33.Al-Ah'zab |
Imeshuka Madina | Ina aya 73 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
1
2. Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi.
Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.
1
3. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni
wa kutegemewa.
3
4. Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani
ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo
yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto
wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu
tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia.
4
5. Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki
zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika
yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
5
6. Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake
ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi
Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki
zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni.
6
7. Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim
na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu,
7
8. Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia
makafiri adhabu chungu.
8
9. Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu
yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi
msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
9
10. Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho
yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu
dhana mbali mbali.
10
11. Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali.
11
12. Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao:
Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.
12
13. Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa
Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba
ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa
tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.
13
14. Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa
kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu.
14
15. Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba
hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.
15
16. Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa,
na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.
16
17. Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni
uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo
kuwa Mwenyezi Mungu.
17
18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao
waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.
18
19. Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho
yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu
ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri.
Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na hayo
kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
19
20. Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo
makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza
khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu.
20
21. Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu
kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi
Mungu sana.
21
22. Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema
kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu.
22
23. Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na
Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala
hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.
23
24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao,
na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
24
25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu
yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini
katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.
25
26. Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa
Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi
yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka.
26
27. Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi
msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
27
28. Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na
pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano
mzuri.
28
29. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera,
basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo
makubwa.
29
30. Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu,
atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
30
31. NA MIONGONI mwenu atakeye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki
ya ukarimu.
31
32. Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine.
Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi
katika moyo wake. Na semeni maneno mema.
32
33. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya
kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu,
enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara.
33
34. Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi
Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na
Mwenye khabari.
34
35. Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume
na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao
kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu
wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga
wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na
wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu
amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.
35
36. Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari
katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo
lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea
upotofu ulio wazi.
36
37. Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha:
Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo
taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu
ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza
wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga
watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Mwenyezi
Mungu ni yenye kutekelezwa.
37
38. Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu.
Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi
Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa.
38
39. (Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi Mungu
na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu.
39
40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume
wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila
kitu.
40
41. Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru.
41
42. Na mtakaseni asubuhi na jioni.
42
43. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani
mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.
43
44. Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salama! Na amewaandalia
malipo ya ukarimu.
44
45. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na
mwonyaji,
45
46. Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye
kutoa nuru.
46
47. Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka
kwa Mwenyezi Mungu.
47
48. Wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe
mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
48
49. nyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa t'alaka
kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni
cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema.
49
50. Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na
ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu,
na mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba
zako, na mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke
Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa.
Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia
wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili
isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
50
51. Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze
umtakaye. Na kama ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya
hivi kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi
juu ya kile unacho wapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni
mwenu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
51
52. Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha
kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule uliye mmiliki
kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu.
52
53. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda
kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha
kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii
naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na
mnapo wauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi
zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa
Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo
ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
53
54. Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
54
55. Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala watoto
wao, wala ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa ndugu
zao wanawake, wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao
ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kushuhudia kila kitu.
55
56. Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi
mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu.
56
57. Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu
amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehi.
57
58. Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya
kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri.
58
59. Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini
wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
59
60. Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao
fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao,
kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.
60
61. Wamelaanika! Popote watakapo onekana watakamatwa na watauliwa
kabisa.
61
62. Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita zamani.
Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu.
62
63. Watu wanakuuliza khabari ya Saa (ya Kiyama). Sema: Ujuzi wake
uko kwa Mwenyezi Mungu. Na nini kitakujuvya? Pengine hiyo Saa iko karibu.
63
64. Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto
unao waka kwa nguvu.
64
65. Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru.
65
66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema:
Laiti tungeli mt'ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt'ii Mtume!
66
67. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwat'ii bwana zetu
na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia.
67
68. Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana
kubwa.
68
69. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio mtaabisha Musa, lakini
Mwenyezi Mungu akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima
mbele ya Mwenyezi Mungu.
69
70. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa.
70
71. Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi
yenu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa
mafanikio makubwa.
71
72. Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima;
na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua.
Hakika yeye amekuwa dhaalimu mjinga.
72
73. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anawaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki
wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na anawapokelea
toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
73
Sura Nyingine | Faharasa |