29.Suurat Al A'nkabut |
Imeshuka Makka | Ina aya 69 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Alif Lam Mim (A.L.M.)1
2. Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao
wasijaribiwe?
1
3. Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi
Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.
3
4. Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya
hiyo wanayo hukumu.
4
5. Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi
ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye
kujua.
5
6. Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili
ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.
6
7. Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa
yao, na tutawalipa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
7
8. Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa
watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii.
Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
8
9. Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni
mwa watu wema.
9
10. Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini
wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu
kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola
wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu
hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu?
10
11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na
atawatambulisha wanaafiki.
11
12. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi
tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote
kile. Hakika hao ni waongo.
12
13. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja
na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa
wakiyazua.
13
14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu
kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu.
14
15. Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya
kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote.
15
16. Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu,
na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua.
16
17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na
mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini
riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na
mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa.
17
18. Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha
kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi.
18
19. Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji,
na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
19
20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha
uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
20
21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa.
21
22. Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu.
Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
22
23. Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye,
hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu
chungu.
23
24. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni
moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara
kwa watu wanao amini.
24
25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi
Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku
ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi.
Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
25
26. Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi.
Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
26
27. Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika
dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye
hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.
27
28. Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya
uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo.
28
29. Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika
mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa
kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao
kweli.
29
30. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa!
30
31. Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika
sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika
wamekuwa madhaalimu.
31
32. Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi
nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa
mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
32
33. Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao,
na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike.
Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa
watao kaa nyuma.
33
34. Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka
mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya.
34
35. Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia
akili zao.
35
36. Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi
watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende
katika ardhi mkifisidi.
36
37. Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa
ndani ya nyumba zao nao wamefudikia.
37
38. Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana
na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia,
na hali walikuwa wenye kuona.
38
39. Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara
waziwazi, lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda.
39
40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao
wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa
na ukelele; na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati
yao wapo tulio wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu,
lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao.
40
41. Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano
wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote
ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.
41
42. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho kiomba badala
yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
42
43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye
ilimu.
43
44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika
hayo ipo Ishara kwa Waumini.
44
45. SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala
inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu
ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.
45
46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri
kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini
yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu
wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
46
47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale
tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa
(washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa
makafiri.
47
48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika
kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu.
48
49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio
pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu.
49
50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake
Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji
mwenye kubainisha tu.
50
51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki
wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao
amini.
51
52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na
nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu
na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.
52
53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana
wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea
kwa ghafla, na hali wao hawana khabari.
53
54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa
hakika imewazunguka makafiri!
54
55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu
yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda!
55
56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa.
Basi niabuduni Mimi peke yangu.
56
57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.
57
58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka
katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo.
Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao.
58
59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
59
60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi
Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye
kujua.
60
61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua
na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi
basi wanako geuzwa?
61
62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye
katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
62
63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na
akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi
Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali
wengi katika wao hawafahamu.
63
64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo.
Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua!
64
65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa
kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha.
65
66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja
jua!
66
67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na
hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu,
na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa?
67
68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi
Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa
makaazi ya makafiri?
68
69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye
njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.
69
Sura Nyingine | Faharasa |