenu kuwakirimu na kuwapa mawasiliano mema. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda watu watendao ihsani na mawasiliano.
Rudi kwenye sura

* 9. Ila Mwenyezi Mungu anakukatazeni wale walio kupigeni vita katika Dini ili kukuzuieni nayo, na wakakulazimisheni kutoka majumbani kwenu na nchi yenu, na wakasaidia katika kukutoeni huko, msiwafanye hao kuwa ndio wenzenu wa kusaidiana nao. Na wenye kuwafanya hao ndio wasaidizi wao, basi hao ndio wenye kujidhulumu nafsi zao.
Rudi kwenye sura

* 10. Enyi mlio amini! Wakikujieni wanawake Waumini walio hama kukimbia nchi ya ukafiri, basi wachungueni ili mpate kujua ukweli wa Imani yao. Mwenyezi Mungu anajua zaidi ukweli wa Imani yao. Mkiwaona kama ni Waumini, basi msiwarudishe kwa waume zao makafiri. Wanawake Waumini si halali kwa makafiri, wala wanaume makafiri si halali kwa wanawake Waumini. Na wapeni waume wa kikafiri mahari waliyo yatoa kwa wake zao walio hamia kwenu. Wala hapana ubaya kwenu kuwaoa wanawake hao walio hamia kwenu mkiwapa mahari yao. Wala msiwazuie kwa kifungo cha ndoa wanawake makafiri walio bakia katika mji wa ukafiri au walio fungamana nao. Na takeni kwa makafiri mahari mliyo yatoa kwa wenye kufungamana na mji wa ukafiri. Na wao hao watake kulipwa walicho toa kuwapa wake zao walio hama wakaja kwenu. Hukumu hiyo ni kwa mujibu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, anayo kufafanulieni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema maslaha ya waja wake, ni Mwenye hikima katika kutoa sharia.
Rudi kwenye sura

* 11. Na wakitokea baadhi ya wake zenu wakakukimbieni kwenda kwa makafiri, kisha mkapigana nao vita, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha mahari waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
Rudi kwenye sura

* 12. Ewe Nabii! Wakikujia wanawake Waumini kukuahidi kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatwauwa watoto wao, wala hawatawabandikiza waume zao watoto wao (wa haramu) kwa uzushi na uwongo wanao uzua baina ya mikono yao na miguu yao. (yaani matumboni mwao, au kwa ndimi zao na tupu zao); wala hawendi kinyume nawe katika jambo jema unalo waitia, basi pokea ahadi zao juu ya hayo, na waombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na kurehemu. (Mtume s.a.w. haamrishi ila jema, lakini sharia hapo inasema kuwa mtawala yeyote hut'iiwa akiamrisha jema tu. Ama kwa lilio ovu, Mtume s.a.w. amesema: "Hapana kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.")
Rudi kwenye sura

* 13. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake, msiwafanye kuwa rafiki zenu watu ambao Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia. Hao wamekata tamaa na Akhera na yote yatakao kuwapo huko, ya kulipwa na kuhisabiwa, kama makafiri walivyo kata tamaa kufufuliwa waliomo makaburini.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani