UTANGULIZI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU


Sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani zimshukie aliye khitimisha Mitume wote, Bwana wetu Muhammad, na Aali zake, na Masahaba wake, na walio wafuata.
Ama baada:
Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyo mteremkia Muhammad s.a.w. kwa ajili ya kupambana na kushinda kuwa ni muujiza wa kiibada kwa kusomewa sisi kwa kupokewa, yaliyo kusanywa baina jalada mbili tangu Sura ya Al-Fatiha (Al- hamdu) mpaka Sura ya Annas (Qul Audhubi Rabbi nnas). Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwa Mtume wake wa mwisho ili iwe ni Kitabu cha mwisho kuwateremkia watu wote, chenye kukusanya yaliyo na kheri kwa wanaadamu na maslaha ya hali zao za sasa na za baadaye, za dunia yao na Akhera yao, ikiteremka kwa mapande mbali mbali, kwa Aya na Sura kwa mujibu wa haja ya mambo yanavyo tokea katika muda wa miaka ishirini na tatu katika maisha ya Mtume s.a.w. Baadhi yake hii Qur'ani iliteremka kabla ya kuhama kwake kutoka Makka kwenda Madina, na baadhi yake nyengine ni baada ya kuhama kwake. Na Aya na Sura za Makka zilizo shuka Makka aghlabu yake zinakusanya misingi ya itikadi za Imani ya Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho. Kisha zikateremka Aya na Sura za Madina. Na hizo zinakusanya mambo ya ibada, na mambo ya matawi, na hukumu za Sharia.
Ndani yake zimo khabari za kabla yetu na khabari za baada yetu, na hukumu za baina yetu sisi. Zimo khabari za umma walio kuwepo kabla yetu na karne zilizo kwisha pita, ndani yake zimo hadithi za Manabii na Mitume, na mataifa na makundi na watu, na vituko, na mambo, na nyendo za taarikhi (historia) za jamii za kibinaadamu zenye mazingatio kwa mwenye kuzingatia, na mawaidha kwa mwenye moyo au mwenye kutega sikio naye anaona, na zinatamka kwa mtindo wake Mwenyezi Mungu ambao hawendi kinyume katika kuwateketeza wapotovu walio dhulumu, na kuwaokoa waongofu walio kwenda sawa. Na kwamba dunia ya watu, na hata ikipitiwa na miaka mingi na dahari haiwezi kusilihi bila ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na kwamba kwa hakika wanaadamu, vyo vyote vile walivyo, hawawezi kufikilia mafanikio wanayo yatafuta ila wakiongozwa na uwongofu wa Mwenyezi Mungu na Ujumbe wake.
Na katika hiyo Qur'ani zipo hukumu za kutatua matatizo yaliyo baina yetu, na masuala ambayo yanahitajia kubainishwa na kuwekwa sawa katika mambo ya itikadi na mambo ya fikra, na masuala ya akhlaki, na mwenendo, na maingiliano katika yaliyo khusu fedha, na mambo ya ibada, na hukumu za baina ya watu binafsi na zisio kuwa binafsi. "Enyi watu! Hakika umekufikieni uthibitisho kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na tumekuteremshieni nuru iliyo dhaahiri."
"Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho eleza kila kitu, na ambacho ni uwongofu na rehema, na bishara kwa Waislamu."
Hapana hukumu ya Sharia ya Dini au hukumu au tatizo lolote lilio gusana na dunia ya watu na maisha yao, au linazama katika maisha hayo ila utayakuta yote hayo katika Qur'ani kama mshipa unao pwita, au chemchem isiyo kauka. Na utakuta humo uwongofu, na ufafanuzi na uwongozi ama moja kwa moja kwa uwazi, au kwa makisio."Bila ya shaka imekwisha kujieni nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinacho bainisha, ambacho kwacho Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka." Naam, hakika bila ya shaka yoyote hii Qur'ani tukufu ni mwenge wa uwongofu ulioko njiani kuwaongoza wanaadamu wote, na kuwatoa kwenye giza kuwapeleka kwenye nuru, na kuwashika mkono kuwasogeza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na hapo ndipo pahala pa kuondokea katika taarikhi yake ndefu, kubadilika katika uhai wake wa madhambi na uharibifu na upotovu kuendea maisha ya kheri na Haki na uwongofu, na ndio yakatokea katika ulimwengu wote ya vipimo na kufahamu vyema na mazingatio yaliyo mnyanyua mwanaadamu kutoka kiwango cha chini kabisa na kumfikisha katika cheo cha juu cha kuzagaa na kukamilika. Uwongofu na maana ziliomo ndani ya Qur'ani ambazo zilizo tangulia kuashiriwa haziwezi kujuulikana ila kwa kufasiriwa, yaani kuelezwa ile matini ya Qur'ani yenyewe na Aya zake. Na Tafsiri ni kuweka wazi makusudio ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ujuzi wa makusudio haya kwa maneno yake katika hii Qur'ani ni kwa kiasi ya uwezo wa kibinaadamu. Na ilimu ya Tafsiri ilianza kidogo kidogo, na ikakua kidogo kidogo mpaka ukakamilika muda wake, na ikafikilia kiwango cha kukua kwake. Ikawa hiyo Ilimu ya Tafsiri katika sura ya kushangaza tuijuavyo hii leo. Kwani katika zama za Mtume s.a.w. haikuwapo haja kubwa ya kuipanga Tafsiri, wala kuitunga Ilimu ya Tafsiri, kwa sababu Qur'ani kwa jumla yake ilikuwa iwazi na ikifahamika kwa Mtume s.a.w. na Masahaba zake. Na juu ya hivyo mwenyewe Nabii s.a.w. alikuwa akitoa tafsiri za baadhi ya Aya na maneno ambayo huenda yalikuwa yakifichikana makusudio yake. Na Masahaba nao na Taabii'na, walio wafuata, na walio wafuatia baada yao kadhaalika walikuwa pia na Tafsiri zao zilizo kuwa zinakhitalifiana maoni yake, na ambazo zikileta majadiliano kwa sababu kadhaa au kadhaa ambazo haziachi kutokea katika umma mchanga mwanzoni unapo chipuka kukomboka, na ukaingia katika misukosuko ya taarikhi, na majadiliano ya kimadhehebu, na khitilafu za fiqhi na siyasa.
Qur'ani, basi, haikuacha kuwa, na mpaka sasa ingali kuwa ndiyo ya kati katika utamaduni wa Kiislamu, na harakati za fikra na mambo yote ya kiakili, na hizo Aya zake zimehimiza watu waziangalie na wazizingatie. Kwani amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na hiki Kitabu, tumekiteremsha kwako kimebarikiwa, ili wapate kuzizingatia Aya zake, na wenye akili wawaidhike." Na akasema: "Hawaizingatii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi." Na pia akasema: "Je! Hawaizingatii hii Qur,ani? Au kwenye nyoyo zao pana kufuli?" Na Tafsiri ya haya haiwezi kuwa natija yake ila ni kuwaza na kuzingatia, na maoni ya wenye kufasiri bila ya shaka yamekhitalifiana, na kadhalika njia zao na mbinu zao katika tafsiri. Miongoni mwao wapo walio pendelea makindano ya fikra za itikadi wakajitawanya vikubwa mno katika kuzichambua Aya zilizo khusikana na hayo, na tafsiri zao zikaonyesha kumili upande huo zaidi. Na wapo wengine walio vutika na migogoro ya lugha na ufasihi. Basi wakajitawanya vikubwa mno katika uwanja huo. Bado na wengine walio vutika na mizozano ya Fiqhi na Sharia, na wao wakajitawanya pia katika midani hiyo, na hali kadhaalika walio jitawanya katika masimulizi ya hadithi na khabari na walio jitawanya katika mambo ya akhlaki na tasawwufu na mawaidha na Ishara za Mwenyezi Mungu katika nafsi na katika viumbe na mfano wa hayo. Kadhaalika wapo wafasiri walio endelea kueleza kwa urefu mpaka wakachosha, na walio fupisha mpaka ikawa hawakueleza kitu. Na wapo walio kuwa wakati na kati, baina ya hawa na hao. Na wapo ambao walio mili kufuata tafsiri za kizamani zilizo pokewa, na wapo ambao wanao tumia maoni yao wenyewe. Wapo wenye mtindo wa kufasiri kwa njia za kubania bania zisio kuwa nyepesi kufahamika, na wako wanao andika kwa njia ya uwazi. Na wote, wa pande zote, wametuachia utajiri mkubwa wa ilimu, na mawazo ya akili yanayo pelekea mastaajabu na kuyathamini, na yapasa sifa kwa umma ulio tumikiwa Kitabu cha Mola wao Mlezi kwa mfano usio pata kutokea kwa kitabu chochote duniani, kwa kuhifadhiwa, na kudhibitiwa, na kuchambuliwa, na kuchujwa, na kutukuzwa, na kutakaswa kwa muda wa karne kumi na nne, zikifuatiwa na karne na karne nyengine mpaka Mwenyezi Mungu atapo irithi ardhi na vilio juu yake. "Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakao ulinda." "Na bila ya shaka hayo ni Kitabu chenye nguvu. Haitakikifia baat'ili mbele yake wala nyuma yake; kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa."
Fikra zinazuka mpya, na tamaduni mbali mbali zinatiana mimba, na maisha yanageuka, na kila siku mpya yanazuka mawazo mapya ya mwanaadamu. Kila zama zikiendelea mbele wanaadamu wanazidi kukaribiana na kuchanganyika, na njia za kuwasiliana na maendeleo zinasaidia hayo, kana kwamba wanataka kufasiri kwa kitendo kauli ya Qur'ani isemayo: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanmke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye khabari." Na kuyashikilia waliyo yasema watu wa mwanzo, bila ya kuleta lolote jipya au kuanzisha ni kuacha kuwa na maendeleo na kubakia nyuma. Na kuwa na uwezo juu ya mageuzo na kutafautisha baina ya kavu na nono, na mzozano wa kubakia, na kubakia linalo faa, ni alama ya uhai, na ndio akili ya maisha, na ndio mwenendo wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake. Na Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni bahari isiyo kuwa na ufukwe, wala kina chake hakitambulikani, wala ukubwa wake hauweleweki.
Huchoki kukichungua na kukizingatia, wala hukomi kukifikiri kwa kuendelea.

         Usowe wazidi kukupendeza
                   Kwa kila kipindi ukikyangaza
                   Uzuri jadidi wa kushangaza                

Haya ndiyo yaliyo fungua fursa kwa kila yanayo patikana katika Tafsiri na wenye kufasiri. Na haya ndiyo yaliyo ikabili Baraza Kuu ya Mambo ya Kiislamu (ya Misri) hata ikaunda halmashauri za ilimu za mabingwa wanazuoni wakubwa wakubwa, na wachunguzi wataalamu na watu wa fikra, ili washughulikie kutunga Tafsiri kwa njia za kisasa, nyepesi, iliyo kunjuka, yenye ibara wazi, mukhtasari, si tupu wala haichoshi, haina khitilafu za kimadhehebu, wala maneno maneno ya kifundi fundi ya kutatanisha, na kujaza jaza itikadi za maneno, ili iwe katika hali ya kusilihi kutarjumiwa katika lugha nyengine za kigeni, ambazo inatarajiwa wasemao lugha hizo wasome yaliomo katika Qur'ani hii na wafahamu itikadi na misingi, na mafunzo ya kuwaongoza, kutimiza waajibu ulio juu ya shingo zetu, sisi tunao sema lugha ya Kiarabu, nao ni kutarjumu maana ya Qur'ani kwa wasio kuwa Waarabu ili ipate kuwa sahali Ujumbe wa Muhammad kuwafikilia watu wote na wangakhitalifiana ndimi zao na rangi zao. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na hatukumpeleka Mtume yeyote isipo kuwa kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia." Ilivyo kuwa Ujumbe wa Mtume s.a.w. ni kwa watu wote, na yeye ni Mwaarabu mwenye kusema lugha ya Kiarabu basi hapana shaka Ujumbe wake lazima ufike kwa wasio kuwa Waarabu kwa njia ya tarjama itakayo chukua pahala pa asli, na kwa hii tarjama iliyo sawa na sahihi yenye kufuata uaminifu, iliyo simama juu ya kufahamu na kuelewa kwa huyo mwenye kutarjimu. Na huyo mtarjimu tunamfungia njia asiziendee tarjuma chungu nzima zilizo potolewa makusudi kwa kujazwa uharibifu na upotovu.
Na tafsiri fupi itakuja fuatwa karibu na tafsiri nyengine ya ukunjufu zaidi kidogo, yaani yenye kuzidi uchunguzi na uangalizi, na kuchambua ibara na ufasihi na mafunzo, na uwongozi wa kuwashika mkono Waislamu ili wazindukane na waendeshe maisha yao kwa mujibu kama waadhi huu wenye hikima unavyo wataka washike njia za kuwaletea nguvu, na utukufu na hishima. Na humo mnaashiriwa mambo yanayo ongozwa na Aya zake kwenye sharia za maisha, na siri za ulimwengu, na mambo yake ya ki-ilimu ambayo yalikuwa hayakuwa yakijuulikana ila katika zama hizi za mwisho kwa kuvumbuliwa na sayansi. Na hayumkini kuwa Qur'ani kuyaashiria mambo hayo hapo zamani ila kwa kuwa hayo si maneno ya mwanaadamu bali ni maneno ya Mwenyezi Mungu Muumbaji Mwenye Nguvu na Uweza, ambaye ameahidi kwa uwazi katika Kitabu hichi hichi: "Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwa Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?" Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwezesha.


HALMASHAURI YA QUR'ANI NA SUNNA.
Sura Faharasa
Soma Sura:

Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani