49.Suuratul Al H'ujuraat |
Imeshuka Madina | Ina aya 18 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Enyi mlio amini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia,
Mwenye kujua.
1
2. Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii,
wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi, visije
vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui.
2
3. Kwa hakika wanao teremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Hao
watakuwa na maghfira na ujira mkubwa.
3
4. Hakika hao wanao kuita nawe uko nyuma ya vyumba, wengi wao hawana
akili.
4
5. Na lau wao wangeli ngojea mpaka uwatokee ingeli kuwa kheri kwao.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.
5
6. Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni,
msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo
yatenda.
6
7. Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nanyi. Lau angeli kut'iini
katika mambo mengi, bila ya shaka mngeli taabika. Lakini Mwenyezi Mungu
amekupendezeeni Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amekufanyeni
muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walio ongoka,
7
8. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
8
9. Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni.
Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu
mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni
kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao
hukumu kwa haki.
9
10. Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu,
na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
10
11. Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake
wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane
hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya
baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu.
11
12. Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya
dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi.
Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia
hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea
toba, Mwenye kurehemu.
12
13. Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na
mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika
aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu
zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
13
14. Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni:
Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
14
15. Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi
Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.
15
16. Sema: Ati ndio mnamfundisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali
Mwenyezi Mungu anayajua ya katika mbingu na ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua
kila kitu?
16
17. Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu
kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni hisani kwa kukuongoeni
kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.
17
18. Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi
Mungu anayaona myatendayo.
18
Sura Nyingine | Faharasa |