KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 

NENO LA CHUO KIKUU KITUKUFU CHA AL AZHAR 
KATIKA KUKADIMISHA NA KUSIFU


Ni jambo kuu kwa mtu kuleta utangulizi mbele ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu ambacho "Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake" kwani hicho "kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa." (Sura Fussilat Aya 42). Hapana mtu ambaye amekifanyia ikhlasi (Kitabu hichi) kwa kukijua na kukitenda ila hupata mafanikio ya duniani na akhera. Na hapana ajabu ya hayo kwani kheri yake ni kheri yenye kukusanya kheri zote za Mitume na Manabii wote: "Na pale  Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii: Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie.   Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: 'Tumekubali.  Akasema: Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia  Watakao geuka baada ya haya, basi hao ndio wapotovu." (Sura Al I'mran Aya 81, 82)
Ilivyo kuwa "Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu" (Al I'mran Aya 19), basi Qur'ani ndiyo Katiba ya Uislamu. Na kwa hivyo Uislamu ndiyo hii kheri iliyo bebwa na Qur'ani kwa faida ya wanaadamu wote. Na kheri ya Uislamu inaonekana katika Sharia yake ambayo anaijua kila mwenye kuisoma kuwa ama ni ya kuleta manufaa ya kuwaenea watu wote au kukinga uharibifu wa kuwateketeza walimwengu. Kwa hivyo imekuwa mwenye Kuisoma Qur'ani na akaifunza inakuwa ndiyo anaitia kuleta manufaa na anafanya kazi ya kukinga uharibifu. Kwa hivyo basi anakuwa ni miongoni mwa bora ya watu ambao wanastahiki kauli ya Nabii wa Rehema Muhammad s.a.w. alipo sema: "Mbora wa watu ni yule awafaao mno watu" Na yote haya yanafafanua maana ya hadithi ya Mteuliwa s.a.w. alipo sema: "Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Qur'ani na akawafunza watu."
Na Al Azhar Tukufu itaselelea kuwa ni bora ya taasisi za ilimu, na yenye manufaa kabisa kuliko zote, maadamu inashikilia ahadi yake na mwendo wake kusimamia utumishi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ilimu zake,  kwa kufundisha na kutenda. Na Waislamu wote wa karibu na wa mbali wanashuhudia hayo kwa zile kheri wanazo zipata kutokana na wanazuoni wake wenye kufanya kazi   kila kipembe katika ncha za ulimwengu.
Manufaa haya na kheri hizo hupatikana kwa vile Al Azhar tukufu ilivyo kuwa inasimamia Wito wa kheri kama inavyo onekana katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wawepo kutokana na nyinyi umma wanao lingania kheri na wanao amrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio watakao fanikiwa."
Basi imekuwa Al Azhar Tukufu -- na taarikhi (historia) inashuhudia -- ndio huo umma unao tajwa.
Kutarjimu maana za Qur'ani Tukufu na kuifasiri katika lugha nyengine ni moja ya njia hizo za Daa'wa (Wito) huo. Na hii hapa Al Azhar Tukufu imeshika moja ya njia mbili, ama inafanya tarjama au inashughulikia kusahihisha ikiwa yapo makosa yoyote. Katika ya yaliyo khusiana na tarjama hii ya Kiswahili Al Azhar Tukufu imeshika hiyo njia ya pili, ya kusahihisha.
Na mimi nimeona sharaf mwaka 1414 A.H. (1993 B.K.) ilipo nitaka Al Azhar niipitie tarjama ya maana ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili1  aliyo itarjimu  mtarjimu mwenye uwezo,  Bwana Ali Muhsin Al Barwani.2
Basi nikasimama kufanya kazi hiyo pamoja na wenzangu wa Al Azhar, walimu wa lugha ya Kiswahili katika Sehemu ya Lugha za Kiafrika katika Chuo cha Lugha na Tarjama katika Chuo Kikuu cha Al Azhar, nao ni: Dk Ali Shaaban, na Dk Mustafa Husein Al Halugi na Dk Abdul Hadi Marzooq. Tumeipitia tarjama hii mara tatu, mara ya kwanza kutoa makosa, mara ya pili kupitia matengenezo ya makosa, na mara ya tatu kupitia yale mapitio tena ya masahihisho.
Na Idara ya Utafiti na Utungaji na Tarjama katika Mkusanyo wa Tafiti za Kiislamu katika Al Azhar Tukufu -- na khasa wa kutajika Mkurugenzi wake  Mkuu,  Bwana Fat-hallah Yasin Jazar na mwakilishi wake bingwa mheshimiwa Bwana Muhammad Omar -- wawili hao ndio walio kuwa viungo wa kuunganisha baina yetu na upigishaji chapa. Kiungo hichi kikawa hakipumziki wala hakichoki kufuatiliza kazi ya utiriri ya mfululizo. Kwa hakika hao walikuwa kweli ni kiungo kisicho katika kabisa.
Na hii tarjama  iliyopo mikononi mwetu ina sahifa elfu na mia nne na sabiini na tisa. Imekusanya -- pamoja na maana ya Qur'ani Tukufu -- tafsiri yake, yaani maelezo yake, vile vile. Mwenye kuisoma Tarjama hii na mwenye kufungua Kitabu hichi ataona mbele ya kila aya tarjama yake upande wa kushoto, na inafuatia Tafsiri yake (yaani maelezo) yake chini ya kila sahifa.
Tunapenda kutaja kuwa hiyo Tafsiri ya Kiswahili tuliyo itaja kuwa iko chini ya kila Aya, hiyo ni tarjama ya  Kitabu cha Tafsiri cha Kiarabu kiitwacho "AL MUNTAKHAB" ambacho kimetengenezwa na Halmashauri (Kamiti) ya Qur'ani na Sunna ya Baraza Kuu la Mambo ya Kiislamu pamoja na Wizara ya Wakfu ya Misri. Na hii ni Tafsiri waliyo ikubali Waislamu wa kila nchi katika dunia bila ya pingamizi. Hata tangulizi alizo zitanguliza huyu mwenye kutarjimu mbele ya kila Sura, na pia yaliyo ongezwa pembezoni ambayo huenda yakakutikana katika baadhi ya sahifa ili kutilia mkazo au kuzidi kueleza jambo fulani, -- hayo pia yote ni tarjama ya maneno yaliyo tiwa kwa uaminifu yaliyomo katika hicho kitabu "AL MUNTAKHAB".  Hali kadhaalika mtarjimu huyu hakuacha kitu chochote kiliomo katika kitabu cha "AL MUNTAKHAB", ila amekitaja, na yeye pia hakuzidisha kitu juu yake.
Na haya yametufanya sisi tuwatake Waislamu wa Kiswahili watue nyoyo zao kwa tarjama hii aminifu, na waitegemee kwa kuyapata wanayo yataka kuyapata. Kwani hii "AL MUNTAKHAB", kama isemavyo Halmashauri ya Qur'ani na Sunna ya Al Azhar Tukufu3 : imekuja "kwa njia za kisasa, nyepesi, iliyo kunjuka, yenye ibara wazi, mukhtasari, si tupu wala haichoshi, haina khitilafu za kimadhehebu, wala maneno maneno ya kifundi fundi ya kutatanisha, na kujaza jaza itikadi za maneno, ili iwe katika hali ya kusilihi kutarjumiwa katika lugha nyengine za kigeni, ambazo inatarajiwa wasemao lugha hizo wasome yaliomo katika Qur'ani hii na wafahamu itikadi na misingi, na mafunzo ya kuwaongoza, kutimiza waajibu ulio juu ya shingo zetu, sisi tunao sema lugha ya Kiarabu, nao ni kutarjimu maana ya Qur'ani kwa wasio kuwa Waarabu ili ipate kuwa sahali Ujumbe wa Muhammad kuwafikilia watu wote na wangakhitalifiana ndimi zao na rangi zao."
Hivi basi huyu hapa mtarjimu mzuri, mwenye uwezo, na mtambuzi ni kama kwamba ni mwenye kutimiza yaliyomo katika mausio haya, na hakika ndivyo hivyo alivyo fanya. Furaha iliyoje basi hii!!
Shukrani zote anastahiki Mwenye Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote kwa kuwa Al Azhar Tukufu, Chuo Chake na Msikiti wake, ndiyo iliyo simamia kutunga hichi kitabu na ndiyo iliyo ipitia na kuisahishisha tarjama yake kwa lugha ya Kiswahili.
Haya na Tawfiqi ni kwa Mwenyezi Mungu.

