4.Surat An-Nisaai |
Imeshuka Makka | Ina aya 176 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi
moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na
wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu
ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwaangalieni.
1
2. Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri.
Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa.
2
3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni
mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa
hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia
imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.
3
4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni
kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha.
4
5. Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia
yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno
mazuri.5
6. Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni
wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja
kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi
naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi
Mungu anatosha kuwa Mhasibu.
6
7. Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio
karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa
walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa.
7
8. Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini,
wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno mema.
8
9. Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao
watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme
maneno yaliyo sawa.
9
10. Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote
wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.
10
11. Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume
ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi
watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke
ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao
apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na
wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi
moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada
ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi
hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni
Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
na Mwenye hikima.
11
12. Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto.
Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia
waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa
hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha,
baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke
anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu
mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko
hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au
kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
12
13. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu
humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
13
14. Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia
mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu
ya kudhalilisha.
14
15. Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni
watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka
wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine.
15
16. Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea
basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye
kurehemu.
16
17. Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao
uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia
toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima.
17
18. Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao
mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao
kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
18
19. Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu.
Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa wakifanya
uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda
mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
19
20. Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa
chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua
kwa dhulma na kosa lilio wazi?
20
21. Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi,
na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?
21
22. Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo kwisha pita.
Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya.
22
23. Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi
zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama
zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu,
na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu
mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia
mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa
pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
23
24. NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa na mikono
yenu ya kulia. Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mmehalilishiwa
wasio kuwa hao, mtafute kwa mali yenu kwa kuowa pasina kuzini. Kama mnavyo
starehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni waajibu. Wala hapana lawama
juu yenu kwa mtakacho kubaliana baada ya kutimiza waajibu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua na Mwenye hikima.
24
25. Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana
Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa
wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama
ada, wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa
kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo
wekewa waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anaye ogopa kuingia katika
zina. Na mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
na Mwenye kurehemu.
25
26. Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo
za walio kuwa kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu wake. Na Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
26
27. Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na
wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.
27
28. Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanaadamu ameumbwa
dhaifu.
28
29. Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe
biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwarehemuni.
29
30. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi huyo tutamwingiza
Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
30
31. Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo,
na tutakuingizeni mahali patukufu.
31
32. Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko
wengine. Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana fungu
katika walio vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
32
33. Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo yaacha wazazi
wawili na jamaa. Na mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
33
34. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi
Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi wanawake
wema ni wale wenye kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi
Mungu ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu wanasihini,
muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia ya kuwaudhi
bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.
34
35. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni
muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke.
Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye khabari.
35
36. Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na
wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani
wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio
milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye
kiburi wanao jifakhiri,
36
37. Ambao wanafanya ubakhili na wanaamrisha watu ubakhili, na wanaficha
fadhila alizo wapa Mwenyezi Mungu. Na tumewaandalia makafiri adhabu ya
fedheha,
37
38. Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala hawamuamini
Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa ndiye
rafiki yake, basi ana rafiki mbaya mno.
38
39. Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu? Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema.
39
40. Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu hata uzito wa chembe moja. Na
ikiwa ni jambo jema basi Yeye hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo
makubwa.
40
41. Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma shahidi, na
tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa?
41
42. Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe
juu yao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote.
42
43. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue
mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka mkoge.
Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa
wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu
na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria.
43
44. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue
mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka mkoge.
Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa
wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu
na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria.
44
45. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na Mwenyezi Mungu
anatosha kuwa ni Mlinzi, na anatosha kuwa ni Mwenye kukunusuruni.
45
46. Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala
pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikilizwa. Na
husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili kuitukana Dini. Na lau
kama wangeli sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na "Undhurna" (Utuangalie),
ingeli kuwa ni kheri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewalaani
kwa kufuru yao; basi hawaamini ila wachache tu.
