Al Fatiha maelezo
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Utangulizi:
Rudi kwenye sura
* 1. Sura inaanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu ambaye hapana anayefaa kuabudiwa
ila Yeye aliye sifika kwa kila sifa za ukamilifu, na ametakasika na kila la upungufu. Yeye ndiye Mwenye
rehema ambaye ananeemesha kwa neema kubwa na ndogo, na za kuwapa wote, na za kuwapa walio khusika.
Na Yeye ndiye mwenye kusifika kwa sifa ya Rehema yenye kudumu. (Kauli ya mwanzo aliyo semezwa
Mtume s.a.w. na kuamrishwa na Mwenyezi Mungu ni "Iqra` bismi Rabbika", yaani: "Soma kwa jina la
Mola wako Mlezi!" Naye Mtume s.a.w. amesema: "Jambo lolote lisilo anziwa kwa Bismillahi ni pungufu."
Kila Sura ya Qur'ani, isipo kuwa Sura Attawba, imeanziwa kwa Bismillahi Rrahmani Rrahim.)
Rudi kwenye sura
* 2. Sifa njema za namna yote na katika kila hali ni za Mwenyezi Mungu pekee. Na
tunamsifu Yeye kwa sifa zote kwa sababu Yeye ndiye mwenye kuviumba viumbe vyote na mwenye
kuviangalia na kuvilea. (Neno Rabb, kwa Kiarabu, lina maana ya Ubwana na Ulezi na Utengenezaji. Ndiyo
tukatumia Mola Mlezi. Neno Baba lina upungufu.)
Rudi kwenye sura
* 3. Na Yeye ndiye Mwenye rehema ya kudumu, na rehema inatokana naye. Ananeemesha
kwa neema zote ndogo na kubwa. (Arrahman ni jina lake Mwenyezi Mungu tu, na hafai mtu kuitwa hivyo.)
Rudi kwenye sura
* 4. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye kumiliki Siku ya Malipo na Hisabu, yaani Siku ya
Kiyama, anafanya atakavyo wala hapana mwenye kushirikiana naye walau kwa kuonekana tu.
Rudi kwenye sura
* 5. Hatumuabudu yeyote ila Wewe tu, wala hatutaki msaada kwa yeyote ila kwako tu.
Rudi kwenye sura
* 6. Tunakuomba utuwafikishe kuendea Njia ya haki, na kheri na mafanikio.
Rudi kwenye sura
* 7. Na njia hiyo ndiyo ya waja wako ulio wawezesha kukuamini Wewe, na
ukawajaalia neema ya uwongofu na radhi, sio njia ya walio stahiki kupata ghadhabu zako na
wakaiwacha njia ya haki na kheri, kwa sababu hao wameitupa imani kukuamini Wewe na kuelekea
kwenye uwongofu wako.
(Hapana katika Vitabu vyote vitakatifu, vya dini zote, dua inayo lingana na hii kwa uzuri wake, na
utimilivu wake. Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu kwa Rehema yake isio na ukomo wala kipimo,
na kumshukuru Mola Mwenye kuviumba na kuviangalia na kuvilea kwa huruma viumbe vyote, na
kuhakikisha kuwa tunajua kuwa hapana Mungu ila Yeye tu wa kuabudiwa na kuombwa msaada, na
kuwa hapana wa kumuingilia katika Ufalme wake na Uwezo wake wa kulipa hisabu kwa kila alitendalo
mtu, hapo tena ndio tunaomba. Na tunaomba nini? Si mkate wa kula, wala riziki yoyote, wala jambo
lolote la manufaa ya kimwili duniani, bali tunaomba Uwongofu kwenye Njia Iliyo Nyooka, Njia ya
kumwendea Yeye Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema. Tunaomba tusiendee njia waliyo ifuata wale
walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kuwa walifunzwa wakajua, lakini kwa chuki na jeuri
wakakataa kuongoka, wala sio njia ya wale ambao labda kwa ujinga wamepotea. Hiyo kwa mukhtasari
ndiyo Dua ambayo Waislamu, wanafunzwa waiombe, na wanaiomba mara kadhaa wa kadhaa katika Sala
zao, na katika kila fursa inapo tokea.)
Rudi kwenye sura
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani