Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili
26.Suurat Shu'araa

Imeshuka Makka Ina aya 227
Utangulizi Sura Nyingine Faharasa


KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0



1. T'aa Siin Miim. (T'.S.M.) 1



2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. 2



3. Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini. 3



4. Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao. 4



5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao. 5



6. Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. 6



7. Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri? 7



8. Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. 8



9. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 9



10. Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu, 10



11. Watu wa Firauni. Hawaogopi? 11



12. Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe. 12



13. Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun. 13



14. Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa. 14



15. Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. 15



16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 16



17. Waachilie Wana wa Israili wende nasi. 17



18. (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? 18



19. Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? 19



20. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. 20



21. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. 21



22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili? 22



23. Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote? 23



24. Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini. 24



25. (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi? 25



26. (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza. 26



27. (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu. 27


1
28. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini. 28



29. (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani. 29



30. Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? 30



31. Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. 31



32. Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. 32



33. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. 33



34. (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. 34



35. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? 35



36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. 36



37. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. 37



38. Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu. 38



39. Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika? 39



40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda. 40



41. Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda? 41



42. Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele. 42



43. Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa. 43



44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda. 44



45. Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua. 45



46. Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. 46



47. Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote. 47



48. Mola Mlezi wa Musa na Harun. 48



49. (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote. 49



50. Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. 50



51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini. 51



52. Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. 52



53. Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. 53



54. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. 54



55. Nao wanatuudhi. 55



56. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari. 56



57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, 57



58. Na makhazina, na vyeo vya hishima, 58



59. Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili. 59



60. Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. 60



61. Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! 61



62. (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! 62



63. Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. 63



64. Na tukawajongeza hapo wale wengine. 64



65. Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. 65



66. Kisha tukawazamisha hao wengine. 66



67. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. 67



68. Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 68



69. Na wasomee khabari za Ibrahim. 69



70. Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini? 70



71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. 71



72. Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? 72



73. Au yanakufaeni, au yanakudhuruni? 73



74. Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo. 74



75. Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- 75



76. Nyinyi na baba zenu wa zamani? 76



77. Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 77



78. Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, 78



79. Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. 79



80. Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. 80



81. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. 81



82. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. 82



83. Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. 83



84. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. 84



85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. 85



86. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu. 86



87. Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa. 87



88. Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana. 88



89. Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi. 89



90. Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu. 90



91. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. 91



92. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu 92



93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? 93



94. Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu, 94



95. Na majeshi ya Ibilisi yote. 95



96. Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo: 96



97. Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri, 97



98. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. 98



99. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. 99



100. Basi hatuna waombezi. 100



101. Wala rafiki wa dhati. 101



102. Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini. 102



103. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. 103



104. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 104



105. Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume. 105



106. Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu? 106



107. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 107



108. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 108



109. Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 109



110. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 110



111. Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini? 111



112. Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya? 112



126. Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua! 113



114. Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. 114



115. Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri. 115



116. Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. 116



117. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. 117



118. Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini. 118



119. Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni. 119



120. Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia. 120



121. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 121



122. Kina A'd waliwakanusha Mitume. 122



123. Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? 123



124. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 124



125. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 125



126. Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 126



127. Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? 127



128. Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! 128



129. Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. 129



130. Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. 130



131. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. 131



132. Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. 132



133. Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. 133



134. Na mabustani na chemchem. 134



135. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. 135



136. Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha. 136



137. Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani. 137



138. Wala sisi hatutaadhibiwa. 138



139. Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 139



140. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 140



141. Kina Thamud waliwakanusha Mitume. 141



142. Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu? 142



143. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 143



144. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. 144



145. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 145



146. Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? 146



147. Katika mabustani, na chemchem? 147



148. Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. 148



149. Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. 149



150. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 150



151. Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka, 151



152. Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi. 152



153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa. 153



154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. 154



155. Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu. 155



156. Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa. 156



157. Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta. 157



158. Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 158



159. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 159



160. Watu wa Lut'i waliwakanusha Mitume. 160



161. Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu? 161



162. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu. 162



163. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. 163



164. Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 164



165. Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? 165



166. Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka! 166



167. Wakasema: Ewe Lut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji! 167



168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu. 168



169. Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo. 169



170. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote, 170



171. Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma. 171



172. Kisha tukawaangamiza wale wengine. 172



173. Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa. 173



174. Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 174



175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. 175



176. Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume. 176



177. Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu? 177



178. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 178



179. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 179



180. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 180



181. Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja. 181



182. Na pimeni kwa haki iliyo nyooka; 182



183. Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi. 183



184. Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia. 184



185. Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa. 185



186. Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo. 186



187. Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. 187



188. Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda. 188



189. Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa. 189



190. Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 190



191. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 191



192. Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 192



193. Ameuteremsha Roho muaminifu, 193



194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji, 194



195. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi. 195



196. Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. 196



197. Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili? 197



198. Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu, 198



199. Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini. 1990



200. Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu. 200



201. Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. 201



202. Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari. 202



203. Na watasema: Je, tutapewa muhula? 203



204. Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu? 204



205. Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka, 205



206. Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa, 206



207. Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa? 207



208. Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji 208



209. Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu. 209



210. Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, 10



211. Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi. 11



212. Hakika hao wametengwa na kusikia. 12



213. Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa. 13



214. Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe. 14



215. Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini. 15



216. Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda. 16



217. Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 17



218. Ambaye anakuona unapo simama, 18



219. Na mageuko yako kati ya wanao sujudu. 19



220. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. 20



221. Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani? 21



222. Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi. 22



223. Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo. 23



224. Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. 24



225. Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde? 25



226. Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? 26



227. Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka. 27


Sura Nyingine Faharasa

Chagua Sura Nyingine:

Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com 
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani