42.Suuratul Ash-shuura |
Imeshuka Makka | Ina aya 53 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. H'a Mim
1
2. A'yn Sin Qaf
2
3. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima anavyo
kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.
3
4. Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi. Na Yeye ndiye
Mtukufu, Mkuu.
4
5. Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola
wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
5
6. Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi
Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
6
7. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu
wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano,
haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
7
8. Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja, lakini
anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana mlinzi
wala msaidizi.
8
9. Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu
ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza
wa kila kitu.
9
10. Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko
kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye
mtegemea na kwake Yeye narejea.
10
11. Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume
katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna
hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
11
12. Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki
amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu.
12
13. Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia
wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala
msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi
Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
13
14. Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda
iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola
wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli
hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia
shaka inayo wahangaisha.
14
15. Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa,
wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi
Mungu katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi
Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo
vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu
na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
15
16. Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja
za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na
itakuwa kwao adhabu kali.
16
17. Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa Haki, na Mizani.
Na nini kitakacho kujuulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama ipo karibu?
17
18. Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanao amini
wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao
wanao bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.
18
19. Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku ampendaye. Naye
ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
19
20. Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika mavuno yake,
na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini katika Akhera
hana fungu.
20
21. Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo itolea
idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua basi wangeli
katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu.
21
22. Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya waliyo
yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo
katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi.
Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
22
23. Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini
na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika
kujikurubisha. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani.
23
24. Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu
akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu
na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliomo vifuani.
24
25. Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa,
na anayajua mnayo yatenda.
25
26. Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na anawazidishia
fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu.
26
27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki waja wake,
basi bila ya shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini anaiteremsha
kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
27
28. Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kwisha kata tamaa,
na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa.
28
29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama alio
waeneza. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.
29
30. Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono
yenu. Naye anasamehe mengi.
30
31. Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna
mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu.
31
32. Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini
kama vilima.
32
33. Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu
ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
33
34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo yatenda hao
watu. Naye husamehe mengi.
34
35. Na ili wajue wanao jadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana
pahala pa kukimbilia.
35
36. Basi vyote mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini
kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio
amini, na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi,
36
37. Na wanayo yaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapo
kasirika wao husamehe,
37
38. Na wanao mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo
yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulicho waruzuku
wakawa wanatoa,
38
39. Na ambao wanapo fanyiwa jeuri hujitetea.
39
40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe,
na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Yeye hawapendi wenye kudhulumu.
40
41. Na wanao jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.
41
42. Bali lawama ipo kwa wale wanao wadhulumu watu, na wanafanya jeuri
katika nchi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
42
43. Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya
kuazimiwa.
43
44. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana mlinzi baada
yake. Na utawaona wenye kudhulumu watakapo iona adhabu wanasema: Je! Ipo
njia ya kurudi?
44
45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge,
wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika wapatao
khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama
hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima.
45
46. Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
46
47. Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo epukika
itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala hamtakuwa
na cha kukingia.
47
48. Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao.
Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema
kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyo yatanguliza
mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
48
49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo,
anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa
kiume,
49
50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa.
Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.
50
51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila
kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia
ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
51
52. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui
Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo
tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye
Njia Iliyo Nyooka.
52
53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni
na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.
53
Sura Nyingine | Faharasa |