46
47. Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha yenye kusadikisha
yale mliyo nayo, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au tukawalaani
kama tulivyo walaani watu wa Sabato (Jumaamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu
ni lazima ifanyike
47
48. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo
duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika
amezua dhambi kubwa
48
49. Jee huwaoni wale wanao dai kuwa ati wametakasika? Bali Mwenyezi
Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kadiri ya kijiuzi kilichomo
ndani ya uwazi wa kokwa ya tende
49
50. Tazama vipi wanavyo mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na haya yatosha
kuwa dhambi iliyo dhaahiri.
50
51. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu
na Shet'ani! Na wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi katika
njia kuliko Walio amini.
51
52. Hao ndio Mwenyezi Mungu amewalaani. Na ambaye Mwenyezi Mungu
amemlaani basi hutamwona kuwa na mwenye kumnusuru
52
53. Au wanayo sehemu ya utawala? Basi hapo wasingewapa watu hata
tundu ya kokwa ya tende.
53
54. Au wanawahusudu watu kwa yale aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila
yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hikima na tukawapa utawala
mkubwa.
54
55. Basi wapo miongoni mwao waliyo yaamini, na wapo walio yakataa.
Na Jahannamu yatosha kuwa ni moto wa kuwateketeza
55
56. Hakika wale walio zikataa Ishara zetu tutawaingiza Motoni. Kila
zitapo wiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine ili waionje hiyo
adhabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
56
57. Na wale walio amini na wakatenda mema tutawaingiza katika Pepo
zipitazo mito kati yake kwa kudumu humo milele. Huko watakuwa na wake walio
takasika, na tutawaingiza katika vivuli vizuri kweli.
57
58. Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe.
Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini
Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia,
Mwenye kuona.
58
59. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na
wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni
kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
59
60. Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa
kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya
upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea
mbali
60
61. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu, na njooni kwa Mtume; utawaona wanaafiki wanakukwepa kwa upinzani
61
62. Basi inakuwaje unapo wasibu msiba kwa sababu ya yale iliyo tanguliza
mikono yao? Hapo tena hukujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hatukutaka
ila wema na mapatano
62
63. Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo ndani ya
nyoyo zao. Basi waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri
na kuingia katika nafsi zao.
63
64. Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na lau pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia, wakamwomba
Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangeli
mkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
64
65. La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe
ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika
nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.
65
66. Na lau kuwa tumewaamrisha: Jiueni, au tokeni majumbani kwenu,
wasingeli fanya hayo ila wachache tu miongoni mwao. Na lau kama wangeli
fanya walio waidhiwa ingeli kuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi.
66
67. Na hapo tunge wapa malipo makubwa kutoka kwetu
67
68. Na tungeli waongoa Njia iliyo nyooka.
68
69. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale
alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi,
na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!
69
70. Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi wa kutosha.
70
71. Enyi mlio amini! Chukueni hadhari yenu! Na mtoke kwa vikosi au
tokeni nyote pamoja!
71
72. Na yupo kati yenu anaye bakia nyuma; na ukikusibuni msiba husema:
Mwenyezi Mungu kanifanyia kheri sikuwa nao.
72
73. Na yupo kati yenu anaye bakia nyuma; na ukikusibuni msiba husema:
Mwenyezi Mungu kanifanyia kheri sikuwa nao.
73
74. Basi nawapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanao
uza uhai wa dunia kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu
kisha akauliwa au akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.
74
75. Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale
wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu!
Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na
mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako
75
76. Walio amini wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio
kufuru wanapiana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shet'ani.
Hakika hila za Shet'ani ni dhaifu
76
77. Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike
Sala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao
liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi.
Na wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge
tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo,
na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata
uzi wa kokwa ya tende.
77
78. Popote mlipo mauti yatakufikieni, na hata mkiwa katika ngome
zilizo na nguvu. Na likiwafikilia jema wanasema: Hili limetoka kwa Mwenyezi
Mungu. Na likiwafikilia ovu wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema: Yote
yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii
kufahamu maneno?
78
79. Jema lilio kufikia limetokana na Mwenyezi Mungu. Na ovu lilio
kusibu linatokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni Mtume.
Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kutosha.
79
80. Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu. Na anaye
kengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao
80
81. Na wanasema: Tunat'ii. Lakini wanapo toka kwako kundi moja miongoni
mwao hupanga njama usiku kinyume na unayo yasema. Na Mwenyezi Mungu anayaandika
yote hayo wanayo yapangia njama za usiku. Basi waachilie mbali, na umtegemee
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.