Dk Muhammad Ibrahim Muhammad Abu A'jal
Sehemu ya Lugha za Kiafrika
Chuo cha Lugha na Tarjama
Chuo Kikuu cha Al Azhar
23/5/1415 A.H.
28/10/1994 B.K.


1. Lugha ya Kiswahili ni lugha iliyo enea sana pande mbali mbali katika Afrika ya Mashariki na ya Kati na ya Kusini mbali na baadhi ya visiwa katika Bahari ya Hindi. Na katika mwahali ilipo enea lugha ya Kiswahili ni: Kusini ya Somalia, Kenya, Tanzania, Uganda, Zaire, Ruanda, Burundi, Zambia, Malawi, Msumbiji,  Bukini, Visiwa vya Comoro. Kadhaalika hivi karibuni imeenea mpaka kusini mwa Sudan na baadhi ya pwani za dola za Ghuba ya Arabuni.

 2.  Mtarjimu amezaliwa Zanzibar mwaka 1337 A.H., 1919 B.K. Baada ya kukamilisha masomo yake ya Chuo Kikuu na kujifunza kwa baba yake na Mashekhe wengine masomo ya Kiislamu alifanya kazi kuwa ni Mhandisi wa Zaraa hapo Zanzibar kwa muda wa miaka mitano, kisha akawa Mhariri Mkuu wa gazeti la Mwongozi kwa muda wa miaka kumi na tano.
Tena akawa Waziri wa Ilimu, na wa Mambo ya Ndani, na wa Mambo ya Nje katika Serikali ya kidemokrasia kabla ya kuangushwa serikali hiyo katika mwaka 1383 A.H.,  1964 B.K.  Ameshughulika kuandika vitabu vya Kiislamu na vya ilimu nyenginezo

3.  "Al Muntakhab Fi Tafsiri Al Qur'ani Al Karim", upigaji chapa wa mara ya kumi na saba, Cairo katika mwaka 1413 A.H., 1993 B.K., ukarasa wa "H" na kufuatia. 


Sura Nyingine Faharasa
Chagua Sura Nyingine:

Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com 
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani