At taghaabun maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suuratul At taghaabun

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa laiki na utukufu wake. Yeye ndiye peke yake Mwenye ufalme ulio timia, na Mwenye sifa njema, na ndiye Mwenye uweza ulio timia juu ya kila kitu.
Rudi kwenye sura

* 2. Yeye peke yake ndiye aliye kuumbeni mlipo kuwa si chochote. Basi kati yenu yupo anaye kanya Ungu wake, na miongoni mwenu yupo anaye sadiki. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda, na atakulipeni kwa mujibu wa vitendo vyenu.
Rudi kwenye sura

* 3. Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa hikima isiyo na ukomo, na akakuumbeni kwa sura, na akazifanya nzuri sura zenu, kwa kuwa amewafanya wanaadamu ndio viumbe walio nyooka vizuri. Na kwake Yeye ndiyo marejeo Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye sura

* 4. Yeye Mwenyezi Mungu anajua yote yaliomo katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha, na mnayo yaeneza, ikiwa maneno au vitendo. Na Mwenyezi Mungu ametimia ujuzi wake kwa mnayo dhamiria katika nyoyo zenu.
Rudi kwenye sura

* 5. Zimekwisha wafikieni khabari za walio kufuru kabla yenu, na wao wakameza ubaya wa matokeo wa mambo yao katika dunia. Na Akhera watapata adhabu yenye machungu makali.
Rudi kwenye sura

* 6. Masaibu hayo yaliyo wapata ni kwa sababu Mitume wao waliwajia na miujiza iliyo dhaahiri, nao wakasema kwa kukanya: Ati atujie mtu kama sisi kutuongoza? Wakakanya kuwa watafufuliwa. Wakaiacha Haki. Mwenyezi Mungu akadhihirisha kuwa hana haja na imani yao kwa kuwaangamiza. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ukwasi wake (kujitosha kwake), si Mwenye kuwa na haja na viumbe vyake. Ni Mwenye kustahiki kusifiwa na kuhimidiwa kwa uzuri wa neema zake.
Rudi kwenye sura

* 7. Makafiri wamedai kwa uwongo kwamba hawatafufuliwa baada ya kufa kwao. Ewe Muhammad! Waambie: Mambo sio kama mnavyo dai nyinyi. Ninaapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka yoyote nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa kwenu, na hapana shaka yoyote kuwa mtaambiwa mliyo yatenda duniani. Kisha mtalipwa kwayo. Na huko kufufuliwa, na kuhisabiwa, na kulipwa, ni jambo sahali na jepesi kabisa kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 8. Basi msadikini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ongokeni kwa kuifuata Nuru tuliyo mteremshia hata akakufahamisheni kwa uwazi kuwa kufufuliwa kunakuja bila ya shaka yoyote. Na Mwenyezi Mungu ana ujuzi wa kutumia kwa yote yanayo tokana nanyi.
Rudi kwenye sura

* 9. Siku atapo kukusanyeni katika Siku ya Mkusanyo wa walio tangulia mwanzo na walio kuja mwisho, akulipeni kwa vitendo vyenu! Siku hiyo ndiyo Siku ya Taghaabun, Kupunjana, kutapo dhihiri kupunjika kwa makafiri kwa kuacha Imani, na kupunjika Waumini kwa kupuuza kuongeza ut'iifu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema atamwondolea maovu yake, na atamtia katika Bustani zenye kupita kati yake mito, wakae humo milele. Malipo hayo ndio kufuzu kukubwa.
Rudi kwenye sura

* 10. Na walio ikataa Imani, na wakaikanusha miujiza yetu tuliyo wapa Mitume wetu kuwaunga mkono, hao ndio watu wa Motoni. Watadumu humo. Na marudio maovu ni hayo walio yarudia hao.
Rudi kwenye sura

* 11. Mja hasibiwi na balaa ila kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumsadiki Mwenyezi Mungu basi humwongoa moyo wake kwendea katika yanayo mpendeza. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ujuzi wake.
Rudi kwenye sura

* 12. Na mt'iini Mwenyezi Mungu kwa aliyo kuamrisheni, na mt'iini Mtume kwa Ujumbe aliyo kufikishieni kutoka kwa Mola wake Mlezi. Mkiupuuza ut'iifu huu, basi Yeye hadhuriki kitu kwa mapuuza yenu. Na hakika Mtume wetu hana jukumu juu yake ila kufikisha Utume wake tu kwa uwazi.
Rudi kwenye sura

* 13. Mwenyezi Mungu, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye tu peke yake. Basi Waumini nawamtegemee Yeye tu katika mambo yao yote.
Rudi kwenye sura

* 14. Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu, ambao wanakuzuilieni msimt'ii Mwenyezi Mungu kwa kutaka kuwatimizia hao matakwa yao. Basi kuweni na hadhari nao. Na mkiweza kuyavuka makosa yao yanayo kubalika kusameheka, na mkayapuuza, na mkawafichia, basi Mwenyezi Mungu naye atakughufirieni nyinyi. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Rudi kwenye sura

* 15. Hakika mali yenu na watoto wenu ni majaribio na mtihani. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa kwa anaye pendelea kumt'ii Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye sura

* 16. Basi tumieni juhudi zenu na nguvu zenu katika kumcha Mwenyezi Mungu. Na sikieni mawaidha yake, na t'iini amri zake, na toeni katika alicho kuruzukuni kwa ajili ya hicho alicho amrisha kitolewe kwa ajili yake. Na tendeni kheri kwa sababu ya nafsi zenu. Na mwenye kuzuiliwa na Mwenyezi Mungu ubakhili na uchoyo wa roho yake, basi watu kama hao ndio walio jaaliwa kupata kila kheri.
Rudi kwenye sura

* 17. Mkitoa katika mambo ya kheri kutoa kwa moyo safi, basi Mwenyezi Mungu atazidisha mardufu thawabu za mlicho toa, na atakusameheni madhambi yenu yaliyo kuponyokeni. Na Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa shukrani, na kuwalipa watendao mema, na ni Mpole, hafanyi haraka kuwaadhibu wanao muasi.
Rudi kwenye sura

* 18. Yeye ni Mjuzi wa vilivyo fichikana na vinavyo onekana, Mwenye nguvu, Mtenda nguvu, Mwenye hikima katika mipango ya viumbe vyake, Mwenye kuweka kila kitu kwa pahala pake.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani