1.Surat Ibrahim |
Imeshuka Makka | Ina aya 52 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
0. KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU;
0
1. Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya
Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
1
2. Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote viliomo katika
mbingu na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali!
2
3. Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia
watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea
mbali.
3
4. Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia.
Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa amtakaye.
Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
4
5. Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu
wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi
Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
5
6. Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu
aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio
kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha
hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola
wenu Mlezi.
6
7. Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni;
na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
7
8. Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika
Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
8
9. Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu,
na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi
Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono
yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa,
na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
9
10. Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba
mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni
muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu
kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi
tuleteeni hoja ilio wazi.
10
11. Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu
kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja
wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
11
12. Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa
kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo
tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
12
13. Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi
yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi:
Hakika tutawaangamiza walio dhulumu.
13
14. Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anaye ogopa
kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu.
14
15. Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi.
15
16. Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji ya usaha.
16
17. Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia
kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine
kali vile vile.
17
18. Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama
jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi
kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali.
18
19. Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki?
Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya!
19
20. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.
20
21. Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia
walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo
hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli
tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika
au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
21
22. Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu
alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni.
Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia.
Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi
wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu
zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na
adhabu chungu.
22
23. Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani
yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio
yao humo yatakuwa: Salaam.
23
24. Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa neno zuri?
Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.
24
25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi.
Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
25
26. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya
ardhi. Hauna imara.
26
27. Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara
katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea
hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
27
28. Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa
kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
28
29. Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
29
30. Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze watu kwenye
Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
30
31. Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe katika
tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa
na biashara wala urafiki.
31
32. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akateremsha
maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na
akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na
akaifanya mito ikutumikieni.
32
33. Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na
akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.
33
34. Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi
Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye
kuzikufuru neema.
34
35. Na Ibrahim alipo sema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie mji huu
uwe wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.
35
36. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi
aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
36
37. Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu
katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola
wetu Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao,
na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru.
37
38. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha na tunayo
yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi
wala katika mbingu.
38
39. Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu aliye nipa juu
ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusikia
maombi.
39
40. Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika
dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu.
40
41. Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini,
siku ya kusimama hisabu.
41
42. Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo yafanya madhaalimu.
Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho yao.
42
43. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao
tupu.
43
44. Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme:
Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate
Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?
44
45. Na mkakaa katika maskani zile zile za walio zidhulumu nafsi zao.
Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi tukakupigieni mifano
mingi.
45
46. Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua
Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.
46
47. Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi
yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na ni Mwenye
kulipiza.
47
48. Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao
watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.
48
49. Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo;
49
50. Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao.
50
51. Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo yachuma.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
51
52. Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa
hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.
52
Sura Nyingine | Faharasa |