Al Jumua' maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Jumua'

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi vinamsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa laiki, Yeye ndiye Mfalme wa kila kitu, Mwenye kuendesha atakavyo bila ya mpinzani, Mwenye kutakasika kwa ukamilifu na kila cha upungufu, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya kufika mwisho.
Rudi kwenye sura

* 2. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mtuma Mtume kwa watu wasio jua kuandika, naye ni katika wao wenyewe, anawasomea Aya zake Mwenyezi Mungu, na anawasafisha na mambo machafu ya itikadi na tabia, na anawafundisha Qur'ani na kuijua Dini. Na wao kabla ya kuletwa yeye walikuwa wamepotoka kabisa kuiacha haki.
Rudi kwenye sura

* 3. Na pia Mwenyezi Mungu amempeleka Muhammad kwa watu wenginewe, ambao hawajaja bado, lakini watakuja. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya kufikia ukomo katika vitendo vyake.
Rudi kwenye sura

* 4. Kuletwa Mtume huko ni fadhila inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Anamkirimu kwayo aliye mkhitari katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu peke yake, ndiye Mwenye fadhila kubwa.
Rudi kwenye sura

* 5. Mfano wa Mayahudi walio funzwa Taurati, na wakalazimishwa waifuate, na wao hawakuifuata kwa vitendo, ni mfano wa punda aliye beba vitabu ambavyo hajui ndani yake mna nini. Ni mbaya mno mfano wa watu wanao kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hawasaidii kufikilia uwongofu watu ambao kazi yao ni kudhulumu.
Rudi kwenye sura

* 6. Ewe Muhammad! Sema: Enyi nyinyi mlio Mayahudi! Kama mnadai kwa uwongo kwamba nyinyi peke yenu ati ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, basi takeni mauti kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika hayo madai ya kwamba Mwenyezi Mungu anakupendeni.
Rudi kwenye sura

* 7. Mwenyezi Mungu anasema: Wala Mayahudi hawatamani mauti milele kwa sababu ya ukafiri na vitendo viovu walio kwisha vitenda. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema walio dhulumu.
Rudi kwenye sura

* 8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia hamwezi kuyakimbia, bila ya shaka yatakukuteni tu. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kujua ya siri na ya dhaahiri. Na Yeye atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Rudi kwenye sura

* 9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, basi nendeni kwa hima na hamu kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo mliyo amrishwa yana nafuu zaidi kwenu nyinyi, ikiwa mnajua.
Rudi kwenye sura

* 10. Mkisha maliza kusali basi tawanyikeni katika nchi kwa ajili ya maslaha yenu, na mtake fadhila za Mwenyezi Mungu. Na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenu na ndimi zenu kwa wingi, ili asaa mkafuzu katika kheri za duniani na Akhera.
Rudi kwenye sura

* 11. Na wakiona bidhaa za biashara, au pumbao lolote hutawanyika kuendea hayo, na wakakuacha wewe umesimama unakhutubu! Waambie: Fadhila na thawabu zilioko kwa Mwenyezi Mungu zina nafuu zaidi kwenu kuliko pumbao na kuliko biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao toa riziki. Basi itafuteni riziki yake kwa kumt'ii Yeye.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani