22.Suratul Hajj |
Imeshuka Madina | Ina aya 78 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya
Kiyama) ni jambo kuu.
1
2. Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye,
na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na
kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
2
3. Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu
bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi.
4. Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika
atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.
4
5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika
Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana
na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye
umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika
matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni
kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi
wanao kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge
kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi
imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka,
na kumea kila namna ya mimea mizuri.
5
6. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba
hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza
wa kila kitu.
6
7. Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na
kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.
7
8. Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya
ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
8
9. Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi
Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya
kuungua.
9
10. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako.
Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.
10
11. Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni.
Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake.
Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
11
12. Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala kumnufaisha.
Huko ndiko kupotolea mbali!
12
13. Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi
kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.
13
14. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema
katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.
14
15. Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika
dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila
yake itaondoa hayo yaliyo mkasirisha?
16
16. Na namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya zilizo wazi,
na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.16
17. Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo
na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina
yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
18
18. Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni
na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti,
na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na
anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi
Mungu hutenda apendayo.
18
19. Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi.
Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa
vyao maji yanayo chemka.
19
20. Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao
pia.
20
21. Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma.
21
22. Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa
humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua!
22
23. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema
katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo
ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri..
23
24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa kwenye Njia
ya Msifiwa.
24
25. Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu
na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa,
kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa
dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu.
25
26. Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia:
Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanao
izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanao
sujudu.
26
27. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia
aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.
27
28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu
katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika
hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.
28
29. Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na waizunguke
Nyumba ya Kale.
29
30. Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu
basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa
nyama hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu,
na jiepusheni na usemi wa uwongo.
30
31. Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha.
Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni,
kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
32. Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo
ni katika unyenyekevu wa nyoyo.
33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahala
pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.
34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada
ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika
wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake
tu, na wabashirie wanyenyekevu.
35. Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanao
vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika tulivyo
waruzuku.
36. Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo
kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi
Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika
hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya
hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
37. Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia
uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi
Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi
Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema.
39. Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa
- na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia .
40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa
wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa,
na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi
Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule
anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.
41. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na
wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi
Mungu ndio marejeo ya mambo yote.
41
42. Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu,
na kina A'ad na kina Thamud,
42
43. Na watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i
43
44. Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda makafiri,
kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu!
44
45. Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa imebaki
magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?
45
46. Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia,
au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo
pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.
46
47. Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda
kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni
kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi.
47
48. Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, na kisha
nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote.
48
49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye dhaahiri.
49
50. Basi walio amini na wakatenda mema watapata maghfira na riziki
za ukarimu.
50
51. Na wanao jitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.
51
52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anapo soma, Shet'ani
hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayo yatia
Shet'ani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi Mwenye hikima.
52
53. Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe ni fitna
kwa wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu.
Na hakika madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali.
54. Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola
wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu
ndiye anaye waongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka.
54
55. Na walio kufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa hilo mpaka
Saa iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa.
55
56. Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina
yao. Basi walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani zenye neema.
56
57. Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata
adhabu ya kufedhehesha.
57
58. Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au
wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku.
58
59. BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
59
60. Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha
akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira.
60
61. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana,
na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia Mwenye kuona.
61
62. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale
wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye
Juu na ndiye Mkubwa.
62
63. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni,
na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na Mwenye
kujua.
63
64. Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa.
64
65. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo
katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika
mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu.
65
66. Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni, na kisha atakufufueni.
Hakika mwanaadamu hana fadhila.
66
67. Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi wasizozane
nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika
wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka.
67
68. Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayo
yatenda.
68
69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo
mnayo khitalifiana.
69
70. Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na
katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu
ni mepesi.
70
71. Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia
ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu hawatakuwa na wa
kuwasaidia.
71
72. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso
za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu.
Sema: Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi
Mungu amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo.
72
73. Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao
waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika
kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika
kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.
73
74. Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa.
Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.
74
75. Mwenyezi Mungu huteuwa Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni
mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
75
76. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na kwa Mwenyezi
Mungu yatarejeshwa mambo yote.
76
77. Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi,
na tendeni mema, ili mfanikiwe.
77
78. Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki
jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika
Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni
Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi
juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni
Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora
kabisa, na Msaidizi bora kabisa.
78
Sura Nyingine | Faharasa |