81
82. Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye
kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi
82
83. Na linapo wafikia jambo lolote lilio khusu amani au la kitisho
wao hulitangaza. Na lau kuwa wangeli lipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka
kati yao, wale wanao chunguza wangeli lijua. Na lau kuwa si fadhila ya
Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngeli mfuata Shet'ani ila wachache
wenu tu.
83
84. Basi pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Hukalifishwi ila nafsi
yako tu. Na wahimize Waumini. Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulio
ya walio kufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mkali zaidi wa kushambulia na
Mkali zaidi wa kuadhibu.
84
85. Mwenye kusaidia msaada mwema ana fungu lake katika hayo, na mwenye
kusaidia msaada mwovu naye ana sehemu yake katika hayo. Na hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye uweza na ujuzi juu ya kila kitu..
85
86. Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo
bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuhisabu kila kitu.
86
87. Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Kwa yakini atakukusanyeni
Siku ya Kiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani msema kweli kuliko Mwenyezi
Mungu?
87
88. Mmekuwaje kuwa makundi mawili kwa khabari ya wanaafiki, na hali
Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyo yachuma? Je! Mnataka
kumwona mwongofu ambaye Mwenyezi Mungu amemhukumu kuwa kapotea? Na aliye
mhukumu Mwenyezi Mungu kuwa amekwisha potea wewe hutampatia njia
88
89. Wanapenda lau kuwa nanyi mnge kufuru kama walivyo kufuru wao,
ili muwe sawa sawa. Basi msiwafanye marafiki miongoni mwao mpaka wahame
kwa ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na wakikengeuka basi wakamateni na
wauweni popote mnapo wapata. Wala msimfanye rafiki katika wao wala msaidizi
89
90. Isipokuwa wale walio fungamana na watu ambao mna ahadi baina
yenu na wao, au wanakujieni na vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi, au
kupigana na watu wao. Na lau angeli penda Mwenyezi Mungu angeli wasaliti
juu yenu wakapigana nanyi. Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na
wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao
90
91. Mtawakuta wengine wanataka wapate salama kwenu na salama kwa
watu wao. Kila wakirudishwa kwenye fitna hudidimizwa humo. Ikiwa hawajitengi
nanyi, na wakakuleteeni salama, na wakazuia mikono yao, basi wakamateni
na wauweni popote mnapo wakuta. Na juu ya hao ndio tumekupeni hoja zilizo
wazi
91
92. Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa
Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa
jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa
wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini.
Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe
diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge
miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi na Mwenye hikima.
92
93. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni
Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani,
na amemuandalia adhabu kubwa.
93
94. Enyi mlio amini! Mnapo safiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu basi
hakikisheni, wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si Muumini; kwa
kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu
zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi
Mungu akakuneemesheni. Basi chunguzeni sawa sawa. Hakika Mwenyezi Mungu
anazo khabari za mnayo yatenda
94
95. Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu wala hawanadharura, na wale
wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi
Mungu amewatukuza cheo wale wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao kuliko
wale wanao kaa tu. Ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi wote mashukio mema,
lakini Mwenyezi Mungu amewafadhili wanao pigana kwa ujira mkubwa kuliko
wanao kaa tu.
95
96. Ni vyeo hivyo vinavyo toka kwake, na maghfira na rehema. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu.
96
97. Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao wamejidhulumu
nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani
ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makaazi
yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa.
97
98. Isipo kuwa wale walio kuwa wanyonge miongoni mwa wanaume na wanawake
na watoto wasio na uweza wa hila ya kuongoza njia ya kuhama.
98
99. Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa maghfira
99
100. Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi
duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anaye toka nyumbani kwake kuhama
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani
basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu
100
101. Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha
Sala, iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi. Hakika
makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.
101
102. Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni
mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida
zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali,
lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru
wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio
wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua
au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika
Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
102
103. Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa,
na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni Sala kama dasturi.
Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu
103
104. Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui. Ikiwa mnaumia,
basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji kwa Mwenyezi
Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima
104
105. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili upate kuhukumu
baina ya watu kwa alivyo kuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe mtetezi wa
makhaaini.
105
106. Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
106
107. Wala usiwatetee wanao khini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu
hampendi aliye khaaini, mwenye dhambi.
107
108. Wanataka kujificha kwa watu, wala hawataki kujificha kwa Mwenyezi
Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapo panga njama usiku kwa maneno asiyo
yapenda. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema wanayo yatenda.
108
109. Hivyo nyinyi mmewatetea hawa katika uhai huu wa duniani. Basi
nani atakaye watetea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani atakuwa
wakili wao wa kumtegemea?
109
110. Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba
maghfira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira,
Mwenye kurehemu.
110
111. Na anaye chuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake mwenyewe.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
111
112. Na atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa,
basi amejitwika dhulma na dhambi iliyo wazi.
112
113. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema
yake, kundi moja kati yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi ila
nafsi zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia
Kitabu na hikima na amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi
Mungu zilizo juu yako ni kubwa.
113
114. Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa siri, isipo
kuwa kwa yule anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha
baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu,
basi tutakuja mpa ujira mkubwa
114
115. Na anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu, na akafuata
njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na tutamuingiza
katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu.
115
116. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini
Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi
Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali.
116
117. Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi
ila Shet'ani aliye asi.
117
118. Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shet'ani alisema: Kwa yakini
nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako.
118
119. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha,
basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo
umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi wake badala
ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri.
119
120. Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi ila udanganyifu.
120
121. Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati makimbilio kutoka
humo.
121
122. Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza katika Bustani
zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi
Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu
122
123. Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa Kitabu! Anaye
fanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatajipatia mlinzi wala wa kumnusuru,
isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
123
124. Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini
- basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya
kokwa ya tende.
124
125. Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye usilimisha uso
wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya Ibrahim
mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani.
125
126. Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo
duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.
126
127. Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu ana
kutoleeni fatwa juu yao, na mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu mayatima
wanawake ambao hamwapi walicho andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu
wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na
kheri yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu anaijua.
127
128. Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi
si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa
machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika
Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
128
129. Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia.
Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliye tundikwa.
Na mkisikizana na mkamchamngu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira
na Mwenye kurehemu.
129
130. Na wakitengana Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja katika
wao kwa ukunjufu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu Mwenye hikima.
130
131. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote viliomo katik mbingu na viliomo
katika dunia. Na kwa hakika tuliwausia walio pewa Kitabu kabla yenu, na
nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu. Na mkikataa, basi ni vya Mwenyezi
Mungu viliomo mbinguni na viliomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi,
anajitosha, na Msifiwa.
131
132. Na ni vya Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na viliomo katika
ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi.
132
133. Akitaka atakuondoeni, enyi watu! Na awalete wengineo. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa hayo
133
134. Anaye taka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo
ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
134
135. Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi
wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu anawastahikia
zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa
au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayo yatenda.
135
136. Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na
Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha
kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu
vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali.
136
137. Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha
wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaghufiria wala wa kuwaongoa
njia.
137
138. Wabashirie wanaafiki kwamba watapata adhabu chungu,
138
139. Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki badala ya Waumini.
Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi
Mungu.
139
140. Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnapo
sikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae
pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi
mfano wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri
wote pamoja katika Jahannamu.
140
141. Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao toka kwa Mwenyezi
Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni sehemu ya
makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni, nasi
tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu
Siku ya Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda
Waumini.
141
142. Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye
ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa unyong'onyo,
wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo
tu.
142
143. Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko hawako.
Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia njia.
143
144. Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio marafiki badala
ya Waumini. Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi juu yenu?
144
145. Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini kabisa Motoni,
wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.
145
146. Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na wakashikamana
na Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi hao ni
pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa.
146
147. Mwenyezi Mungu hakuadhibuni mkimshukuru na mkamuamini. Na Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani na ndiye Mwenye kujua.
147
148. MWENYEZI MUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa mwenye
kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
148
149. Mkidhihirisha wema au mkiuficha, au mkiyasamehe maovu, hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Muweza.
149
150. Hakika wale wanao mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanataka
kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa kusema: Wengine
tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia iliyo kati
kati ya haya.
150
151. Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia makafiri adhabu ya
kudhalilisha.
151
152. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala wasimfarikishe
yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
maghfira, na Mwenye kurehemu
152
153. Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshia kitabu kutoka mbinguni.
Na kwa hakika walikwisha mtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walisema: Tuonyeshe
Mwenyezi Mungu wazi wazi. Wakapigwa na radi kwa hiyo dhulma yao. Kisha
wakamchukua ndama kumuabudu, baada ya kwisha wajia hoja zilizo wazi. Nasi
tukasamehe hayo, na tukampa Musa nguvu zilizo dhaahiri.
153
154. Na tukanyanyua mlima juu yao kwa kufanya agano nao. Na tukawaambia:
Ingilieni mlangoni kwa unyenyekevu. Na tukawaambia: Msiivunje Siku ya Sabato
(Jumaa mosi). Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti.
154
155. Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi zao, na kuzikataa kwao
ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na kusema
kwao: Nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa kufuru
zao, basi hawaamini ila kidogo tu
155
156. Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu uwongo mkubwa.
156
157. Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu,
Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa
tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao
hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa
yakini
157
158. Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
158
159. Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla
ya kufa kwake. Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao
159
160. Basi kwa dhulma yao Mayahudi tuliwaharimishia vitu vizuri walivyo
halalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia ya Mwenyezi
Mungu.
160
161. Na kuchukua kwao riba, nao wamekatazwa, na kula kwao mali ya
watu kwa dhulma. Basi tumewaandalia makafiri katika wao adhabu yenye uchungu.
161
162. Lakini walio bobea katika ilimu miongoni mwao, na Waumini, wanayaamini
uliyo teremshiwa wewe, na yaliyo teremshwa kabla yako. Na wanao shika Sala,
na wakatoa Zaka, na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho - hao
tutawapa malipo makubwa.
162
163. Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi
Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na
Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na
Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.
163
164. Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine
hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno.
164
165. Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja
juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
nguvu, Mwenye hikima.
165
166. Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyo kuteremshia wewe.
Ameyateremsha kwa kujua kwake - na Malaika pia wanashuhudia. Na Mwenyezi
Mungu anatosha kuwa shahidi.
166
167. Hakika walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, wamekwisha
potelea mbali.
167
168. Hakika wale walio kufuru na wakadhulumu hawi Mwenyezi Mungu
kuwasamehe wala kuwaongoa njia.
168
169. Isipo kuwa njia ya Jahannamu. Humo watadumu milele. Na hayo
kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
169
170. Enyi Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki itokayo kwa
Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo kheri yenu. Na mkikakanusha basi hakika
viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu tu. Na hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima
170
171. Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme
Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu
ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na
ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake.
Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote
viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa
kutosha
171
172. Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala
Malaika walio karibishwa. Na watakao ona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu
na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.
172
173. Na ama walio amini na wakatenda mema atawalipa ujira wao sawa
sawa, na atawazidishia kwa fadhila yake. Na ama wale walio ona uvunjifu
na wakafanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu iliyo chungu. Wala hawatopata
mlinzi wala wa kuwanusuru asiye kuwa Mwenyezi Mungu.
173
174. Enyi watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi.
Na tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi.
174
175. Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu, na wakashikamana naye,
basi atawatia katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa kwenye Njia
Iliyo Nyooka.
175
176. Wanakuomba uhukumu, sema: Mwenyezi Mungu anakupeni hukumu juu
ya mkiwa. Ikiwa mtu amekufa, naye hana mtoto, lakini anaye ndugu wa kike,
basi huyo atapata nusu alicho acha maiti. Na mwanamume atamrithi ndugu
wa kike ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni ndugu wa kike wawili, basi watapata
thuluthi mbili za alicho acha maiti. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake,
basi mwanamume atapata sehemu iliyo sawa na ya wanawake wawili. Mwenyezi
Mungu anakubainishieni ili msipotee; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila
kitu.176
Sura Nyingine | Faharasa |