27.Suuratun Naml |
Imeshuka Makka | Ina aya 93 |
Utangulizi | Sura Nyingine | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu kinacho bainisha;
1
2. Uwongofu na bishara kwa Waumini,
2
3. Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo.
3
4. Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao,
kwa hivyo wanatangatanga ovyo.
4
5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio
watapata khasara zaidi.
5
6. Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana kwake Mwenye
hikima Mwenye kujua.
6
7. (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto,
nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili
mpate kuota moto.
7
8. Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu
na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa
walimwengu wote.
8
9. Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
9
10. Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka
nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu
Mitume.
10
11. Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya,
basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
11
12. Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya
maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika
hao walikuwa watu waovu.
12
13. Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema:
Huu ni uchawi dhaahiri.
13
14. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi
zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!
14
15. Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu
Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha kuliko
wengi katika waja wake Waumini.
15
16. Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa
usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri.
16
17. Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na
ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.
17
18. Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu
chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni
Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua.
18
19. Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema:
Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi
na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema
yako katika waja wako wema.
19
20. Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud,
au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?
20
21. Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee
hoja ya kutosha.
21
22. Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo gundua
wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini.
22
23. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila
kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.
23
24. Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi
Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo
hawakuongoka
24
25. Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana
katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.
25
26. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi
tukufu..
26
27. Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni
mwa waongo.
27
28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame
watarejesha nini.
28
29. (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua tukufu.
29
30. Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa rehema, Mwenye kurehemu.
30
31. Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye
kusalimu amri.
31
32. Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu hili,
kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.
32
33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko
kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.
33
34. Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya
wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.
34
35. Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi
nayo wajumbe.
35
36. Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo
ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi
kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.
36
37. Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza
kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na
wanyonge.
37
38. Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea
kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.
38
39. Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka
pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.
39
40. Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa
jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika
fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru.
Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake;
na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.
40
41. Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka,
au atakuwa miongoni mwa wasio ongoka.
41
42. Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni
kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake wakasema):
Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu.
42
43. Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia.
Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.
43
44. Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona alidhani
ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema:
Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola
wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja
na Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
44
45. . Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Saleh kuwaambia: Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana.
45
46. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya
wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?
46
47. Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye
akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni
watu mnao jaribiwa.
47
48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala
hawafanyi la maslaha.
48
49. Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku
yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo
ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli.
49
50. Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na
wao hawatambui.
50
51. Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza
wao pamoja na watu wao wote.
51
52. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika
bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua.
52
53. Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu.
53
54. Na Lut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu nanyi mnaona?
54
55. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala ya wanawake?
Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa!
55
56. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Wafukuzeni wafwasi
wa Lut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi.
56
57. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe; tukamkadiria
katika walio baki nyuma.
57
58. Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua ya walio
kwisha onywa.
58
59. Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani
ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni bora, au wale
wanao washirikisha naye?
59
60. AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni
maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza?
Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu? Bali hao ni watu walio potoka.
60
61. Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia
ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili kiziwizi?
Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.
61
62. Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo mwomba, na akaiondoa
dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.
62
63. Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na bahari, na
akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu pamoja
na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha naye.
63
64. Au nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha? Na nani anaye
kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu? Sema: Leteni hoja zenu kama nyinyi ni wasema kweli.
64
65. Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipo kuwa
Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa.
65
66. Kwani huo ujuzi wao umefikilia kuijua Akhera? Bali wao wamo katika
shaka nayo tu, bali wao ni vipofu nayo.
66
67. Na wakasema walio kufuru: Tutapo kuwa mchanga, sisi na baba zetu,
hivyo kweli tutakuja tolewa?
67
68. Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya
ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale.
68
69. Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje mwisho wa wakosefu.
69
70. Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila
zao wanazo zifanya.
70
71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema kweli?
71
72. Sema: Asaa ni karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayo yahimiza.
72
73. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa watu, lakini
wengi wao hawashukuru.
73
74. Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha vifua vyao na
wanayo yatangaza.
74
75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kinacho
bainisha.
75
76. Hakika Qur'ani hii inawasimulia Wana wa Israili mengi wanayo
khitalifiana nayo.
76
77. Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini.
77
78. Hakika Mola wako Mlezi atawahukumu kwa hukumu yake, naye ni Mwenye
nguvu Mjuzi.
78
79. . Basi mtegemee Mweneyezi Mungu; hakika wewe uko juu ya Haki iliyo
wazi.
79
80. Kwa hakika wewe huwezi kuwafanya maiti wasikie, wala kuwafanya
viziwi wasikie wito, wanapo kwisha geuka kwenda zao.
80
81. Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao. Huwezi kuwafanya
wasikie isipo kuwa wenye kuziamini Ishara zetu; na hao ndio wat'iifu.
81
82. Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi
atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana na yakini na Ishara zetu.
82
83. Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi katika wanao kadhibisha
Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu.
83
84. Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je! Nyinyi si mlizikanusha
Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?
84
85. Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo dhulumu. Basi
hao hawatasema lolote.
85
86. Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili watulie, na mchana
wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
86
87. Na Siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika waliomo mbinguni
na katika ardhi, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni
wanyonge.
87
88. Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo
wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila
kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.
88
89. Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika
na mahangaiko ya Siku hiyo.
89
90. Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao Motoni.
Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?
90
91. Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu aliye ufanya
ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni
mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.
91
92. Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida
ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa
waonyaji.
92
93. Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi si mwenye
kughafilika na myatendayo.
93
Sura Nyingine | Faharasa |