Al Munaafiqun maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul Munaafiqun

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Ewe Muhammad! Wanapo kujia wanaafiki, wanasema kwa ndimi zao: Tunashuhudia kuwa hakika wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kwamba wewe ni Mtume wake; na Mwenyezi Mungu anashuhudia kwamba wanaafiki hapana shaka ni waongo katika kujidai kwao wanaamini, kwani hawasadiki katika nyoyo zao.
Rudi kwenye sura

* 2. Wamezifanya yamini zao za uwongo ni kinga, au ngao za kujikingia ili wasichukuliwe kuwa ni makafiri. Basi wakajizuia wenyewe wasiishike Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka. Hakika ni mabaya mno hayo wanayo yatenda ya unaafiki na kujitia imani ya uwongo.
Rudi kwenye sura

* 3. Hayo waliyo yafanya ndiyo mazoea ya kudhihirisha yasiyo ya kweli, na kuapa yamini za uwongo, kwa sababu hao wameamini kwa ndimi zao, kisha wakakufuru katika nyoyo zao, basi nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa ukafiri huu. Hao hawafahamu yepi ya kuwaokoa na adhabu za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 4. Na ukiwaona miili yao inakupendeza kwa uzuri wao, na wakizungumza unavutika kuwasikiliza kwa utamu wa maneno yao. Kumbe wao juu ya yote hayo nyoyo zao zitupu, hazina Imani ndani yake. Kama magogo yaliyo egemezwa, hayana uhai wowote. Wao hudhania kila linalo zuka basi linawalenga wao, kwa sababu wanaitambua hali yao ya unaafiki. Hao ndio maadui, basi tahadhari nao. Mwenyezi Mungu kesha wafukuza kwenye rehema yake. Vipi wanavyo iacha Haki wakauendea unaafiki wanao ushikilia?
Rudi kwenye sura

* 5. Na wakiambiwa: Jongeeni, apate Mtume wa Mwenyezi Mungu kukuombeeni msamaha, hutikisa vichwa vyao kwa kejeli, na utawaona wanageuka kwa kiburi hawataki kut'ii.
Rudi kwenye sura

* 6. Ni sawa kwa hawa wanaafiki, ukiwaombea msamaha, au ukito waombea. Kwa sababu hao hawauachi unaafiki wao. Basi Mwenyezi Mungu hatawasamehe kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi kuwapeleka kwenye Haki wale wanao kataa kufuata amri yake na kumuamini.
Rudi kwenye sura

* 7. Hao wanaafiki ndio wanao waambia watu wa Madina: Msitoe chochote kuwapa hao Waumini walio na Mtume wa Mwenyezi Mungu ili wapate kumwacha! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina zote za mbinguni na duniani, na riziki zote ziliomo humo. Lakini wanaafiki hawajui hayo.
Rudi kwenye sura

* 8. Wanaafiki wanasema kwa kutoa ahadi: Tukirejea Madina hapana shaka kikundi chetu, ambacho ndicho chenye nguvu zaidi, kitakitoa kikundi cha Waumini ambao ni wanyonge! Nguvu anazo Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini; sio hawa wanao jitia kuahidi. Lakini wanaafiki hawajui kitu.
Rudi kwenye sura

* 9. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Yasikuhangaisheni mali yenu, na watoto wenu, hata mkaacha kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kutekekeleza aliyo kuamrisheni kuyafanya. Na wenye kushughulishwa na mali zao na watoto wao wakaacha hayo, basi hao ndio watao kuwa wamekhasiri Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye sura

* 10. Enyi Waumini! Toeni katika mali tuliyo kuruzukuni upesi upesi kabla mmoja wenu hayajamfikia mauti akasema kwa majuto: Ewe Mola wangu Mlezi! Hebu hunipi muhula kidogo, nikapata kutoa sadaka, na nikawa miongoni wa watu wema watendao vitendo vyema?
Rudi kwenye sura

* 11. Wala Mwenyezi Mungu hampi muhula mtu yeyote ukisha fika wakati wake wa kufa. Na Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa kujua yote myatendayo, na Yeye atakulipeni kwa hayo.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani